Elimu Kishapu: Wanafunzi wasomea uwanjani,tangi la maji lageuzwa bao

19Apr 2016
Marco Maduhu
Nipashe
Elimu Kishapu: Wanafunzi wasomea uwanjani,tangi la maji lageuzwa bao

WAKATI Serikali ya awamu ya tano ya Rais Jonh Magufuli imefuta michango yote katika shule za Msingi na sekondari nchini ili kuhakikisha kuwa,

wanafunzi wa Shule ya Ilobi wakisoma kwenye uwanja

wanafunzi wanasoma bure ili kuzalisha taifa la wasomi watakaolisaidia taifa kuwa na wataalamu wake wenyewe watakaoinua uchumi wa Tanzania.

Sera hii ya elimu bure imeonekana kupokelewa na wazazi kwa mikono miwili, hususani wa vipato vya chini na wafugaji ambao hawakuwa wanaona umuhimu wa elimu kwa kuthamini sana mifugo yao na kuwatumia watoto kuchunga mifugo yao.
Baada ya mwitikio huo kuwa mkubwa, baadhi ya shule nchini zimezidiwa wanafunzi hivyo kusababisha kuwepo changamoto ya uhaba wa walimu, vyoo, madawati , majengo na hata kuwafanya wasome kama vile wapo gerezani.

Moja ya shule za msingi ambayo ni kilelezo cha zilizozidiwa na wanafunzi na kusababisha wanafunzi uonja chungu ya elimu bure ni Shule ya Ilobi iliyopo katika kata ya Mwaweja, wilayani Kishapu. Wanafunzi wa darasa la awali wanasoma wakiwa chini ya mti huku tangi la maji likitumika kama ubao.

Wakati wakiendelea na darasa lao chini ya mti, hulazimika kihama kimvuli kinapohama ama mvua kunyesha ndio inakuwa mwisho wa masomo yao kwa siku hiyo.

Athony Faustine ni mwalimu wa shule hiyo anayefundisha darasa la awali chini ya mti kwa kutumia tangi la maji linalogeuzwa ubao wa kufundishia.

Anasema ufundishaji wake unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo hali ya hewa inapobadilika inabidi asitishe masomo kwa wananfunzi hao.

Faustine anasema licha ya hali ya hewa, hata ubao kuubeba ili kutafuta eneo zuri la kuwafundishia watoto hao haiwezekani kwa sababu tangi hilo la maji lililopo shuleni hapo haliwezi kuhamishika hali inayomuwia vigumu kutoa elimu bora kwa wanafunzi hao wa awali.

“Mwanafunzi anaposomea nje au chini ya mti, umakini kwake unapungua na itampatia ugumu sana wa kuelewa haraka, maana ikipita pikipiki, gari au mdudu kaanguka chini ya mti basi akili yake inahama kwenye masomo kwa muda,” anasema Faustine

Naye mwalimu Marieta Sule anayefundisha darasa la nne katika shule hiyo ambao wanafunzi wote wanasoma wameketi kwenye sakafu iliyobondeka, anasema tatizo analokabiliana nalo ni wanafunzi kuwa na miandiko mibaya, kazi kutomaliza kwa wakati sababu ya kuumia migongo kutokana na kujikunja muda mrefu.

Paulina David ni mwanafunzi wa darasa la nne, anasema Shule hiyo imegeuka kuwa kama gereza kwao, na kwamba tangu aanze darasa la awali, hakuna unafuu hadi amefika kwenye darasa hilo, jambo ambalo limekuwa likimfanya asifurahie elimu na kwamba anasoma kama kutimiza wajibu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Mussa Masunga anasema changamoto hizo ni kikwazo kwao na kuwapatia ugumu wa ufundishaji katika kuhakikisha wanafunzi wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), kutokana na mazingira ya ufundishaji kutokuwa rafiki kwao na kwa wanafunzi.

Masunga anasema wanafunzi wa awali wapo 268 wanaofundishwa na mwalimu mmoja wakati ilipaswa wagawanywe kwenye kundi la wanafunzi 25 wakiwa na walimu wao tisa. Kwa sasa wote hao, wapo kwenye darasa moja hali ambayo ni hatari kwa mwanafunzi kuelewa masomo.

Shule hiyo ina walimu 10 tu kwa wanafunzi 807 ,huku vyumba vya madarasa ni sita vilipaswa kuwa 21. Madawati yaliyopo ni 63 ambayo hutumiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza, tano,sita na saba wakikabiliwa na upungufu wa madawati 370.

