Hali hiyo imekuwa ikiwawia vigumu wanafunzi kupata elimu bora.Ni changamoto kubwa kwa walimu kuweza kuwafikia watoto wote darasani wakati wanapofundisha ili kukagua wanayapokeaje mafundisho.
Uchunguzi wa mwandishi wa makala hii umebaini kwamba wanafunzi wengi katika shule za serikali wanakaa sakafuni huku msongamano wa wanafunzi darasani nao ni mkubwa sana.
Miongoni mwa shule zinazokabiliana na changamoto hizo ni shule ya Kijitoupele, Tunguu, Kisauni, Magogoni, Mwera regenza Mwenzo, Mwanakwerekwe, Kinuni na Maungani.
Mwalimu wa shule moja kati ya hizo,alisema elimu bure imekuwa na changamoto nyingi hasa kuvutia idadi kubwa ya wanafunzi darasani wakikabiliwa na uhaba wa madawati huku kukiwepo ushirikiano mdogo kwa baadhi ya wazazi, walezi na na walimu.
Alisema darasa moja katika shule anayofundisha lina wastani wa wanafunzi 150 hivyo sio rahisi mwalimu kuweza kuwafikia wanafunzi wote hata kufahamu.
“Baadhi ya wanafunzi wapo darasa la nne, lakini hawajui kusoma wala kuandika. Mwanafunzi kama huyo, anahitaji muda wa ziada kuweza kumfundisha, kwa sababu kila mtoto na ufahamu wake,”alisema.
Baadhi ya wazazi na walezi alisema kuwa wanachangia watoto kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao kwa sababu wazazi hao huwa hawafuatilii maendeleo ya elimu ya watoto wao.
“Mwanafunzi wa shule ya msingi unampa kazi ya kwenda kufanyia nyumbani anarejea siku ya pili, daftari lake hajalifanyia kazi yoyote wala mzazi wake nyumbani hajapitia madaftari yake ili kujua kama ana kazi ya shule amepewa,”alisema.
Kimsingi alisema kuwa, unakuta darasa lina wanafunzi zaidi ya 80 muda wa kufundisha ni dakika 40 kwa kipindi kimoja, hivyo sio rahisi muda huo kuweza kuutumia na wanafunzi wote wakaelewa kile walichofundishwa.
Alisema kuwa wanafunzi kukaa sakafuni na idadi kubwa ya wanafunzi darasani, mwalimu huwa hana umakini wa kufundisha hata kuweza kuwafikia wanafunzi wote darasani.
“Darasa hili ninalofundisha ni wanafunzi wa darasa la kwanza. Kama unavyowaona wamekaa chini na wapo 150 darasa moja. Inaikuwa vigumu mwalimu mmoja ninaefundisha kuweza kuwafikia watoto wote. Inabidi nitumie mbinu za ziada ili wengi waweze kufahamu ninachokifundisha,”alisema mwalimu huyo kwa masharti ya kutotajwa jina lake.
Alisema licha ya idadi kubwa ya wanafunzi shuleni, lakini idadi ya walimu ni wachache, hivyo mwalimu hulazimika kufundisha madarasa zaidi ya matano kwa siku moja.
Aliiomba serikali kupitia Wizara ya Elimu kuongeza idadi ya walimu ili kuweza kukidhi mahitaji ya wanafunzi ili ipatikane elimu bora.
Mwanafunzi wa Shule ya msingi Tunguu, Abubakar Ali alisema kuwa kitendo cha wanafunzi kukaa chini sakafuni darasani inawawia vigumu kupata elimu bora.
“Tunachoka sana kukaa chini sakafuni kiuno na mgongo vinauma. Lakini kama hiyo haitoshi, sare zetu za shule zinachafuka inatulazimu tufue kila siku na sare zenyewe ni moja kipindi kama hiki cha mvua inakuwa mtihani,”alisema Abubakar mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule hiyo.
Aisha Khatib mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo alisema idadi ya wanafunzi wanaosoma elimu ya sekondari sio kubwa sana, ikilinganishwa na madarasa ya shule za msingi.
Alisema tatizo la uhaba wa madawati ni kubwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondani, kwani yaliyopo shuleni hapo ni machache.
“Darasa letu lina wanafunzi 30, lakini lina madawati kumi na mbili, hivyo inatulazimu dawati moja kulitumia wanafunzi wanne. Huwa tunapata tabu tunapotaka kuandika kwenye madaftari yetu,”alisema Aisha.
Hali hiyo ya kukaa dawati moja watu wanne imekuwa ikiwapa wasiwasi mkubwa kutokana na kutojulikana sana hali ya kiafya ya kila mmoja na usafi kwa ujumla.
Baadhi ya wanafunzi alisema kuwa ni wachafu wanafika shuleni bila ya kuoga au kufua sare zao za shule hivyo huwa wanatoa harufu mbaya ambayo huwa kero kwa watu wengine.
“Kwa kweli dawati moja kukaa wanafunzi wa nne inatunyima raha na hatupati fursa nzuri ya kuweza kujisomea maana baadhi yetu huwa tunatoa harufu inakuwa shida…….Lakini tutafanyaje kwa kuwa tunatafuta elimu na sisi ni watoto wa familia za kimaskini,”alisema Aisha.
Changamoto nyingine wanazokumbana nazo katika kupata elimu shuleni hapo aliitaja kuwa ni uhaba wa baadhi ya vitabu na vifaa ya kuwawezesha kupata elimu kwa vitendo badala ya kupata elimu ya nadharia pekee.
Aliongeza kwa kusema ”somo la bayolojia, jografia na kemia hatusomi kikamilifu kutokana na ukosefu wa walimu na upungufu wa vitabu vya masomo haya,”alisema.
