Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, anautafsiri kuwa ni zao la nia thabiti ya viongozi hao waasisi wa taifa, kwa kuzingatia uhusiano wa muda mrefu wa wananchi wa pande zote mbili .
Anasema Muungano unabaki kuwa wa kipekee Afrika na duniani kote, akiwataka wananchi wadumu wakiyaenzi, kwa kuutunza na kuulinda, ikiwa ni tunu mojawapo inayoangaza maendeleo ya Watanzania wote, ukishuhudiwa kwa kupiga hatua na kuimarika, ndani ya amani na utulivu nchini.
SABABU ZA KUDUMU
Makamu wa Pili wa Rais SMZ, anasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unadumu kwa sababu umeundwa katika msingi muhimu wa maridhiano ya wananchi yanayotokana na undugu wa damu wa pande zote mbili.
Anarudi kwenye historia kwamba, hata kabla ya Muungano wenyewe kufanyika, tayari viongozi wa pande zote mbili katika kupigania uhuru, walikuwa na uhusiano wa karibu, huku wakishiriki katika mikutano ya kudai uhuru, iliyofanyika katika nchi mbalimbali, ikiwamo Uingereza na Ghana.
Anatoa mfano wa mkutano wa kudai uhuru uliofanyika Lancaster, Uingereza, Rais wa Tanganyika Mwalimu Julius Nyerere alihudhuria mkutano huo pamoja na Rais wa chama cha ASP, Sheikh Abeid Amani Karume, pia viongozi wengine wa vyama vya wapigania uhuru Afrika, akiwamo shujaa Kwame Nkrumah wa Ghana.
''Mara baada ya Tanganyika kupata uhuru wake Desemba 1961, watu hawakushangaa kuona Zanzibar nayo inajikomboa kutoka kwa watawala wa Kiarabu, kwa sababu viongozi wa pande mbili walikuwa wakishirikiana katika hatua mbalimbali, ikiwamo mawazo, mbinu na fikra,' anasimuilia Abdullah.
Hapo Makamu wa Rais, anajivunia mafanikio hayo ya Muungano kufaidika na matunda ya kushirikishwa katika mengi ya msingi yenye unasaba wa pande mbili, Bara na Visiwani.
SMZ YARIDHISHWA
Makamu wa Pili wa Rais, anasema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inatambua mchango mkubwa wa taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar, zinavyofanya kazi kubwa kuhamasisha ukuaji teknolojia na kazi za utafiti, zinazoleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo.
Abdullah anazungumza kwa kielelezo, kwamba kuanzishwa Kituo cha Utafiti wa Bahari katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), kwa kiasi kikubwa kutasaidia kazi za utafiti katika eneo la bahari, ikiwamo kulinda rasilimali za baharini na viumbe vyake.
Anasema, kuanzishwa kituo hicho ni kwenda sambamba na malengo ya SMZ, kuelekea katika uchumi wa buluu, ambao unalinda rasilimali baharini na kuongeza utafiti wa mazao ya bahari.
Abdullah anaipongeza Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya COSTECH ya Jamhuri ya Muungano, kwa kutumia vigezo vyake, hatimaye kuiteua SUZA kufanya kazi za utafiti wa kituo cha bahari.
''Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunaridhishwa na utendaji wa taasisi za Muungano ziliopo nchini katika kuleta mageuzi makubwa ya teknolojia na ubunifu wa kazi za utafiti,' 'anasema Makamu wa Pili wa Rais, huku akitaja mifano ya taasisi hizo za Muungano, ni Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Hapo anafafanua majukumu makuu ya BoT, inatoa sarafu ya Tanzania, pamoja na kusimamia uchumi, pia kudhibiti taasisi za fedha ikiwamo benki zilizopo nchini.
Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, hivi karibu alifika Zanzibar na kuonana na viongozi wa ngazi za juu wa SMZ, akiwamo Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi na Waziri wa Fedha ya SMZ.
Akizungumza nao, Gavana Tutuba akaahidi kufanya kazi zake kwa karibu na SMZ, ikiweka mazingira rafiki na taasisi za fedha, benki ziweke matawi yake Zanzibar, hatua itakayosaidia kuboresha mzunguko wa kuchumi, BOT ikitoa ushauri wa kitaalamu katika uchumi.
- kufanya kazi kwa uadilifu katika pande zote za Jamhuri ya Muungano, nikiamini kwamba Zanzibar ni sehemu ya Benki Kuu, ambayo ni taasisi ya muungano katika kukuza uchumi na maendeleo,' 'anasema Gavana Tutuba.
BALOZI ALI KARUME
Balozi Ali Karume, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, anasema Muungano uliopo umeleta faida kubwa kwa wananchi wa Zanzibar, ikiwamo fursa ya matumizi ya ardhi, soko la pamoja la Muungano la watu milioni 60, wakati Zanzibar ina watu milioni mbili ambapo hiyo ni fursa kubwa kwa uchumi wa Zanzibar.
Anasema, Zanzibar ina eneo ndogo la ardhi na kuwa wakati Zanzibar ilipewa eneo kubwa la ardhi la Makurunge, katika zama za uongozi wa Raisa wa Pili wa SMZ, Aboud Jumbe, ardhi hiyo alikabidhiwa na Rais wa Muungano Nyerere.
Karume, aliyewahi kuwakilisha nchi akiwa ubalozi nchini Italia, anasema Muungano umesadia kuimarisha ulinzi na usalama na kuwataka wananchi kuendelea kulinda misingi wa Muungano, ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere, pia Mzee Karume.
Anataja kauni ya kuugana mataifa mawili, ni lazima kuna upande ukubali kupoteza mamlaka na ndicho kilichotokea mwaka 1964 kwa Tanganyika na Zanzibar.
“Zanzibar isingeweza kubakia salama kama isingeingia katika Muungano, kwa sababu kulikuwa na makundi mawili yanayovutana, wanaounga mkono utawala wa kikoloni chini ya Sultan, jambo ambalo lingesababisha misukosuko na kupoteza utulivu wa nchi,” anasema.
Balozi Karume, anaungana na hoja za wataguilizi wake, kwamba ni Muungano uliosaidia kuimarisha ulinzi na usalama, hivyo anawaasa wananchi kuendelea kulinda misingi wa Muungano.