La kusisitiza hapa si tu ile haki au fursa ya kutoa madai, lakini kuwa wana uwezo, haki na uhalali wa kufanya hivyo.
Kwa miaka mingi, asasi za kiraia pamoja na vyama vya kisiasa vinavyoonekana kuwa ni ‘vya upinzani’, vimekuwa vikilingania haki ya kuandamana.
Binafsi naamini kuita hii ‘haki ya kuandamana’ haiakisi hasa nini kimekusudiwa kwa maana kuwa wanaoilingania haki hii hawatafuti tu kufanya matembezi bali ni hali na haja nzima ya kuonyesha hisia zao au kuunga mkono jambo fulani au kupinga jambo fulani ambalo hawakubaliani au kuridhishwa nalo.
Nchini Brazil kuna vuguvugu linalopinga namna nchi inavyoendeshwa na hususan kuporomoka kwa uchumi.
Pia kuna hisia kuwa watawala wa nchi hiyo wamehusika na matukio ya ufisadi na kuwa kuna njama ya kuyafunika kwa mtindo wa wakuu kulindana.
Bila shaka mahasimu wa chama tawala wamefurahia hili na wamechochea kwa kiasi suala la Rais Dilma Rouseff kuondolewa madarakani kwa kura ya kukosa imani naye.
Lakini pia kuna wafuasi wa chama tawala ambao hawakufurahishwa na hali ya utata iliyojitokeza kati ya Rais Rouseff na Rais aliyemtangulia Luiz Inácio Lula da Silva ambao pia wamejiunga na harakati za kumwajibisha Rais wao hata kama ni mwanachama mwenzao.
Na viongozi wengi wa BRIC wameonja joto ya jiwe na kuona ghadhabu ya wananchi au ya wawakalishi wa wananchi.
Kabla ya haya yaliyojiri Brazil, huko Afrika Kusini Rais Jacob Zuma, aliponea chupuchupu kupigiwa kura ya kukosa imani naye na bunge la nchi hiyo. Ingawa hatua hiyo ilishindikana, lakini Rais Zuma alipata aibu ya kujadliwa kwenye mahakama ya juu kabisa ya nchi. Mahakama hiyo haijasita kumwajibisha kwa kile walichokibaini ni mwenendo usiokidhi matakwa ya katiba ya nchi.
Ingawa huku China dola na chama tawala kimekaba uhuru wa raia kuandamana toka mauaji ya Tianamen Square, tunaona wanaharakati wakipeleka harakati zao nje ya China na kuchagua sehemu ambayo wana hakika dunia itawaona na kuwasikia.
Kwa mfano katika ziara yake ya hivi karibuni Jamhuri ya Czech, Rais wa China alilakiwa na upinzani mkali kupinga sera zake. Waandamanaji walijitokeza siku kadhaa hata kabla ya ujio wake kupinga ziara ya kiongozi huyo kwa misingi ya kiutu na haki za binadamu.
Maandamano dhidi ya China na sera zake zinazokosolewa kuwa zinakandamiza haki za binadamu yamekuwa yakishuhudiwa katika maeneo ambayo yanajitawala ingawa ni sehemu ya China kama Taiwan na Hong Kong.
Labda anapokuja tu katika baadhi ya nchi za kiafrika ndio kasi ya maandamano ambayo yanashuhudiwa katika nchi nyingine ndio hayaonekani, lakini huenda hali hii ikabadilika kadri wananchi wa nchi husika wanapokumbana na mikwara ya wafanyabiashara wa Kichina.
Uingereza nako kunawaka moto, raia wa nchi hiyo wameingia mitaani wakimtaka Waziri Mkuu wao, David Cameroon, awajibike kutokana na sera za chama chake kinachofanya maisha ya wengi kuzidi kuwa magumu, lakini pia kutokana na Waziri Mkuu huyo kuhusishwa na sakata la nyaraka za Panama.
Suala la kuipinga serikali nchini Uingereza si ngeni na ni kama utamaduni kwani ni kawaida kuona watu wamebeba mabango nje ya Bunge la Uingereza au hata nje ya makazi ya Waziri Mkuu. Katika kuiendeleza na kuitukuza uhuru wa maoni kuna eneo limetengwa mahususi katika bustani kubwa jijini London inaitwa Hyde Park.
