Wakulima wa Mwani Z’bar walia na bei kuporomoka

13May 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Wakulima wa Mwani Z’bar walia na bei kuporomoka

KILIO cha muda mrefu kwa wakulima wa zao la la mwani Zanzibar, ni bei ndogo ya bidhaa hiyo isiyolingana na ugumu wa kilimo chake, ambacho hufanyika katika ukanda wa Pwani.

Wakulima wa Mwani Z’bar .

Wakulima wa mwani walitarajia ongezeko la bei ya bidhaa hiyo, kwa kuzingatia Zanzibar ni nchi ya tatu duniani inayosafirisha kwa wingi sokoni zao hilo, ikitanguliwa na Ufilipino na Indonesia.

Zanzibar ilianza kilimo cha zao la mwani tangu mwaka 1989. Ikiwa miaka 27 imepita sasa, kuna dalili za wakulima kuanza kukata tamaa ya kunufaika na ongezeko la bei yake.

Badala ya kuwa na matarajio ya bei ya zao la mwani kusonga zaidi ya Sh. 500 kwa kilo iliyodumu kwa muda mrefu, kinyume imeshuka sasa hadi Sh. 300.

WAKULIMA WALALAMA

“Bora nisilime kabisa mwani kwa bei ya Shilingi 300. Wakati bei ya mwani ilikuwa Shilingi 500, nayo ilikuwa haikidhi mahitaji kutokana na ugumu wa kilimo hicho. Bora nikae nyumbani au nifanye shughuli nyingine,” anatamka mkulima wa mwani, Kazija Machano.

Ni kauli aliyoitoa mbele ya Waziri wa Kilimo, Maliasili, Uvuvi na Mifugo, Hamad Rashid Mohammed, alipowatembelea wakulima wa kijiji cha Uroa, Unguja.

Mkulima huyo anasema kilio chao zaidi kiko katika bei ndogo wanazouza kwa kampuni zinazonunua mwani Zanzibar, anayodai haiendani na gharama ya kilimo chenyewe, pia thamani ya zao hilo.

Anasema baada ya kuona ajira serikalini ni ngumu kupatikana, waliamua kujikita katika kilimo cha mwani ili wajikomboe kiuchumi, lakini imekuwa tofauti na malengo yaliyokusudiwa.

“Baada ya kujikomboa kiuchumi sasa, ndio tunaukaribisha umasikini, kwa sababu gharama kubwa tunazotumia katika kilimo hicho, lakini bei hairidhishi hata kidogo!” analalamik0a.

Anadai wakulima wa mwani hawathaminiwi na wanadharaulika, wakati ndio wazalishaji wakuu wa zao hilo, huku wanaonufaika ni matajiri wanaonunua zao hilo.

Machano anaongeza: “Ukituona wakulima wa mwani wa kijiji cha Uroa, viuno vyetu vimeenda upande kutokana na kazi ngumu ya ukulima wa mwani, lakini faida hatuioni. Tunawatawanufaisha matajiri wanaonua mwani, sisi tunaumia.”

Anawafananisha wakulima wa mwani kuwa sawa na mshumaa anaowaka, huku ukiendekea kuteketea wenyewe, akimaanisha ugumu wa kilimo hicho, haufanani na tija ya kazi yao.

“Ndio maana ukaona wakulima wengi wa mwani ni wanawake, kwa sababu wanaume hawataki biashara zenye utumwa.
“Maana ukulima wa mwani ni bora uuze ubuyu utapata faida kubwa, kuliko mwani ambao ni miongoni mwa kilimo kinachoipatia serikali mapato, ukiachana na utalii na karafuu,” anasema mkulima mwingine, Simni Hassan.

Anaongeza kilio cha bei ndogo ya mwani ni cha muda mrefu, lakini serikali haijaweza kunyamazisha, akipendekeza bei mpya ifikie walau Sh. 1000 kwa kilo.

