Lulu: Waziri mdogo zaidi anayefichua mbinu kutokomeza mfumo dume

20Apr 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Lulu: Waziri mdogo zaidi anayefichua mbinu kutokomeza mfumo dume

NAIBU Waziri wa Kilimo, Misitu, Maliasili, Uvuvi na Mifugo, Lulu Mshamu Abdallah ni waziri mwenye umri mdogo katika baraza la mawaziri la Zanzibar.

naibu waziri wa Kilimo, Misitu, Maliasili, Uvuvi na Mifugo, Lulu Mshamu Abdallah.

Lulu ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28 ambaye anaimani kuwa wanawake wanaweza iwapo tu wataondolewa vikwazo vinavyoikabili jamii ikiwamo suala la mfumo dume.

Anasema kuwa atahakikisha anaitumia vizuri nafasi hiyo ya juu aliyoteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kufanya kazi kwa bidii na uaminifu.

Anasema kuwa atahakikisha pia anawashajihisha wanawake kujiajiri ili kuachana na utegemezi kutoka kwa waume zao au familia na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali kama ufugaji, kilimo cha mboga na biashara.

“Nitafanya kazi kwa bidii na uaminifu, lakini pia nitahakikisha nalitumikia taifa na kujali zaidi masuala ya jinsia ili wanawake nao kuwakomboa kiuchumi na kuondoka na umasikini,” anasema.

Lulu ni miongoni mwa wajumbe saba wanawake wa Baraza la Mawaziri katika baraza hilo lenye mawaziri na naibu mawaziri 22; mawaziri wanne ni wanawake na naibu mawaziri watatu wanawake hali ambayo inaleta taswira nzuri ikilinganishwa na mabaraza ya mawaziri katika serikali zilizopita.

Mwamko wa wanawake katika baraza la mawaziri na hata katika baraza la wawakilishi kwa mwaka huu umeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Baadhi ya watu wamekuwa wakisema kuwa jitihada za wanaharakati mbalimbali wa kutetea masuala ya wanawake zimeanza kuzaa matunda baada ya kuona wanawake nao wanapata nafasi za juu za uongozi serikalini.

Mratibu wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), ofisi za Zanzibar, Mzuri Issa, anasema kuwa uteuzi wa rais wa Zanzibar kwa kiasi fulani kumekuwa na mabadiliko kwa sababu mawaziri wanawake wanne wameteuliwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Afadhali rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amejitahidi kuwapa nafasi wanawake katika baraza la mawaziri, mgawanyiko wa wanawake katika nchi ni asilimia 51 na pia masuala muhimu Ya usawa wa kijinsia asilimia 50 kwa 50, tunaona bado tuna nafasi ya asilimia 19.3 hivyo bado kunakazi lakini rais amepiga hatua,” alisema.

Kuhusu Naibu Mawaziri, anasema kuna hatua kwa sababu kati ya saba walioteuliwa watatu ni wanawake sawa na asilimia 43.
Hata hivyo, anasema bado katika hatua ya juu ya uongozi wa nchi wanaume wanatawala kama nafasi ya urais na umakamu wa pili hivyo asilimia 50 kwa 50 katika usawa wa kijinsia haujafikiwa katika nafasi hizo.

Aidha, mratibu huyo aliwataka Mawaziri wapya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanaangalia usawa wa kijinsia katika utendaji wao wa kazi ili kufikia azma ya usawa wa kijinsia.

“Tamwa Zanzibar imetiwa moyo na idadi ya wanawake walioteuliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein hivi karibuni ambapo inaonyesha utayari wake wa kuleta usawa wa kijinsia,” anasema Mzuri.

Anasema kati ya mawaziri 13 walioteuliwa, wanne ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 30.7, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na vipindi vilivyopita vilivyoongozwa na Dk. Shein pamoja na waliomtangulia.

