Manispaa Bukoba yaingia ubia na mwekezaji kuipaisha ardhi yake

13May 2016
Crispin Gerald
Bukoba
Nipashe
Manispaa Bukoba yaingia ubia na mwekezaji kuipaisha ardhi yake

Mojawapo ya kero katika mikoa mingi nchini, ni ukosefu wa mipango miji, hali inayochangia makazi holela katika baadhi ya maeneo na inaishia kukwaza uchumi wa nchi.

Kwa mfano, jijini Dar es Salaam hadi sasa asilimia 70 ya eneo lake inadaiwa haijapimwa na iko kiholela.

Kero hiyo ya makazi imeshuhudiwa kwa miaka mingi katkia miji mingi mikubwa, kama vile Dar es Salaam, Mbeya, Tanga, Bukoba, Mwanza, Shinyanga, Tabora na Morogoro.

Mbali na kero ya makazi holela kuleta kadhia machoni mwa jamii, pia msongamano wa makazi umekuwa chanzo kikuu cha kuibuka magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, kifua kikuu, homa ya matumbo na kichocho.

Magonjwa hayo yamekuwa yakichochewa na wakazi wa maeneo husika katika kile kinachodaiwa kuwa ni ukosefu wa maeneo ya kutupa taka na ufinyu wa eneo la kuchimba mtaro wa kupitisha maji machafu ya mvua na yanayotoka majumbani.

Aidha serikali katika miaka ya hivi karibuni kwa kutambua na kubaini ukubwa wa tatizo la ukosefu wa mipango miji imeanza kutengeneza ramani mbalimbali za mipango miji ikiwamo Dar es Salaam, hali inayoashiria kuanza kwa kazi ya upimaji wa maeneo na kutoa hati za viwanja.

Katika moja ya hatua iliyochukuliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba Maendeleo ya Makazi, kukabili hali hiyo ni kubuni mradi maalum iliyouita “Mradi wa Viwanja 20,000.”

Huo ni mradi uliobuniwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 chini ya Mkurugenzi marehemu, Venance Mugemuzi, ambayo iliandaa viwanja 20,000 jijini Dar es Salaam na kuviuza kwa wananchi, kuanzia mwaka 2003.

Miongoni mwa maeneo ambayo viwanja hivyo vilipimwa jijini Dar es Salaam kukabili uhaba huo ni pamoja na Mbweni, Bunju, Boko, Tuangoma, Kivule, Mvuti, Kibada na kadhalika,

Ufadhili wa mradi huo, ulitumia mbinu ya kiuchumi kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia, iliyotumika kufadhili mradi huo na malipo ya deni yanafanyika kwa kukusanya fedha za mauzo ya viwanja.

Kwa mujibu wa Mugemuzi, fedha za Mradi wa ‘Viwanja 20,000’ zilifunguliwa akaunti maalumu na zikawa zinakopeshwa kwa halmashauri nyinginezo kufanya upimaji kama huo.

Miongoni mwa halmashauri zilizokopa na kufanya upimaji wa viwanja, kisha kurudisha fedha hizo za mradi ni mji wa Kibaha na Jiji la Mbeya.

VIWANJA VIPYA BUKOBA

Katika kuunga mkono juhudi za serikali, Halmashauri ya Manispaa Bukoba, imeanza kutekeleza mradi wa upimaji viwanja 5,000 vya mji huo, ambao namna ya upatikanaji wa fungu lake unafanana sana na Mradi wa Viwanja 20,000.

Nguzo ya uchumi wa mradi huo, kama Mradi ya Viwanja 20,000 ilitumia nguzo ya uchumi wa fedha kutoka Benki ya Dunia na halmashauri nyingine baadaye zilikopa fedha kutoka akaunti maalumu ya viwanja hivyo.

Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, imetafuta chanzo kipya cha fedha, kutekeleza Mpango Mkakati wa Mwaka 2008 – 2028, ambayo ni miaka 20.

Mradi huo ulibuniwa na Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Makazi la Umoja wa Mataifa (UN- Habitat0 na unatekelezwa chini ya ufadhili wa taasisi ya serikali ya Unit Trust of Tanzania-Project and Infrastructure Development (UTT-PID).

Shirika hilo limetoa fedha kiasi cha Sh. billion 2.9 kwa ajili ya kugharamia mradi huo.

MADIWANI
Naibu Meya wa Manispaa ya Bukoba, Jimmy Kalugendo, anasema madiwani na watendaji wengine wameshakubaliana kuutekeleza mradi huo uliosimama katika miaka ya nyuma, baada ya kuhusishwa na tuhuma kwamba hazina mwelekekeo wa kusaidia wananchi.

