AWAMU YA SITA NA KERO

26Apr 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
AWAMU YA SITA NA KERO
  • Wasomi & wanasiasa katika butwaa la kasi, miaka miwili 15 zimeondoshwa

HADI sasa Dk. Samia Suluhu Hassan, ana miaka miwili akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania. Kuna mengi katika ukanda huo wenye historia ya miaka 59 unaotimu leo, kwa milima na mabonde ya kuwajibikia umma huo.

Mchambuzi wa siasa, Abbas Mwalimu, anasema katika kipindi cha miaka miwili pekee hadi kufika sasa, serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kutatua zaidi ya hoja 15 za Muungano, akitamka: "Hayo ni mafanikio makubwa katika Muungano wetu, kwani kipekee, katika kipindi cha miaka miwili tu, chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, tumeshuhudia idadi hiyo ya hoja zikitatuliwa."

Ni juzi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo akasema bungeni kuwa katika mwaka wa fedha unaoisha 2022/23, ofisi yake iliratibu vikao vitatu vya kujadili masuala ya Muungano, kwamba hoja nne kati ya nane zilizojadiliwa zilipatiwa ufumbuzi.

Dk. Jafo anazitaja hoja hizo ni: Malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, kodi ya mapato (PAYE) na kodi ya zuio; mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume; na ongezeko la gharama za umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwenda Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).

Anasema kamati ya pamoja ya Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi (SMZ), ziliwashirikisha mawaziri na makatibu wakuu husika.

Waziri Jafo anasema hoja ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, ilitokana na kuwapo tofauti za ukadiriaji viwango vya thamani za bidhaa na kodi ya forodha baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, inayosababisha kulipa kodi ya ziada zinazotoka Zanzibar kwenda katika soko la Tanzania Bara.

Jafo anasema ufumbuzi wa hoja hiyo ulipatikana baada ya kubainika uhalisia wake na sasa linaeleweka vizuri kwa wafanyabiashara wa Zanzibar wanaopeleka bidhaa bara.

Kwenye ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Jafo anasema shida ilikuwa kuchelewa kutiwa saini mkataba wa mkopo kati ya serikali na Benki ya Exim ya China, baada ya mkataba kuhusisha vipengele vya kuweka mali za serikali kama dhamana ya mkopo.

Anasema, ufumbuzi ulipatikana baada ya Serikali ya Muungano kukubali kuondoa sharti hilo, hivyo kuwezesha mkataba wa mkopo huo kutiwa saini mnamo Novemba mwaka jana.

Kuhusu gharama ya umeme, akafafanua kwamba shida imekuwa kuongezeka bei ya umeme kwa wateja wa TANESCO ikiwamo Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).

HISTORIA ILIKOTOKA 

Mchambuzi Abbas anafafanua kuwa tangu kuanzishwa Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano mwaka 2006, kuna jumla ya hoja 25 ziliibuliwa na kufikia mwaka 2021 hoja 18, zilishajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi na kuondolewa katika orodha ya hoja za kero za Muungano. 

"Hoja nyingine nne zilipatiwa ufumbuzi katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ cha Disemba 6, 2022, hivyo jumla ya hoja zilizopatiwa ufumbuzi na Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano ni 22," anasema. 

Abbas, anataja baadhi ya hoja hizo zilizopatiwa jina ‘kero za Muungano’ kuwa ni: Utekelezaji wa Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; utekelezaji wa Sheria ya Usafirishaji Majini;  Uwezo wa Zanzibar Kujiunga na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organisation - IMO). 

Anaendelea kwa kauli "nyingine ni ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ushiriki wa SMZ katika masuala mbalimbali ya kimataifa na kikanda na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia."

Kwa mujibu wa Abbas, pia  inajumuisha utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri  ya Muungano na ile ya SMZ, katika kushughulikia masuala ya Muungano na uingizaji wa maziwa kutoka Zanzibar, katika soko la Tanzania Bara.

TIBA YA KERO

Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), mwanasheria Dk. Hellen Kijo-Bisimba anakiri jitihada zinazofanywa na Rais Dk. Samia kumaliza kero za Muungano zina sura ya mafanikio katika kuzitibu. 

"Tunaona juhudi mbalimbali za Rais za kutaka kumaliza kero za Muungano. hasa kukutana na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa kujali mustakabali wa Taifa," anasema Dk. Hellen. 

Anaongeza kuwa Rais Dk. Samia, ameshazungumzia suala la mchakato wa katiba mpya na kwamba hiyo ni muhimu kwa kila jambo, likiwamo suala la Muungano, ambalio umekuwa likilalamikiwa. 

"Kwanza mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar kwa sasa yanapishana na ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tazania, hivyo suala la kuwapo katiba mpya ni la muhimu, kwani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mbili zilizoungana, lakini katiba iliyopo haiongelei vizuri kuhusu Muungano wa nchi hizo mbili," anasema. 

Mwanasiasa James Mbatia, ambaye alishakuwa Mwenyekiti wa chama NCCR -Mageuzi, pia yumo katika orodha ya wanaharakati waliokuwamo katika wadai wa vyama vingi vya siasa mwanzoni mwa miaka ya 1990, anausema Muungano ni muhimu, hasa katika uhalisia watu wote duniani wanaleta nguvu pamoja, akitoa mfano nchi za Ulaya, zinaendelea kuungana kwa kasi zikijua ‘umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.’

Anasema Watanzania nao wamekuwa wakishuhudia jinsi ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akijitahidi kuulinda, kwa kutatua kero zake kama ambavyo imekuwa ikielezwa na wasaidizi wake. 

"Ingawa sijui kero zinazotajwa kutatuliwa ni zipi, lakini inaonyesha kuwa zimepungua kutoka 25 hadi kufikia tatu, lengo likiwa ni kutaka kudumisha Muungano wetu," anasema Mbatia. 

Hata hivyo, ana ushauri kwamba, ni vyema kwa Watanzania wakijiuliza kuhusu hizo kero kwamba ni zinanafasi gani, akifafanua Muungano uliozaa Tanzania unategemea ni kiongozi gani yupo madarakani na kwamba, pamoja na juhudi zinazofanywa na Rais Dk, Samia, bado kuna a haja ya kuwa na Muungano unaodumu milele, kwa kuunganisha watu wenyewe kwa utashi wa kisiasa.

Ana mtazamo wake kwamba iwapo wananchi watapewa nafasi kuelezea muungano wanaoutaka kupitia katiba mpya, manung'uniko yatapungua. 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form