“Vitabu tunavyosomea vilivyopo ni vichache, hivyo huwalazimu kitabu kimoja kutumia wanafunzi wanne kwa wakati mmoja wakiwa darasani,”alisema.
Aliomba waongezewe vitabu,walimu na madawati angalau dawati moja kuweza kukaa wanafunzi wawili ili kuweza kuondokana na changamoto katika kupata elimu shuleni.
Sihaja Suluhu Ame mwanafunzi wa kidatu cha pili, alisema upatikanaji wa elimu Zanzibar ni mgumu kutokana na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu licha ya serikali kutangaza elimu bure.
Alisema kuwa anasikitishwa sana na tabia za baadhi ya wazazi na walezi, kutofuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni ili kuweza kujuwa maendeleo ikiwemo ufaulu wao.
“Mfano mzuri kama mimi, wazazi wangu tokea nimeanza darasa la kwanza hadi sasa nipo darasa la kumi, naishi na mama na baba lakini hakuna hata siku moja maendeleo yangu ya shule yamefuatiliwa mfano kuangalia madaftari yangu au kutaka kujua ufaulu wangu,”alisikitika Sihaja.
Alisema huwa anajisikia unyonge anapoona baadhi ya wazazi wanafuatilia maendeleo ya elimu kwa watoto wao.
Alisema wazazi wake mkazo mkubwa ni kutaka kujua muda wa kurudi kwao akitokea shule na inapotokea akachelewa kurudi nyumbani ndipo wanapomkaripia na kutaka kujua sababu za kuchelewa .
“Wazazi wangu wamekuwa na hofu tu pale wanapoona nimechelewa kurudi nyumbani, baada ya muda wa kuondoka shule umepita,haswa kwa sisi watoto wa kike wanahisi labda tushaenda kwenda kufanya mambo maovu,”alisema.
Alisema mzazi wake hana tabia ya kufahamu alichofundishwa shuleni,wala kutaka kujua ufahamu wake ukoje, wanachokazania ni kurudi nyumbani mapema baada ya muda wa kuwa shule kwisha.
Mwalimu mmoja wa shule hiyo ambae hautaka kutajwa jina lake, alikiri kuwepo uchache wa madawati, vitabu vya kufundishia na idadi kubwa ya wanafunzi darasani.
Alisema tokea serikali iliposisitiza lazima watoto wanaofikia umri wa miaka sita kuanza shule ya msingi na kutangaza elimu kuwa bure, muamko wa jamii umeongozeka wa kuwapeleka watoto shuleni.
Mwamko huo umeongezeka kwa wazazi kuwasukumia ulezi walimu peke yao, kwani idadi kubwa ya wazazi na walezi hawana utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao mashuleni.
“Hali hii ya wazazi au walezi kuwasukumia walimu pekee yao ulezi wa watoto wao katika kupata elimu upo zaidi vijijini kuliko mjini,”alisema.
Aidha alisema tayari tatizo la uhaba wa walimu haswa wa masomo ya sayansi,uhaba wa vitabu na uchache wa madawati wameshawasilisha wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar ili kuweza kufanyiwa kazi.
Alisema Shule ya Tunguu ina wanafunzi 598 na ina madawati 105 na ina walimu 16 lakini licha ya kuwepo kwa changamoto hizo, wamekuwa wakijitahidi katika uwajibikaji na utendaji kazi ili wanafunzi waweze kupata elimu.
Wizara ya Elimu Zanzibar imesema wanafunzi 43, 409 wa Msingi waliandikishwa kuanza masomo katika Shule za serikali Unguja na Pemba kwa mwaka huu wa 2016.
Unguja waliandikishwa wanafunzi 27,939 kati yao wasichana 13,924 na wavulana 14,015. Pemba walikuwa 15,470 wasichana 7,492 na wavulana ni 7,839.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Maandalizi na Msingi, Safia Ali Rijali, alisema ongezeko la wanafunzi walioandikishwa kuanza elimu ya msingi katika shule za Serikali limeongezeka zaidi ikilinganishwa na mwaka jana.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema ongezeko hilo limetokana na Wizara hiyo kufanya uhamasishaji kwa wazazi na walezi wajitokeze kwa wingi kwenda kuwaandikisha watoto wao ili kupata elimu.
Alisema kuwa ongezeko hilo pia limechangiwa na serikali kutangaza elimu ya maandalizi na msingi ni bure katika shule za serikali.
“Tangu Mheshimiwa Rais alipotoa tangazo kuwa elimu itolewe bure, ndipo wazazi na walezi walijitokeza kwa wingi kuwaandikisha watoto wao kwa lengo la kupata elimu na kuonekana kuwa hadi watoto wanaosoma shule binafsi wamewatoa watoto wao na kuwaandikisha katika shule za Serikali,” alisema Mkurugenzi Safia.
“Mwaka jana tulipokea wanafunzi asilimia ndogo, ila kwa mwaka huu asilimia imeongezeka mara mbili yake na mwaka jana UNICEF pia ilifanya utafiti ukagundua kuwa, watoto wengi hawakwenda kuandikishwa na sisi wizara tulitoka kwenda kuwatafuta na tukajua kweli wapo wengi,” alifahamisha.
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo alikiri kuwepo ongezeko kubwa la wanafunzi shule hali iliyosababisha wanafunzi kukaa chini pia msongamano wa wanafunzi darasani.
Alisema ongezeko hilo lipo zaidi katika wilaya ya Magharibi Unguja, ikilinganishwa na mikoa yote ya Zanzibar.
Alisema katika kutatua tatizo hilo, wizara imejipanga kujenga majengo ya shule na madawati ili kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi darasani na kukaa chini.
“ Wizara ya elimu imejipanga kuwatafuta walimu haswa wa sayansi ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu,”alisema.










