Bajeti 2016/17 imezingatia maoni ya wananchi?

20Apr 2016
Restuta James
Dar es Salaam
Nipashe
Bajeti 2016/17 imezingatia maoni ya wananchi?
  • Mchumi asema elimu imeparanganyika na inadidimia zaidi…

BUNGE la bajeti limeanza vikao vyake jana mjini Dodoma na hakuna shaka kwamba ‘litapitisha’ matumizi ya fedha za walipakodi zinazoombwa na serikali.

Dk Philip Mpango.

Watu wengi walitamani sana serikali ya awamu ya tano izingatie matakwa ya wananchi katika kupanga mambo yake ikiwamo bajeti, lakini hilo ni kama halijawezekana.

Hii ni kwa sababu, kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, vipaumbele vya wananchi ni vinne na havijapadilika.

Tafiti mbalimbali tangu mwaka 2003 zinabainisha kuwa vipaumbele vya wananchi ni afya, elimu bora, maji safi na kilimo.

Hata utafiti wa awamu ya sita wa mwaka 2014 wa taasisi ya Afrobarometer umebainisha kupitia swali la ‘ni matatizo gani ambayo yanaikabili Tanzania kwa sasa’ wananchi walitaja afya kama tatizo kuu.

Kwenye utafiti huo, asilimia 56 ya wananchi walisema afya ni tatizo zaidi, wakati asilimia 30 walitaja elimu na asilimia 29 walitaja maji.

Katika utafiti huo, asilimia 59 ya wananchi walipendekeza kuwa kama fedha zaidi zikipatikana, serikali izielekeze kwenye afya.

Sekta zingine na asilimia kwenye mabano ni elimu (51), kilimo (33) na barabara (28).

Kwa mujibu wa tafiti nyingine za taasisi hiyo ni kwamba wananchi hawaridhishwi na huduma za afya, elimu na maji.

Tafiti ziko nyingi ukiwamo ule wa Sikika na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) wa ‘Madaktari wako wapi?, janga la matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 ambayo asilimia 61 ya wanafunzi walipata sifuri na ripoti ya Wildaf ya mwaka 2014 kuhusu hali ya haki za wanawake ambayo inaeleza takribani nusu ya raia wa Tanzania (watu milioni 18.6), hawapati huduma za maji safi; ni kielelezo cha kwanini huduma za kijamii zimekuwa kipaumbele cha wananchi kwa zaidi ya muongo mmoja.

Mtaalamu wa uchumi ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi na Ujasiriamali (IMED), Dk. Donath Olomi, anasema tatizo la vipaumbele vya bajeti ya mwaka huu ni athari ambazo hazionekani kwa haraka.

Anasema kilio cha wananchi kutaja afya na elimu kama vipaumbele vya msingi kwa muda mrefu kinatokana na huduma zisizoridhisha kwenye sekta hizo.

Anatoa mfano kuwa kwenye hospitali kubwa za umma, kifaa muhimu kinachohitaji matengenezo kwa Sh. 200,000 kinaweza kuharibika, lakini inaweza kuchukua miezi sita bila kutengenezwa kutokana na taratibu za kufuata kupata fedha.

Anasema athari za kutokuipa uzito unaostahili sekta ya afya haziwezi kuonekana haraka, lakini ni sekta inayokabiliwa na changamoto nyingi.

Kwenye elimu anasema ipo chini sana na kwamba mpango wa serikali ulitakiwa kuweka mikakati ya kuiinua ili kuzalisha wataalamu watakaoajirika kwenye sekta zote.

Anatoa mfano kuwa kwenye Taasisi ya Elimu ambayo ndiyo inatengeneza mitaala kuanzia chekechea hadi vyuo vya ualimu, uongozi umebadilishwa mara nyingi kiasi cha kutereresha utendajikazi.

Anasema kuyumba kwa taasisi hiyo kunaathiri elimu kwa kiasi ambacho kinaiyumbisha na kuididimiza zaidi.

“Pale taasisi ya elimu ni sehemu ambayo haieleweki sasa, watendaji wakuu wanaondolewa kila mara, elimu haiwezi kuwa nzuri kwa hiyo lazima mfumo mzima wa elimu uimarishwe na naamini hiki ndicho wananchi wanataka,” anasema.

Aliongeza kuwa: “Kuna vitu ambavyo unaweza usione uzito wake kwa macho. Unaweza kujiuliza kwanini hatuna viwanda, lakini bila kukumbuka kwamba hatujajenga watu wa kutosha kuendeleza hivyo viwanda.”

Anasema: “Kwa kukoresha elimu tunaweza kujenga viwanda vyenye manufaa ya watu.”

Anasema sekta ya elimu ni eneo ambalo linapaswa kutiliwa mkazo hata ikiwezekana kwa kuazima wataalamu kutoka nje ya nchi.

VIWANDA

Kuhusu ujenzi wa viwanda kuwa kipaumbele cha bajeti ya mwaka 2016/17, Dk. Olomi anasema ni jambo lisiloeleweka vizuri kwa kuwa sera haiiruhusu serikali kujenga viwanda.

Anasema jukumu la serikali ni kuweka sera, sheria na taratibu zitakazosaidia kustawisha viwanda kwa kuvutia wawekezaji, na siyo yenyewe kuingia moja kwa moja.

“Hili suala halieleweki vizuri, ni muhimu likawekwa wazi kwa sababu serikali ikisema inataka kujenga viwanda inaweza kuwatisha wawekezaji,” anasema.

Anasema viwanda vya serikali vitaendeshwa kwa kodi za wananchi kwa kupata ruzuku, wakati wawekezaji watatakiwa kutafuta mitaji wenyewe, hali ambayo itaondoa ushindani wa bidhaa usio sawa.

Anasema: “Katika mazingira kama haya, mwekezaji atajiuliza mara mbili kabla hajaamua kujenga kiwanda kwa sababu ni vigumu kushindana na serikali.”

BAJETI YA VIWANDA

Mapema mwezi huu, Wizara ya Fedha na Mipango, iliwasilisha kwa wabunge mpango wa Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, inayokadiriwa kuwa takribani Sh. trilioni 29.

Kipaumbele cha bajeti hiyo ni viwanda, elimu na maji; miundombinu ya umeme na barabara.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo, viwanda vitakavyopewa kipaumbele ni vinavyotumia rasilimali zinazozalishwa nchini zikiwamo mazao ya kilimo, ngozi na pamba.

Bajeti hiyo inawasilishwa wakati ambao Marekani imeshatangaza kuifuta Tanzania kwenye nchi wanachama wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), hivyo nchi kukosa Sh. trilioni 1.03 ilizokuwa ipewe na shirika hilo kusaidia ujenzi wa barabara za pembezoni na kusambaza umeme vijijini.

Umoja wa Ulaya (EU) nao upo kwenye hatihati ya Sh. trilioni 1.56, kutokana na kwamba inasubiri hatima ya mazungumzo na hali ya Zanzibar.

Pia baadhi ya mawaziri wa Uingereza nao wanaishauri serikali yao kumyima Tanzania msaada wa Sh. bilioni 622 kutokana hali ya Zanzibar.

Wizara ya Fedha na Mipango imeshatangaza wahisani 10 kati 14 wanaosaidia bajeti kuu ya serikali kujitoa, ambao Uingereza, Canada, Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Norway na Sweden.