Hizi ndizo faida za kufuga nyuki kisasa

18Mar 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Hizi ndizo faida za kufuga nyuki kisasa

Kufuga nyuki na kuzalisha asali kwa mtindo wa kisasa kwa kujenga nyumba ya nyuki, inamwezesha mfugaji kuongeza uzalishaji pamoja na kipato.

mfugaji wa nyuki, Rajab Suleiman Khamis, wa Kijji cha Kitogani Mkoa wa Kusini Unguja akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu ufugaji wa nyuki. PICHA NA RAHMA SULEIMAN.

Ufugaji wa nyuki ni kazi ambayo imekuwapo na kudumu kwa karne nyingi.

Mfugaji Rajab Suleiman Khamis wa Kijji cha Kitogani Mkoa wa Kusini Unguja, anaeleza namna ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa umemkomboa kiuchumi.

Rajab anasema ufugaji nyuki kwa njia za kisasa ni nyanja inayoweza kuchangia uchumi wa taifa na kuinua kipato cha Watanzania.

Anaeleza kuwa alianza kufuga nyuki mwaka 2000 kwa kutumia dhana za ufugaji wa kizamani bila ya kupata manufaa makubwa, lakini baada ya kupata mafunzo ya ufugaji wa nyuki wa njia za kisasa mwaka 2010 umemuwezesha kufaidika na kazi hiyo.

“Mwanzoni nilikua nafuga nyuki kimazowea kwa sababu nilikuwa natumia vifaa vya kizamani hata asali niliyokuwa nikiipata ilikuwa kidogo na ilikuwa haina ubora tofauti na asali ninayovuna sasa Hivi,” anasema mfugaji huyo.

Anasema ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa umempatia umaarufu mkubwa na amekuwa na wateja wengi kutokana na ubora wa asali anayoivuna.

Anaeleza kuwa baada ya kuvuna asali wateja wake humfuata nyumbani kwake Kitogani takribani kilomita 27 kutoka mjini Unguja.
“Teknolojia ya mawasiliano imeturahisishia kazi maana napigiwa simu na watu ambao hata siwafahamu wanataka asali mimi huwaeelekeza nilipo na hunifuata kwa ajili ya kuinunua,” anasema.

Anasema kuwa ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa ni mzuri zaidi kwa sababu sio nyuki wote wanaohitajika kuna nyuki wengine ni maadui hawafai kufugwa na wala hawatoi asali.

Anasema kabla ya kupata elimu ya ufugaji wa nyuki wa kisasa alikuwa hajui kama baadhi ya nyuki hawafai kwa ufugaji wa asali.

“Mfano kuna nyuki anaitwa adui mimi nilikuwa nakusanya wote kumbe hawafai, lakini baada ya kupata elimu sina haja nao sasa kwa sababu ni adui kama jina walilopewa,” anasema.

Katika hatua nyingine, mfugaji huyo anasema kuwa siyo kila nyuki anahitajika kwa ufugaji wa asali kwani wapo nyuki wa aina tatu ambao ndio wanaohitajika zaidi ambao ni nyuki wanaoitwa malkia, kibarua na kidume.

Anafafanua zaidi kuwa malkia kazi yake ni kukaa ndani katika mizinga ya nyuki bila ya kwenda popote, lakini nyuki kibarua wao kazi yao kwenda kutafuta chakula na kumletea nyuki malkia.

Anasema malkia ndie anayetoa asali nyingi zaidi na ndio wafugaji wengi wanaomtegemea, lakini ni lazima yawepo makundi matatu ya aina hiyo ya nyuki.

Anasema nyuki aina ya kidume kazi yake pia ni kutafuta chakula na kumletea malkia, lakini pia kazi yake nyingine ni kumhudumia nyuki malkia ikiwamo kupata watoto wa nyuki (kumpa mimba).

Anasema kuwa elimu ya ufugaji wa nyuki aliipata kwa Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mizengo Pinda, mkoani Dodoma baada ya kupelekwa huko na kupatiwa elimu ya ufugaji wa nyuki kwa kutumia njia za kisasa.

“Kwa kweli Mheshimiwa Mizengo Pinda ni mtoto wa mkulima maana huko shambani kwake tulijifunza mambo mengi ikiwamo ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa na ukulima wa mboga; baada ya kurudi nikawakusanya wanakijiji wezangu na kuwapa elimu ya ufugaji wa nyuki wa kisasa,” anasema.