Anautetea kwamba, lengo la mradi huo ni kuhakikisha maeneo ya mji yanapimwa na kutoa hati za umiliki kwa wananchi.

“Tayari wapo wananchi ambao wameonyesha nia ya dhati ya kuhitaji maeneo yaliyopimwa na kupatiwa hati za wilaya,” anasema Naibu Meya - Kalugendo.

“Kimsingi, mradi huu ulibuniwa kwa lengo la kuongeza maeneo yaliyopimwa na yenye hati ikiwa ni hatua ya kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa makazi holela,” anasema na kuongeza:

“Ni hatua ambayo tunaamini itasaidia kuvutia utalii na kuleta mwonekano mzuri wa mji wa Bukoba.”

Kwa mujibu wa Kalugendo, Halmashauri ya Mji Bukoba, iliingia mkataba wa makubaliano na UTT-PID, baada ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kusema haina fedha ya kufadhili mradi huo.

“Ufadhili wa taasisi ya UTT-PID utagharamia uthamini, kulipa fidia na gharama za upimaji wa maeneo,” anasema Kalugendo.

“Historia ya mji wa Bukoba, haijawahi kuwa na mpango mji ambao ungeweza kuelekeza maeneo muhimu ya huduma za jamii, zikiwamo hospitali, shule, masoko, taasisi za kifedha, nyumba za ibada na ofisi za umma katika maeneo yanayoweza kufikika,” anasema.

Kalugendo anafafanua, hadi sasa mradi umefanikiwa kutenga maeneo ya viwanda, ya uwekezaji, na uboreshaji miundombinu duni.

“Mbali na hayo, taasisi hiyo ya UTT-PID ilitoa jumla ya Shilingi milioni 19, ikiwa ni ufadhili wa ujenzi wa maabara ya Shule ya Sekondari Kibeta iliyopo mjini Bukoba,” anafafanua Meya Kalugendo.

Kwa upande wake, diwani mstaafu Dismas Rutagwerera, anasema baada ya kutambua hawana Mpango Mji wa halmashauri hiyo, mwaka 2007 walikutana na watendaji wengine wa halmashauri kuandaa mpango wa mji huo.

“Hitaji la kuwa na mpango mji, lilikuja kulingana na ukweli kuwa, huduma muhimu za jamii hazikuwa rahisi kupatikana kutokana na makazi holela.

“Mradi huo umehusisha vijiji sita vikiwamo Kahoro, Kagondo, Nyanga, Nshambya, Buhembe, Iyunga na Kitendaguo, kijiji ambacho kilikataa mradi huo,” anafafanua diwani huyo.

OFISA ARDHI
Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Bukoba, Geofrey Mwasonjo, anasema mradi umelenga kupima na kutenga maeneo ya makazi, viwanja vya mpira na biashara, maeneo ya wazi na kwenye huduma za jamii.

“Hadi sasa jumla ya hati 480 zimeshatolewa na 240 bado ziko zinashughulikiwa. Kuna jumla ya hati 1,755 zinatarajiwa kutolewa, baada ya malipo yote kukamilika.

“Mbali na faida zote, mradi utawasaidia wananchi kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha, kwa kutumia hati za viwanja.

“Hivyo, mradi utakapokamilika, utakuwa chanzo kimojawapo cha mapato kwa halmashauri kwa kodi ya majengo,” anasema ofisa huyo.

WANANCHI
Mkazi wa Bukoba, Henerico Lushara anasema kuwa mradi huo utawasaidia wakazi kupata mikopo na kujiendeleza kiuchumi kupitia hati zao za viwanja walizopata kutoka katika Halmashauri.

“Mradi huo utasaidia kubadilisha makazi holela ya mji wa Bukoba kuwa na makazi yaliyopangwa vyema,” anasema Lushara.

Kwa upande wake, Edmund Rushekya, ambaye ni mnufaika, anasema kwamba aluimnga mkono mradi huo na anaamini utakapokamilika, untkuwa na manufaa kwa jamii na kwa serikali kwa jumla.

Ombi lake ni kwamba, Halmashauri ya Manispaa Bukoba, iendelee kutekeleza mradi huo, ili kutengeneza maeneo ya utalii na uwekezaji yatakayoleta manufaa kiuchumi kwa kuongeza makusanyo ya mapato.

UTT-PID ni taasisi inayomilikiwa na serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.

Jukumu kuu la taasisi hiyo, ni kuchochea maendeleo ya miradi ya pamoja ya uwekezaji.

Sehemu ya viwanja vipya vya Manispaa ya Bukoba. (PICHA NA TOVUTI YA WADAU BUKOBA)