Dk. Sezibera: EAC tuko mbioni kuungana na Sadc, Comesa

18Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Dk. Sezibera: EAC tuko mbioni kuungana na Sadc, Comesa

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), ni moja ya muungano mahiri wa kikanda hivi sasa ambao umeendelea kuimarika, hata baada ya wasiwasi wa muda mrefu.

Dk. Sezibera.

Hivi sasa, jumuiya nyinginezo za Afrika kama vile Jumuiya ya Kiuchumi Afrika Magharibi (Ecowas) na ile ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wanafuatilia kasi ya maendeleo ya EAC na taarifa zinaeleza kuwa hata Umoja wa Ulaya (EU), una maofisa wake jijini Arusha wanaojifunza jinsi mambo yanayofanyika.

Wazo la kuanzisha EAC lilikuwa la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Rais wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta, mwaka 1967.

Walifanikiwa kuianzisha na ikadumu kwa miaka 10, hadi mwaka 1977 ilipovunjika kutokana na kukosekana maelewano baina ya wanachama, chanzo kikuu ni mgogoro wa Rais wa Idd Amin Dada wa Uganda.

EAC inaundwa na wanachama sita ambao ni; Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Tanzania na Sudan Kusini iliyojiunga wiki chache zilizopia.

Miaka 23 baada ya kuvunjika kwa EAC ya kina Nyerere, ilianzishwa tena rasmi mwaka 2000, baada ya mchakato kukamilika mwaka mmoja kabla.

Maono ya EAC ni kufikia mafanikio, ushindani, usalama na umoja wa kisiasa. Jukumu lake hilo limejikita katika kupanua na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni ili kuboresha maisha ya watu wa Afrika Mashariki kwa kuongeza ushindani, ongezeko la thamani ya uzalishaji, kuimarisha biashara na uwekezaji.

Rajamu (Brand) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ‘watu wamoja, mwelekeo mmoja.’

Hivi sasa, viongozi wa kisiasa kwa maana ya marais wamejipanga kuhakikisha EAC inaimarika na wananchi wameelewa wazo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo kutokana na fursa kama za kibiashara zilizopo kutokana na mtangamano huo.

Takwimu zinaonyesha kuwa biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikua kwa asilimia 40 kati ya mwaka 2005 na 2009.

Mathalani, mauzo ya bidhaa nje nchini Uganda kwenda Kenya yaliongezeka zaidi ya mara 10 kutoka dola za Marekani milioni 15.5 mwaka 2004 hadi dola za Marekani milioni 172 mwaka 2009.

Aidha, mauzo ya nje ya Tanzania kwenda Kenya katika kipindi hicho yaliongezeka takribani mara tatu, kutoka dola za Marekani milioni 95.5 hadi dola za Marekani milioni 300.

Hali hiyo inatarajiwa kuendelea kukua kutokana na uanzishwaji soko la pamoja.

Moja wa washiriki muhimu katika mafanikio ya EAC ni Katibu Mkuu, aliyeacha madaraka siku kadhaa zilizopita, mwanadiplomasia wa Rwanda, Balozi Dk. Richard Sezibera.

Dk. Sezibera ambaye pia ni meja mstaafu wa jeshi la Rwanda, amewahi kuwa waziri na balozi wa Rwanda nchini Marekani.

Swali: Jumuiya inaendelea kukua, ikiwa na mambo mengi mazuri. Nini matarajio yako kwa miaka miwili ijayo na pengine kabla hujamaliza muda wako?

Dk. Sezibera: Tunajivuna kuwa jumuiya ambayo inajijenga pamoja kwa uwazi, kwa lengo la kuunda shirikisho la kisiasa; ndoto ambayo ilianzishwa na Mwalimu Nyerere, Mzee Kenyatta na wengine mwaka 1967. Urithi ambao tungependa kuona unatimia. Ili kufanikisha hili kuna hatua kadhaa tunatarajia kupitia ili kufikia lengo hilo ambazo ni:

Kuanzisha Umoja wa Forodha kwa ajili ya kuruhusu mwingiliano huru wa watu, bidhaa na mitaji; soko la pamoja, idara moja ya fedha na hatimaye shirikisho la kisiasa.

Maeneo muhimu yatakayowezesha kuendelea mbele naweza kuyataja kuwa ni usafirishaji huru wa bidhaa ndani ya Afrika Mashariki, kitambulisho au hati moja ya kusafiria, kuondoa vibali vya kazi na matumizi ya kadi moja ya utambulisho kwa wanachama.

Vingine ni miundombinu, ikiwamo reli, nishati, usafiri wa ndani wa majini na bandari.

Ninafurahi kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi tunajenga reli ya kisasa. Mathalani, kati ya miaka ya 1954 hadi 2000, Uganda ilikuwa na bwawa moja tu lililojengwa na Uingereza katika mto Nile mwaka 1954.

Hivi sasa, kuna uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya nishati kwa nchi zote wanachama na naona kitu kingine kitakachotufikisha tunakotaka kwenda, ni kuwashirikisha raia wetu. Vijana, wanawake na viongozi wa dini kwani ni muhimu sana katika kuelekeza mtangamano.

Swali: Unaweza kutabiri nini kuhusu Shirikisho la Kisiasa Afrika Mashariki?

Dk. Sezibera: Huwezi kulazimisha umoja wa kisiasa kwa watu, linapaswa kutoka ndani, kutoka kwa wana Afrika Mashariki wanaoitamani Afrika Mashariki na njia bora ni kuwaletea mafanikio.

Ukizungumza na wafanyabiashara wana kiu kubwa na Mtangamano wa Afrika Mashariki na upanuzi wa benki katika nchi wanachama ni mfano halisi.

