Magwiji wa uchumi wataja njia kuondoa umaskini

18Mar 2016
Restuta James
Dar
Nipashe
Magwiji wa uchumi wataja njia kuondoa umaskini

MAGWIJI 22 wa uchumi nchini wameandika kitabu kuelezea namna ambavyo Tanzania inaweza kutoka kwenye umaskini hadi kwenye mafanikio.

Kitabu hicho cha kwanza na cha aina yake kilizinduliwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kinaeleza fursa na changamoto zilizopo kwenye sekta mbalimbali hasa kilimo katika kuchangia mageuzi ya kiuchumi.

Katika kitabu hicho chenye kurasa 436, wachumi wanaeleza umuhimu wa kufanya mageuzi ya kilimo yenye mafanikio kwa wakulima wadogo na wakubwa.

Pia kinaeleza umuhimu wa maliasili kwenye mageuzi ya kiuchumi na kijamii na kutaja mambo ya kutiliwa mkazo kuwa ni kujenga uchumi unaokua ili kuzalisha ajira bora, kuongeza tija kwenye kilimo kwa kuongeza matumizi ya pembejeo bora na kuwatambua watu maskini nchini na wenye mahitaji maalum na kutatua kero zinazowakabili.

Pia, magwiji hao wanaeleza kuwa unahitajika uongozi wenye hulka ya kutekeleza na kupenda kuona matokeo kwa kuweka na kusimamia viwango vya juu vya uadilifu, mifumo na taasisi.

Wanasisitiza kuwapo mipango endelevu ya kiuchumi ya muda mrefu na kuepuka mabadiliko ya sera ya mara kwa mara ili kuwapa wadau wengine utulivu, hususani sekta binafsi ili iwekeze kwa muda mrefu.