Mwenyekiti wa kamati wa shule Kulwa Jandikile anasema kutokana na sera hii ya elimu bure, ni kama hawana nguvu tena ya kuhimiza wananchi kuchangia maendeleo ya shule. Wananchi wamekuwa wakijitetea kuwa Serikali imesema hawaruhusiwi kuchangia chochote kile.

Jandikile anasema wanachokifanya sasa ni kutafuta wadau wa maendeleo na mashirika binafsi kusaidia kutatua changamoto hizo, maana fedha inayoletwa na serikali kuhusu elimu hiyo kuwa bure haiweza kumaliza matatizo hayo.

Renatus Mahona ni mkazi wa kijiji cha Mwaweja anasema kutokana na adha wanayoipata watoto wao shuleni hapo, itabidi viongozi wa kijiji na kamati yote ya shule akiwamo mkuu wa wilaya wajitahidi kutoa elimu kwa wananchi angalau wachangie ujenzi wa madarasa na kununua madawati.

Mahona anasema binafsi halidhishwi kuona watoto hao wakisoma wamekaa sakafuni, wengine chini ya mti na kugeuza tangi la maji kuwa ubao, jambo ambalo halimuingii akilini na kubainisha kuwa serikali inabidi iongeze juhudi ili kuhakikisha sera hiyo ya elimu bure inafanikiwa vinginevyo watoto wataenda shule kama sehemu ya kukulia tu na si kupata elimu bora.

Naye Mwenyekiti wa vijana taifa Bavicha (Chadema) Patrobasi Katambi akizungumza kwenye moja ya mikutano yake mjini Shinyanga aliwasihi wazazi kuacha kubweteka na elimu hiyo bure ,inayokabiliwa na changamoto lukuki, hivyo wajitahidi kusaidia watoto wao kwa kuchangia maendeleo ya shule.

Katambi anasema wazazi wakiitelekezea kila kitu serikali watoto wao watamaliza masomo yao bila ya kujua (KKK), kwani shule nyingi hazina vitabu, madawati, uhaba wa majengo ya kusomea, walimu hawatoshi, hivyo zinahitajika jitihada za wazazi ili kuhakikisha kuwa watoto wao wanafanikiwa kielimu.

Sostenece Mbwilo ni Ofisa elimu wa Shule za msingi katika halmashauri hiyo ya wilaya ya Kishapu anakiri kuwapo changamoto hizo, na kubanisha kuwa, suala la elimu bure ndio limechangia shule nyingi kuwa na mapungufu lukuki kwa wazazi kupeleka kuandikisha watoto wenye umri wa miaka sita hadi nane

Mbwilo anasema mwaka jana waliandikisha wanafunzi 53,530 kwa halmashauri yote ya wilaya. Mwaka huu (2016) idadi imeongezeka kwa kuandikisha wanafunzi 58,060 na ongezeko hilo pia limechangiwa na wazazi hasa wafugaji kupeleka watoto wao kuanza shule baadhi yao wakiwa na umri mkubwa.

Ofisa huyo anafafanua kuwa, Shule zote za msingi zilizopo ni 115 madarasa 812 yanayohitajika ni 1,367. Walimu ni 109 na wanaohitajika ni 1,628 na kueleza kuwa, kutokana na miundombinu ya ufundishaji na mazingira kuwa mibovu kwa wastani kila mwaka walimu 80 hukimbia.

Kwa upande wake,Mkuu wa wilaya ya Kishapu Hawa Ng’humbi anasema, kwa historia alivyokuta wananchi wa wilaya hiyo walikuwa hawaithamini elimu zaidi ya kupenda mifugo na kilimo, ndio maana changamoto hizo hazikuwa na nguvu sana, lakini baada ya elimu bure mwamko ndio ukawa mkubwa.

Ng’humbi anasema, licha ya wilaya hiyo kukabiliwa na changamoto hizo za elimu, wanaendelea kujitahidi kutafuta wafadhili, mashirika, makampuni na wadau wa maendeleo ili kusaidiana na serikali kutatua mapungufu hayo na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu katika mazingira rafiki.

Aidha kwa Sera hii ya Elimu bure inabidi serikali ya awamu ya tano iliangalie kwa macho matatu, na siyo kutafuta sifa kuwa wamefuta michango mashuleni na isije hapo baadae tukazalisha Taifa la watu zero kichwani tofauti na isivyotarajiwa, hali inapaswa kutengua kauli yake na kuruhusu wananchi kuchangia maendeleo ya shule.