Aidha, anasema elimu aliyoipata ambayo ilikuwa ya muda mfupi, aliitumia vizuri na ndio mpaka sasa ufugaji wa nyuki na uuzaji wa asali ndio mkombozi wa maisha yake.

Rajabu licha ya kufuga nyuki, pia ni mkulima wa mboga na anaishukuru Jumuiya ya Uhifadhi wa Mazingira ya Msitu wa Jozani na Ghuba ya Chwaka (Jeca), ambayo ndio iliyompeleka Dodoma kwa Pinda kupata elimu ya ufugaji wa nyuki kisasa.

Anasema baada ya kupata elimu hiyo kwa mwaka, anavuna asali mara mbili mwanzoni mwa mwaka na mwishoni mwa mwaka.

Alieleza kuwa anamizinga ya nyuki ya kisasa 12 na anazalisha asali lita 50 kwa mwaka na lita moja ya asali anauza elfu 30,000.

Anasema msimu mzuri wa ufugaji ni kipindi cha mvua wakati ambao maua huchanua na nyuki huwa na chakula cha kutosha ikilinganishwa na kipindi cha kiangazi.

Alisema kipato anachokipata kwa mwaka kutokana na ufugaji wa nyuki ni Sh. 1,500,000, fedha ambazo humsaidia kuendesha familia ikiwamo kununua chakula, huduma za afya kwa watoto wake watano na mke wake mmoja pindi wapougua na pia kununulia vifaa vya shule kwa watoto wake.

Anasema ufugaji wa nyuki unafaida kubwa kwa sababu asali ina soko kubwa Zanzibar, lakini hata pia nje ya Zanzibar na wateja wake wengi humfikia mwenyewe kwa sababu kuna uchakachuaji mkubwa wa asali unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara hivyo asali yake huwa ni ‘original.’

Anaongeza kuwa anatarajia kununua mizinga ya nyuki ya kisasa mingi zaidi na kujenga mabanda mengi kwa ajili ya kuhifadhi mizinga hiyo ili kuzalisha asali nyingi na kupata tija zaidi kwani mizinga aliyonayo kwa sasa ni 12 ambayo anaona haitoshelezi uzalishaji kulingana na soko.

Anasema awali alikuwa akifuga nyuki bila ya kuwa na mavazi maalum ambayo nyuki hawezi kumng’ata, lakini sasa hali ni tofauti.
“Mwanzoni nilipokuwa sina mavazi maalum, nyuki walikuwa wakinitafuna na nyuki wanauma licha ya kuwa baadhi ya watu wanasema nyuki anakinga ya mwili na ili kinga hiyo uipate lazima akung’ate,” anasema.

Hata hivyo, anaeleza kuwa biashara ya ufugaji wa nyuki inakabiliwa na changamoto ya wizi wa asali.

“Kama wewe ndugu mwandishi nyuki unawaogopa kuna wenzeko hawawaogopi maana wanatuibia asali ikiwa katika mizinga ya nyuki,” anasema.

Naibu Katibu Mkuu wa Jeca, Awesu Shaabani Ramadhani, anasema ufugaji wa nyuki kisasa umesaidi kuhifadhi msitu wa Taifa wa Jozani ambao ndio msitu mkubwa Zanzibar na ni kivutio kikuu cha watalii.

Anasema wafugaji wa nyuki wanaotumia ufugaji wa kisasa wamekuwa wakihamasishana kuhifadhi mazingira kwani bila ya msitu asali haiwezi kupatikana.

Anasema kabla ya kupatiwa elimu ya ufugaji nyuki kisasa, wafugaji wengi walikuwa wakitumia njia za kizamani ikiwamo kutumia moto hali ambayo ilikuwa inauchoma msitu wa Jozani mara kwa mara.

Aidha, anasema Kijiji cha Kitogani kimepakana na hifadhi ya msitu wa Taifa wa Jozani, hivyo baada ya kuona msitu huo unachomwa mara kwa mara kunatokana na wafugaji wa nyuki, ndio wakawawezesha baadhi ya wafugaji nyuki kuwapatia elimu ya ufugaji wa kisasa ili washiriki kuuhifadhi.

Hata hivyo, anasema pamoja na elimu hiyo kuongeza uzalishaji wenye tija, bado kuna wafugaji nyuki haramu ambao wanatumia moto wakiwa msituni.

Anawataka wafugaji hao kuachana na ufugaji huo na kufuga kisasa ili kulinda mazingira na kupata tija zaidi katika ufugaji nyuki.