Kwa mfano, Banque de Kigali, sasa imefungua tawi Nairobi na inataka kuingia Uganda, wakati benki ya CRDB ya Tanzania sasa ina matawi Burundi. Hali kadhalika, benki za Kenya na biashara nyinginezo zimepanuka sana kwenye ukanda wetu.

Swali: Ufanyaji wa biashara ndani ya Jumuiya unakabiliwa na vizuizi kadhaa. Ni jinsi gani tunakabiliana na suala hili?
Dk. Sezibera: Bado inachukua muda mrefu kutoa bidhaa nchi moja hadi nyingine na ni gharama kubwa.

Hii inasababishwa na kucheleweshwa kwenye vituo vya ukaguzi kuanzia bandarini, vizuizi vya barabarani na kwenye mizani.
Mathalan, ilikuwa inachukua takribani siku 21 kutoa bidhaa bandari ya Mombasa hadi Kigali. Hata hivyo, siku hizo zimepungua hadi tano.

Pia, gharama za usafirishaji zimepungua kutoka zaidi ya dola za Marekani 1, 070. Lengo la Jumuiya ni kupunguza siku za kutoa mzigo Dar es Salaam hadi Bujumbura na Kigali, iwe chini ya siku tano kwa barabara.

Pale Mombasa, kuna kitu kinaitwa ‘Mombasa road Charter’ ambayo inaunganisha wakala wote na mfanyabiashara anaweza kulipia mzigo wake kabla na hata kama hutolipia, lengo ni kuhakikisha kwamba kontena halikai bandarini kwa zaidi ya siku saba.

Maana yake ni kwamba, hivi sasa wanafanyakazi kwa saa 24 kila siku, jambo linalolenga kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara ndani ya Jumuiya.

Swali: Nini sera ya EAC ya vijana na wanawake?

Dk. Sezibera: Tunayo Sera ya Vijana ya Afrika Mashariki na inazitaka serikali za nchi wanachama kutenga bajeti maalum ya kuendeleza wanawake na vijana kwenye nchi zao.

Tuna mashirika ya vijana Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya na Tanzania. Kwa upande wa wanawake, chini ya Baraza la EAC tunahamasisha miradi ya wanawake. Mwisho wa siku, ni wajibu wa kila mhusika kusimama kuzikabili changamoto na kuangalia fursa zinazoweza kuwakwamua.

Swali: Je, tunafikiria kuipanua zaidi Jumuiya kwa kuongeza nchi za Ethiopia na DRC?
Dk. Sezibera: EAC haitafuti wanachama. Nchi zinaomba na zikikidhi vigezo zinajiunga. Kwa sasa ni Somalia na Sudan Kusini ndizo zimeomba.

Kwa Somalia kumekuwa na kikwazo kutokana na sababu zilizowazi.

Kuna mambo mahsusi tunayozingatia kwenye Jumuiya. Aidha, EAC, Comesa na SADC tuko kwenye majadiliano ya kuanzia eneo huru la biashara, ili kuwaingiza majirani zetu.

Katika hili, tuna mikakati maalum ya miundombinu na uhuru wa mwingiliano wa wafanyabiashara.

Kwamba haitakuwa na manufaa kwa mfano kujenga reli itakayokufikisha Kigali, lakini haikufikishi Kongo (DRC).
Mkakati huu ukikamilika, utaziunganisha nchi 26 zenye pato la dola za Marekani trilioni moja.

Swali: Ulikabiliwa na shinikizo gani tangu ulipokabidhiwa jukumu hili?

Dk. Sezibera: Ni fursa kubwa ya kuwajibika ambayo nimeifurahia sana.

Swali: Ni kwa namna gani ungependa kuona Waafrika wanaoishi ughaibuni (Diaspora), wanajihusisha katika Jumuiya kwa manufaa ya jamii yao kwa ujumla?

Dk. Sezibera: Kwanza kabisa ninafurahi kwamba mchango wa ‘diaspora’ kwenye nchi zote ni mkubwa na ni chanzo kikuu cha mapato.

Hata hivyo, ningependa kuona ‘diaspora’ wa Afrika Mashariki wakileta siyo tu mitaji, bali utaalam na ujuzi wao.

Tunalo Baraza la Biashara la Diaspora la Afrika Mashariki (EADBC), lililopo Marekani na tumezungumza nao. Kuna namna ambavyo wanaweza kupanua wigo wa mchango wao kwenye uwekezaji na tunatarajia kuanzisha mahusiano imara na baraza hili na ninaamini mabaraza mengine zaidi yatafunguliwa kwingineko.

Swali: Ni changamoto ipi kubwa umekabiliana nayo au pengine nini mafanikio?

Dk. Sezibera: Mafanikio yangu ni ya Jumuiya yote, ikiwamo kuanzishwa kwa Kituo Kimoja cha Forodha, utekelezaji wa Soko la Pamoja na kukamilisha mazungumzo kuhusiana na Umoja wa Sarafu.

Nyingine ni kujikita kwenye kuendeleza miundombinu kama reli, nishati, bandari na usafiri wa ndani wa majini na kadhalika. Vivyo hivyo, kuwashirikisha raia wa Afrika Mashariki katika ajenda ya muungano.
Swali: Nje ya kazi, ni mambo gani binafsi huwa unayafanya?

Dk. Sezibera: Nasoma, nacheza tenesi na kupumzika na familia yangu. Hivi sasa, nasoma kitabu kinachoitwa Mitaji na Kukosekana kwa Usawa (Capital and Inequality).

LDk. Sezibera aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa EAC Aprili 19, mwaka 2011.