Mzuri anasema ni muda muafaka sasa kwa Mawaziri hao kuingiza masuala ya kijinsia katika utekelezaji wa shughuli zao zote ikiwamo kupanga, kuripoti na kutathmini.

Anasema ajenda ya usawa wa kijinsia imeanza kufanyiwa kazi tokea miaka ya 1980, lakini haikuweza kufikiwa kutokana na kutokuwapo kwa mfumo madhubuti wa utekelezaji na tathmini.

“Hichi ni kipindi kizuri kwa Mawaziri hao wapya kuweka misingi imara kuhakikisha kuwa katika kila sekta maendeleo ya wanawake yanapatikana badala ya kuachiwa Wizara ya Wanawake pekee,” alisema.

Aidha, alisema mapungufu makubwa ya kijinsia yanawaathiri zaidi wanawake yanaonekana katika ufikiaji na umiliki wa zana za uzalishaji, ushiriki katika nafasi za maamuzi na ukatili wa kijinsia ikiwamo ufikiaji wa haki za kisheria.

Anasema Tamwa inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wanawake hawaachwi nyuma katika harakati za kimaendeleo na ndio maana ilikuwa ikitoa elimu kwa jamii kupitia mradi wa Gewe ambao lengo lake ni kuwawezesha wanawake.

“Mradi wa Gewe na miradi mingine ambayo tupo nayo imetusaidia sana kutoa elimu kwa jamii na sasa ile dhamira ya usawa wa kijinsia imeanza kuzaa matunda,” alisema Mzuri.

Hata hivyo, alieleza ni faraja kubwa kuona wanawake saba katika baraza la wawakilishi wamechaguliwa na wananchi majimboni na kuongeza idadi ya wanawake katika baraza la wawakilishi hadi kufikia 31 kati ya wajumbe 84 waliomo katika baraza hilo.

Naye mwanaharakati Khatibu Suleiman wa kutetea haki za wanawake, anasema uteuzi wa rais umezingatia usawa wa kijinsia ikilinganishwa na miaka iliyopita ingawa asilimia 50 kwa 50 bado haijafikiwa.

“Rais amechukua ujasiri mkubwa sana kuwateua mawaziri na manaibu waziri wanawake mimi nadhani ameanza kuwaamini wanawake hivyo wanawake nao waoneshe uwezo wao wasimwangushe rais wakifanikiwa hapo wanawake uwezekano upo wa kuongezeka kwa nafasi mbalimbali,” alisema mwanaharakati huyo.

Alimshauri rais licha ya kupiga hatua nzuri ya wanawake kuwateua katika baraza la mawaziri, lakini pia asiwasahau katika nafasi nyingine kama nafasi za ukatibu mkuu kwani ni waaminifu na watendaji katika majukumu yao ya kazi.

Moza Saleh naye ni mwanaharakati wa kupigania haki za wanawake na watu wenye ulemavu, anasema usawa wa jinsia sasa umeanza kukua na kuongeza kuwa kundi maalum la watu wenye ulemavu halijalizingatiwa katika baraza la mawaziri.

“Kundi la watu wenye ulemavu linahitaji kusemewa hivyo anayevaa kiatu ndie anaejua saizi...wakiteuliwa watu wenye ulemavu ndio watakaoweza kueleza matatizo ya walemavu,” anasema Moza.

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein hivi karibuni alitangaza baraza la mawaziri lenye wajumbe 21 ambao 15 ni mawaziri na saba ni naibu waziri, lakini kati ya hao mawaziri na manaibu waziri wanawake ni saba.

Mawaziri na manaibu waziri hao wanawake pamoja na wizara zao kwenye mabano ni Riziki Pembe Juma, (Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali), Moudline Castico, (Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto), Salama Aboud Talib (Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira), na Balozi Amina Salum Ali (Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko).

Wengine ni Lulu (Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi), Choum Kombo Khamis (Naibu Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo) na Harusi Said Suleiman (Naibu Waziri wa Afya).