Lakini, mapinduzi ya kidijitali hayajawaacha wengi salama. Ni athari na majanga kila kona na hata watoto ni waathirika wa matumizi mabaya ya intaneti.
Kutumia vifaa vya kielektroniki kuanzia kompyuta, simu na televisheni kumechochea ukatili wa kimtandao kwa watoto na kuwasababishia madhara ya kudumu.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), watoto wanatumia muda mwingi mtandaoni kuliko awali, na kwamba duniani kote, mtoto huingia mtandaoni kwa mara ya kwanza kila baada ya nusu sekunde.
UNICEF inasema unyanyasaji wa mtandaoni unaweza kuathiri watoto kila wakati wanapoingia kwenye mitandao ya kijamii au majukwaa ya ujumbe wa papo hapo, na kwamba wakati wa kuvinjari wanaweza kukabiliwa na ujumbe wa chuki na maudhui hatari mengine yakichochea kujidhuru na hata kujiua.
“Watoto wanaweza kuumizwa kupitia kutayarisha, kusambaza na kutumia nyenzo za unyanyasaji wa kijinsia, au wanaweza kutayarishwa kwa ajili ya kunyanyaswa kingono, huku wahusika wakijaribu kukutana nao ana kwa ana au kuwahimiza watoe maudhui machafu,” inasema UNICEF.
Thelma Dhaje ni Mkurugenzi wa Taasisi ya CISEMA ya Dar es Salaam, inayojihusisha na kutetea haki za watoto, akizungumza na Nipashe, anasema tatizo la kimtandao kwa watoto linaongezeka kwa kuwa kila kunapowekwa vizuizi vya unyanyasaji watu wanabuni mbinu mbadala kufanya kile wanachodhamiria kwa watoto.
“Huwezi kutofautisha ukatili unaofanyika mtandaoni na ule wa mazingira ya kawaida, inawezekana mtoto akafanyiwa ukatili au kubakwa na akarekodiwa katika mazingira ya kawaida na ukahamishiwa katika mtandao jambo litakaloathiri maisha yake yote,” amesema Dhaje.
KATUNI NI SHIDA
Mkurugenzi wa CISEMA, anaeleza kuwa dunia inatambua kuwa watoto wengi hupenda kuangalia katuni kwenye televisheni, simu au kompyuta hivyo wasiokuwa na nia njema hutumia nafasi hiyo kutengeneza programu zenye kutambua wakati na mahali mtoto anapoangalia katuni kupitia vifaa vya intaneti.
Anafafanua kwamba watu wanaoendesha programu hizo baada ya kutambua kuwa kuna mahali mtoto anatazama katuni kwa kutumia simu au kompyuta huzidukua na kuziweka katika mfumo unaowawezesha kuwasiliana nao moja kwa moja na kumrubuni kwa maneno na baadaye kumwamrisha kufanya vitu ambavyo ni kinyume na maadili.
“Baadhi ya programu hizo za katuni zimetengenezewa mtu mwenye sura ya kitoto ambaye anatumika kuongea na mtoto anayetazama na kumfanya aamini kuwa anaongea na mtoto mwenzake, baadaye humshawishi avue nguo na kuonyesha maungo huku akijirekodi.
“Katuni zimeonekana ni chanzo cha mtoto kufanyiwa matendo maovu na nyingine humwandaa kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili ‘online gruming child for sexual pupose’.”
Anatoa rai kwa watoto, wazazi au walezi kuwa makini na kuepuka kuwaachia watoto kuangalia vitu hivyo kwenye simu au kompyuta wakiwa wenyewe.
Ananukuu utafiti uliofanywa mwaka 2022 kwa watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 umebainisha kwamba asilimia 67 ya watoto wanatumia mitandao ya kijamii kama facebook, X (twitter), instagram, whatsap, tiktok na telegram.
Aidha, inabainisha kuwa asilimia nne ya watoto waliotumia mitandao hiyo walifanyiwa aina tofauti za ukatili, pamoja na kukutana na wahalifu waliowasiliana nao moja kwa moja kupitia mtandao. Huku asilimia tano wakikutana na vitisho, kushawishiwa na kulazimishwa kutuma picha zao za utupu.
Mhadhiri wa elimu na saikolojia, katika Chuo Kikuu cha Ualimu Dar es Salaam (UDSM) Dk. Hezron Onditi, anaunga mkono hatari ya simu akisema kuwa watoto wengi wameathirika kutokana na matumizi ya simu.
Onditi mtafiti wa masuala ya teknolojia na vyombo vya habari katika ukuzaji wa watoto na vijana, anashauri jamii ibadilike na kuwalinda watoto.
Anadai kwamba kuna wazazi wanawapa watoto uhuru wa kuchezea simu kupitiliza bila kujua kuwa wanawaharibu huku wengine wakifikia kiwango cha kuvitambua vifaa hivyo kuliko wazazi jambo ambalo linageuka kuwa gumu kuwadhibiti katika matumizi.
“Kutumia teknolojia ni haki yao hatuwezi kuwazuia ila kitu tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kwamba vifaa tunavyowapa wanavitumia kwa usahihi katika kusoma na kujiongezea uelewa na sio kutazama vitu vinavyowaharibu kimaadili,” anashauri Onditi.
HATUA ZA SERIKALI
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Dk.Dorothy Gwajima, anasema serikali inakusudia kuweka mkakati madhubuti kama kupitia sheria na kanuni kudhibiti ukatili wa watoto mtandaoni.
Anasema teknolojia inakwenda kwa kasi na maudhui yanayosambaa mtandaoni ni hatari kwa watoto hivyo elimu haina budi kutolewa kwa walezi na wazazi kwakuwa wamejisahau na kuwapa watoto hao vifaa vya kielektroniki ikiwamo simu pasipo kuwa karibu nao kujua nini wanakitazama.
“Tunakwenda kutoa mwarobaini, kumekuwapo na jitihada mbalimbali za kisera na kisheria za kimataifa, kikanda na kitaifa katika kuwalinda watoto na vijana balehe dhidi ya ukatili wa mitandaoni zikiwamo sheria ya makosa ya kujamiiana ya 1998.