Hassan anaiomba serikali ichukue hatua ya kuongeza bei kama ilivyofanyika kwa karafuu. Anaongeza: “Huu mwani tulio nao kwa bei ya sasa ya Shilingi 300 hatuuzi. Tuna hiyari tulale na njaa kama hatuna kazi zingine za kuweza kupata fedha.”
Anasema kwamba, kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akilima mwani na anakumbusuha alianza na bei ya kilo moja Sh. 40, lakini wakati huo fedha ilikuwa ikiridhisha kutokana na gharama za maisha wakati huo ilikuwa ndogo, kulinganisha na ilivyo sasa.
Hassan analalamika kilimo cha mwani kinaumiza, kwa sababu wanatumia nguvu katika kilimo hicho.

Ombi lake kwa serikali kupitia Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSCT), lifanye jitihada za kuinua zao la mwani, kama wanavyonunua karafuu kutoka kwa wakulima.

“Serikali kuziachia kampuni binafsi kununua mwani wamiliki wa kampuni hizo, ndiyo wanatuumiza sisi wakulima,” anasema Hassan na kuongeza:
“Sasa tunaiomba serikali kama ilivyopiga marufuku uuzaji wa karafuu kwa watu wengine zaidi ya serikali na mwani wafanye hivyo hivyo, ili na sisi wakulima wa mwani tupate faida.”

WAZIRI WA KILIMO
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed, anakiri bei ndogo ya mwani ya Sh. 300 kwa kilo, haiendani na thamani ya zao lenyewe.

Hamad ambaye yuko madarakani kwa wastani wa nusu mwaka sasa, anasema ili kuendeleza kilimo hicho, ni lazima kuongezwe bei na thamani ya matumizi ya mwani, kwa kujenga kiwanda.

Waziri Hamad anasema kuwasaidia wakulima, ni lazima serikali itafahamu gharama za uzalishaji wa zao hilo.

“Kama karafuu zinanunuliwa na Shirika la Biashara la ZSTC, hakuna sababu ya zao hili la mwani ambalo ni la pili kwa ukubwa, kushindwa kutoa bei ya kianzio kwa wakulima.
“Hatutawazuia wafanyabiashara binafsi kununua mwani, lakini tutaliambia shirika la ZSTC, pale wakulima wa mwani wanapopewa bei ndogo, shirika liweze kununua mwani, ili wakulima wasikandamizwe,” anasema waziri.

Anaongeza kuwa ni lazima serikali kukaa na wafanyabiashara wanaonunua mwani, ili kuwashauri wawekeze katika zao hilo na si kuishia katika malighafi pekee.

Waziri Hamad anaorodhesha matumizi ya mwani kuwa ni pamoja na kutengeneza sabuni, shampuu, mafuta na dawa za kansa na ina wakulima zaidi ya 23,000 Zanzibar, jambo lihnalochangia kufuta umasikini Visiwani.

Anataja sifa nyingine kuwa, zao la mwani ni pekee linalolimwa mara sita kwa mwaka na kila baada ya siku 60, ni msimu wa mavuno kwa zao hilo.

Hamad anawataka wakulima wa mwanimnizao hilo kuwa na moyo wa subira na kuwaahidi kuwa kilio chao atakifikisha katika ngazi za juu ya serikali na ndani ya wiki moja, serikali itatoa maamuzi kuhusu bei ya mwani na kujua sababu za kushuka bei yake.

Mtafiti wa sayansi ya bahari upande wa bailojia katika masuala ya mwani kutoka Chuo cha Sayansi na Mazao ya Baharini Dk. Flow Ezekel Msuya, anasema mwani unaolimwa Zanzibar una faida nyingi mwilini kwa sababu una vitamini mbalimbali na virutubisho, ikiwemo madini joto.

Madini hayo husaidi kutibu ugonjwa wa tenzi ya shingo na kutibu matatizo ya tumbo, ugonjwa wa ngozi na mwani hutumika pia kama chakula.

Mtafiti huyo alieleza changamoto kwa wakulima wa zao hilo, ni bei ndogo ya mwani kutokana na gharama na muda unaotumika kwa kilimo hicho.

Anasema ili mwani uwe na bei kubwa, ni lazima Zanzibar isindike mwani unaovunwa, kusaidia kuachana na utegemezi wa bei ndogo.

Kwa mujibu wa mtafiti huyo, licha ya kuwapo changamoto zinazowakabili wakulima wa mwani, inadaiwa maisha ya wanawake wanaolima zao hilo yamebadilika kwa uchumi wao kubadilika.