Huko utakuta watu wanabeba vistuli vyao ambavyo huvitumia kama majukwaa ya kuhutubia. Ukitaka kusikia hoja za kupinga serikali kuu au serikali za majimbo au kiwanda au biashara Fulani, basi jikokote mpaka Hyde Park usikilize wakereketwa kwa mamia ambao kutwa hutoa malalamiko yao au sera zao kwa yoyote anayetaka kusikia na kuwaunga mkono.
Na hakuna lolote linalowafika. Hakuna mtu anayewakamata labda wawe kwa namna moja au nyingine wamechafuana na mshiriki mwingine wakahatarishiana amani.
Lakini kama lengo ni kusema tu basi wanahutubia tani yao na hawana mipaka ya mada.
Huko Ufaransa kwa takriban muongo mmoja nchi imekumbwa na maandamano mbalimbali. Kwa kiasi kikubwa maandamano yanayohusu masuala ya wakimbizi au wahamiaji ndio yamesikika zaidi.
Hata hivyo kuna maandamano ya muda mrefu yanayowahusu vijana wanaopinga ukosefu wa kazi na tabia ya serikali kuondoa kinga za jamii katika mfumo wa kiuchumi.
Kadhalika kuna vuguvugu la muda mrefu linaloendeshwa na wakulima dhidi ya serikali zao kufuata sera ambazo zinawatetea zaidi wakulima wakubwa.
Tumesikia pia kuwa waziri mkuu wa Iceland, Sigmundur David Gunnlaugsson na wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk, wamelazimika kujiuzulu baada ya wananchi wao kupinga vitendo vinavyoashiria ukiukwaji mkubwa wa maadili ikiwamo kuwakingia kifua watendaji au wanasiasa ambao wameshutumiwa kuhusika na ufisadi.
Hapa kwetu kuna nini kuwa wananchi hawaruhusiwi kuonyesha hisia zao? Kwa nini dola na hususan chama tawala wanatafsiri kila maandamano kuwa ni ‘upinzani au ukosoaji’ dhidi yao na si kuwa na haki ya wananchi kuonyesha hisia zao?
Kwa nini ni ngumu nchini kwetu kuona wananchi wakionyesha ‘spontaneous action’ yaani wanaonyesha kutumwa na ‘msukumo wa hafla’kuelezea hisia zao juu ya jambo lenye maslahi makubwa kwa taifa au kwa raia.
Kukosa kuwa na mazingira ya watu kuandamana au kuonyesha hisia yako juu ya mambo mbalimbali ni kuidhoofisha katiba ya nchi inayojinasibu kuwa ina msingi wa kidemokrasia.
Ni lazima watu wadhihirishe demokrasia kwa namna hai na kwa vitendo si kwa porojo za kuunga mkono nadharia, lakini kukawa na kigugumizi katika kutekeleza nadharia husika.
Wanandoa watathibitisha kuwa baada ya fungate kila muda ukipita utamu wa ndoa na kila mmoja kumuona mwenzake malaika hufifia. Hata mzazi ampende mwanae vipi iko siku ya watakerana au kukwaza. Lakini kukwazana si kuhamasiana.
Kwa kuelewa kile kilichomkwaza mtoto wake ndipo mzazi atapojifunza namna ya kuimarisha mahusiano na mwana.
Lakini kama mzazi ataendeleza udikteta na kutaka kumtawala mtoto bila ya kujali mapendekezo ya mwanawe, basi kuna uwezekano mkubwa ya mzazi kuhamasiana na mwanae.
Kwa mantiki hii watawala hawawez kutegemea kupendwa kila wakati au kila siku. Kadhalika watawala hawawezi ‘kutengeneza’ hali ya kuungwa mkono kwa kuruhusu tu maandamo yanayowatukuza au kuunga mkono maamuzi yao, ambayo mengi yanafanywa kwa misingi ya kisiasa si kwa msingi wa ustawi wa nchi na watu wake.
Tanzania inafukuta na kuna mambo mengi yanayowafanya raia au makundi mbalimbali kutaka kuingia mitaani kupinga hali wasiokubaliana nayo au hata kupongeza yale ambayo wanataka yaendelezwe. Kutoruhusu watu kuandamana halitoondoa fukuto, labda litachelewesha tu kulipuka kwake.
Hakika ni vigumu kuwadhibiti watu ambao hawana uzoefu na ‘mfumo huru’ kuliko wale ambao wamezoea kuishi katika uhuru wa fikra na matendo. Hawa wanajua mipaka yao na wanatambua pia umuhimu wa kukondoisha mawazo yao. Wenzao wamezoea kuwekewa mipaka hivyo wanapopata uhuru hata mdogo wanalewa.










