Rais alivyoliandaa Bwawa Nyerere kufuta shida umeme,...

01Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Rais alivyoliandaa Bwawa Nyerere kufuta shida umeme,...
  • ...ziada bidhaa mpya kimataifa
  • *Biteko: Mteja Zambia yu sokoni akisubiri megawati 70

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, mwaka juzi alishuhudia ujazaji maji Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, akipongeza hatua zilizopigwa, licha ya changamoto na hujuma zilizoshuhudiwa wakati wa kuanzishwa kwa mradi huo.

Sehemu ya mtambo wa kuzalisha umeme katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. PICHA: MTANDAO.

Hiyo ilikuwa Machi 22, 2022 akisema mradi huo utasaidia kukabiliana na mafuriko ya kila mara Mto Rufiji, pia kuimarisha kilimo cha umwagiliaji.

“Nataka nitoe ahadi kwenu ndugu wa Tanzania kwamba nitausimamia mradi huu hadi ukamilike.” akatamka Rais Dk. Samia Suluhu, katika matarajio ya kuzalisha megawati 2,115 za umeme kitaifa, wakati huo .

Rais akafafanua kuwa handaki la kuchepusha maji lina urefu wa mita 700, yaani sawa na viwanja saba vya mpira wa miguu lilijengwa miaka mitatu kabla kwa gharama yake takribani shilingi bilioni 235.

Sasa hatua ya kuzindua mitambo inayofua umeme, inatajwa kuihamisha nchi kutoka upungufu wa kati ya megawati 200 na 400 za umeme, hadi ziada ya megawati 70, pale mitambo yote itakapofanya kazi mwezi huu.

Bwawa hilo pia lina sifa ya pili, kuwa kivutio cha watalii kwa kuwa liko ndani ya hifadhi na litabadili kabisa taswira ya hifadhi hiyo na thamani yake kuongezeka ndani na nje ya Tanzania.

Hadi wakati huo mwaka juzi, mradi ulishafikia asilimia 78 ya utekelezaji wake tangu kuanza kujengwa, huku katika uzunduzi, Rais Dk. Samia akaahidi kufutika kilio cha umeme kitaifa.

Maharage Chande, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), akaweka wazi makadirio kuwa misimu miwili ya kipindi cha mvua, itaweza kujaza maji katika bwawa hilo.

“Tunaanza kujaza maji mwezi huu wa Desemba (2022) ambapo kuna mvua za vuli, pia tunategemea mvua za masika mwezi Machi 2023, ambazo zitakuwa mvua za msimu wa kwanza, pia tutapata vuli ndani ya kipindi hicho.

“Kisha tutapata zile za masika katika mwaka 2024 pamoja na vuli ya kipindi hicho, hivyo mvua mbili kubwa za masika zinaweza kujaza bwawa kwa hesabu zilizopo,” akasisitiza Chande.

Sasa hatua ilikofika wastani wa wiki mbili hadi sasa, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, akasema majaribio ya Mtambo Namba Tisa kwenye Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wa Megawati 235 yamekamilika, hivyo kutatua changamoto ya mgao wa umeme nchini.

Wiki hii, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, anasema: “Kwa ratiba tulio nayo ya kawaida, umeme huu ulikuwa utufike mwezi wa sita (Juni, 2023), lakini kwa msukumo mkubwa wa Raisw Samia, leo tunafanikisha.

 

“Tulikuwa na upungufu wa megawati 200 hadi 400, sasa tunakuwa na ziada ya megawati 70,” anasema Dk. Biteko, mwenye ufafanuzi kwamba, ziada hiyo itauzwa nchini Zambia, ambako njia ya umeme kupeleka huko ulishanza kuandaliwa tangu… ukitarajiwa kumaliza mwaka ujao.

 

Wiki moja iliyopita, Naibu Waziri Mkuu Dk. Biteko, akatangaza uzinduzi wa mradi unatarajiwa kufanyika mwezi huu, Rais Dk. Samia akiwa na mgeni wake, Rais wa Misri Albdel Fatah Alsisi, kukiingizwa katika Gridi ya Taifa, jumla ya megawati za umeme 470.

 

UMEME KUUZWA ZAMBIA

Hadi sasa inatajwa soko la kuuzwa ziadfa ya umeme nchini Zambia, unaosafirishwa kwa njia maalum ya, ikipita Iringa hadi nchini Zambia (TAZA), mradi ulioazna mwanzo wa mwaka jana, kwa matarajio ya kwisha mwezi Januari mwaka ujao.

 

Njia hiyo inatajwa kusafirisha umeme kilovoti 400, pia utaimarisha upatikanaji umeme katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa.

 

Pia, akizungumza wiki hii na chombo kimoja cha kimataifa, Dk, Bitelo akasema itafunga fursa Tanzania kufanya biashara ya umeme katika nchi za Kusini mwa Afrika na ndani ya Afrika Mashariki.

 

Mnamo Julai mwaka 2022, aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba, akafafanua kuwa eneo ambako kungejengwa kituo cha kupoza na kukuza umeme cha Tunduma wilayani Momba, mkoani Songwe ni kati ya vituo vitano vya kupoza umeme vitakavyojengwa kwenye mradi huo.

 

Mratibu wa Mradi huo, Mhandisi Elias Makunga, anasemja utatekelezwa kwa gharama shilingi Trilioni 1.4 ambazo tayari Tanzania inazo na kwamba mradi utakuwa ni kiunganishi cha kwanza cha umeme wa juu kati ya Nchi Wanachama wa Kusini mwaka Afrika na Nchi Wanachama wa Mashariki mwa Afrika (EAPP).

 

Inatajwa kuwa ni hali itakayochagiza biashara ya umeme, ikiwezesha Tanzania inaweza kuuza umeme nje ya nchi pale inapokuwa na ziada, pia inamudu kununua umeme huo, pale itakapotokea upungufu.

 

Wakati mradi huo unaandaliwa, serikali ilishatenga shilingi bilioni 23.1 za kulipa fidia kwa wananchi zaidi ya 6,198 waliopisha mradi huo.