Nimekuandalia mada ihusuyo ‘ndoto’, ambayo ninaamini msomaji wangu utajifunza mambo mengi. Huenda kuna baadhi ya mambo yake hukuwahi kuyaelewa kabla.
Kwa kifupi maana ya ndoto ni taswira, sauti au hisia ambazo akili huzifikiria wakati binadamu anapokuwa usingizini. Hata hivyo uzito au malengo ya ndoto hadi sasa bado hayafahamiki ipasavyo.
Ingawa kuna mada au simulizi za kiudadisi ambazo zimerekodiwa kuhusiana na historia ya ndoto, lakini wapo wanasayansi waliosomea masuala ya ndoto ambao kwa kitaalamu huitwa ‘Oneirology’
Kupitia historia, watu wamekuwa wakiamini kuwa, ndoto nyingi zina maana fulani. Lakini kisaikolojia ndoto imekuwa ikielezewa kuwa ni uwajibikaji wa asili wa kiakili wakati wa usingizi.
Hata hivyo upande wa pili wa saikolojia ya watu wenye imani mbalimbali, inadaiwa kuwa ndoto ni maono ya kiroho au ujumbe kutoka kwa Mungu, miungu, mababu waliokufa kale, utabiri wa mambo yajayo na wengine wanaamini kuwa ndoto ni lugha ya kitabiri.
Mila nyingi za wa watu duniani wanatumia ndoto kama maono ya mpito na wanaamini kuwa ndoto ni ujumbe kutoka kwa Mungu au miungu mbalimbali wanayoiamini.
Watu wa jamii ya Judaism wanayo kawaida ya kufanya sherehe za kiutamaduni wanazoziita ‘Hatavat Halom’ wakimaanisha ‘kufanya ndoto ziwe nzuri’.
Kupitia kwenye sherehe hizo za ndoto, Judaism wanaamini kuwa wanaweza kujiepusha na mambo mabaya au hata kuwasaidia watu kushinda kesi zinazowakabili mahakamani.
Lakini hadi sasa hakuna maelezo yaliyokubalika kibaiolojia katika kuelezea maana ya ndoto. Hata hivyo mwaka 1952 mwanasayansi mmoja aliyekuwa akifanya kazi ya ushauri wa wanafunzi waliokuwa wakisomea udaktari wa falsafa (PhD), Eugene Aserinsky aligundua kuwa, binadamu anapokuwa ndotoni, jicho lake huwa likizunguka kwa ndani wakati kope zikiwa zimefunga. Hatua hiyo aliita kwa lugha ya kitaalamu kuwa ni ‘rapid eye moment ‘ (REM) Sleep.
Pia alitumia mashine au kifaa kiitwacho kwa kitaalamu ‘Polygraph’ kupima mawimbi ya akili wakati binadamu anapokuwa ndotoni, wakati akiendelea na jaribio hilo, aliweza kubaini kuwa, mtu mmoja aliyekuwa akimfanyia majaribio hayo, alikuwa akilia au kucheka akiwa usingizini na kuamini kuwa wakati huo mtu huyo alikuwa akiota ndoto.
Mwaka 1953 Aserinsky pamoja na washauri wake walihitimisha jaribio lao kwa kuthibitisha kuwa ndoto hutokea wakati binadamu anapokuwa usingizini na kutoa jarida lililoelezea mambo mbalimbali kuhusu ndoto.
Utafiti wa kina unaonyesha kuwa, ndoto zina uhusiano mkubwa na REM, ambapo kwa kutumia mashine ya kupima mawimbi ya ubongo wakati binadamu anapokuwa usingizini, utafiti huo unaonyesha kuwa, ubongo huendelea kufanya kazi hata wakati mtu anapokuwa amelala.
Aidha utafiti unaonyesha kuwa watu wengi hawakumbuki ndoto zao na kuwa ni baadhi ya watu wachache wenye uwezo wa kukumbuka ndoto baada ya kutoka usingizini.
Kukumbuka ndoto ni suala lisilotegemewa, ingawa ni taaluma inayoweza kufundishwa, ndoto inaweza kukumbukwa ikiwa tu mtu atashtuka wakati akiota. Utafiti umeonyesha kuwa wanawake ndio wenye uwezo mkubwa wa kukumbuka ndoto zao kuliko wanaume.
Ndoto inaweza kukumbukwa kirahisi baada ya kuona, kusikia au kupatwa na hisia ambazo mtu alikuwa akiziota. Hata hivyo zaidi ya asilimia 95 ya ndoto zote zinazootwa na binadamu hazikumbukwi.
Utafiti zaidi unaonyesha kuwa katika muda wote wa maisha yake, binadamu hutumia takriban miaka sita akiwa ndotoni, muda ambao ni wastani wa saa mbili kwa siku, ambazo binadamu huwa yuko ndotoni.
Wataalamu wa ndoto wanadai kuwa ndoto nyingi huanza na kumalizika ndani ya muda wa dakika tano hadi 20, ingawa pia haijafahamika ni sehemu gani ya ubongo wa binadamu ambapo ndoto huanzia.
Hata hivyo utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa, sio binadamu pekee ambao ubongo wao huonekana ukifanya kazi wakati anapokuwa amelala, hata viumbe wengine hasa walio katika kundi la mamalia na kundi la ndege nao vipimo vimeonyesha kuwa, ubongo wao uko ‘bize’ wanapokuwa usingizini, hali inayoonyesha kuwa, huenda na wao pia huota ndoto..
Kwa mujibu wa ripoti za utafiti, ubongo wa panya unaonyesha ushahidi kuwa huwa ukifanya kazi nyingi na ngumu wakati anapokuwa usingizini kuliko ubongo wa binadamu.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, aina nyingi za viumbe walio katika kundi la mamalia na ndege, macho yao huzunguka ndani ya kope wanapokuwa usingizini (REM) Sleep kama ilivyo kwa macho ya binadamu, hali inayoonyesha kuwa wanyama wa kundi hilo huota ndoto nyingi wanapokuwa usingizini.
Utafiti pia unaonyesha kuwa binadamu wa kawaida anapoingia kulala huanza kupata ndoto kuanzia dakika ya 60 hadi 90 tangu alipoanza kusinzia.
Hata hivyo, wapo watu wasiopata kabisa ndoto katika kipindi chote cha maisha yao. Hii haimaanishi kuwa, watu hao wana matatizo ya kimaumbile na wala hakuna utafiti wa kisayansi ulioweza kubaini kama watu wasiopata ndoto wana matatizo ya kimaumbile, kisaikolojia wala kiakili.
Kumekuwa na simulizi nyingi juu ya maana ya ndoto wanazoota binadamu, lakini kwa vile ndoto hizi zinagusa au kuhusiana na baadhi ya imani za watu, kila mtu amekuwa akitoa maana ya ndoto kutokana na imani yake na kama nilivyoeleza hapo juu kuwa baadhi ya watu wanaamini kuwa ndoto ni maono au ujumbe kutoka kwa Mungu au miungu wanayoiamini.
Kuna ushahidi kuwa kuna baadhi ya ndoto zinageuka kuwa tiba ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua muotoji. Hata hivyo mara nyingi maradhi yanayotibiwa kwa ndoto yamekuwa ni yale yanayohusiana na saikolojia au kiimani.
Ndoto njema!
Makala hi imeandaliwa na Emmanuel Lengwa kwa msaada wa mtandao. Lengwa ni Mwandishi wa Habari. Anapatikana kupitia barua pepe: emmanuellengwa@yahoo.com. Simu: 0756 431 633.










