Na kwa namna alivyopigana hadi sasa, hii inatupa fundisho kwamba kwa kila mwenye ulemavu awe amezaliwa au amekutana nao ukubwani kwa sababu mbalimbali akiwa na kipaji bado anaweza kufikia ndoto zake za juu akipewa ushirikiano wa kutosha.
Hili limedhihirishwa kwa Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ya Watu wenye Ulemavu (Tembo Warriors) walivyofanya vizuri ikiwa ni mara yao ya kufuzu na kucheza michuano ya Kombe la Dunia nchini Uturuki mwaka huu, ambapo ilifika hatua ya robo fainali.
Wapo wachezaji wengi waliofanikisha hilo, lakini kwa leo hapa tunaye kipa namba moja wa Tembo Warriors, Ali Juma Abdalla, ambaye ni mlemavu wa mkono (ana mkono mmoja), ana mengi ya kusisimua kuhusu maisha yake ya soka, twende sasa...
Alivyoanza soka
"Nilianza kucheza mpira nikiwa shuleni timu za madarasa baada ya hapo nikawa nacheza timu za mtaani na timu za ligi tofauti tofauti wakati huo nilikua sijapata ulemavu wa mkono, nilikuwa na mikono yote miwili.
"Timu nilizowahi kuzichezea kabla sijapata ulemavu wa mkono Chuoni fc na Amani Fresh, pamoja na Amani Fresh FC.
"Amani Fresh wakati huo ilikuwa Daraja la Tatu kabla ya kutua Negro FC nakuwa miongoni mwa wachezaji walioipandisha hadi Daraja la Pili," anasema Ally ambaye alizaliwa Oktoba 8, 1990, Mjini Magharibi, Zanzibar na kupata elimu visiwani humo hadi Kidato cha Nne.
Kupata ulemavu
Anasema amezaliwa akiwa mzima, mikono yake ikiwa kamili, lakini harakati zake za maisha ya soka ndizo zilizomsababishia hali hiyo.
"Ulemavu niliupata nikiwa mkubwa mnamo Septemba Mosi, 2011. Wakati huo tulikuwa tunarudi nyumbani kutoka kucheza mechi, ilikua ni muda wa jioni tunatoka kijijini kurudi mjini kwa bahati mbaya tukapata ajali ya gari.
"Kuna wachezaji wengine watatu waliumia kidogo tu, lakini mimi pekee ndiye nilivunjika mkono. Nilikaa siti ya mbele wakati ile gari inaanguka ililalia upande wangu na ndipo apo ulipovunjika mkono wangu wa kushoto na kulazimika kukatwa kabisa wakati huo nilikuwa naichezea Negro FC."
Baada ya ulemavu
"Nilikuwa na kipindi kigumu sana, sikuweza kufikiria chochote zaidi ya kuwapo katika wimbi kubwa la mawazo, ilichukuwa muda zaidi ya mwaka kukubaliana na hali hiyo," anasema.
Anasema kwa kuwa ndoto zake ni kucheza soka hali ambayo ndoto hiyo aliamini tayari imepotea baada ya ajali hiyo, hivyo soka la ushindani aliona halitawezekana tena kwake.
"Ilinichukua miezi kadhaa kukubaliana na hali yangu ya ulemavu baada ya kupona, nikawa naenda kucheza mazoezi na wasio na ulemavu wowote, nikiamini njia ya kujipa furaha kwa sababu ya kupoteza ndoto zangu," anasema kipa huyo.
Anasema baada ya kipindi kifupi kufanya mazoezi na timu zingine zilizokuwa na wachezaji ambao hawana ulemavu, hakuwahi kuwaza kama kuna siku ndoto zake za kucheza soka la watu wenye ulemavu zinaweza kutokea.
Baada ya kujiunga na timu ya watu wenye ulemavu
"Nilijisikia vizuri na matumaini ya kufikia ndoto zangu niliona ni njia sasa ya kwenda kutimia kwa sababu naweza kupata nafasi ya kucheza kulingana na uwezo wangu wa kucheza nafasi nyingi.
"Nilipata nafasi ya kuitwa katika Klabu ya Drogheda FC, maskani yake iliyopo Dar es Salaam, inayoshiriki Ligi ya Watu wenye Ulemavu, ambayo nacheza nafasi ya kipa hadi sasa," anasema kipa huyo.
Anasema kabla ya kupata ajali alikuwa akicheza nafasi ya kipa, lakini akiwa na uwezo wa kucheza nafasi mbili tofauti namba tatu na 11, ila baada ya ajali akaamua kubobea katika nafasi ya kipa kwa sababu ya sheria za mchezo huo wa soka la watu wenye ulemavu.
Kuitwa Tembo Warriors
Anasema mchezaji wa mchezo wowote ule, hakuna ambaye hatamani kuchezea timu ya taifa na ndivyo ilivyokuwa kwake, ndoto ambayo imetimia.
"Nilijisikia furaha sana maana nilikua natamani sana kuitumikia timu ya taifa langu kupitia kipaji changu, kitu hicho nimefanikiwa katika maisha yangu," anasema Ally.
Sapoti ya familia
"Kwetu tupo tisa, kati ya hao hakuna anayecheza mpira zaidi ya mimi mwenyewe, bahati nzuri nilipata ushirikiano mzuri katika familia yangu kabla ya kupata ulemavu na hata sasa hivi nikiwa katika hii hali."
Changamoto
"Nilikutana na unyanyasaji wakati sijapata timu ya kucheza, kipindi nacheza timu za mtaani, wachezaji wa timu pinzani walinikejeli kwa ulemavu wangu na kuniambia kuwa soka ndio basi.
"Niliumia sana na kuendelea kukata tamaa ya kuwa ipo siku nitakuja kutimiza ndoto zangu za kucheza soka la ushindani," anasema Ally kwa masikitiko.
Anasema anamshukuru rafiki yake Ali Khatib, ambaye naye alikuwa mlemavu akiishi Dar es Salaam, siku moja alifika Zanzibar kwa shughuli za Chama cha Watu wenye Ulemavu kwa ajili ya elimu ya ujasiriamali.
"Tulipokutana hapo aliniahidi atanisaidia kutimiza ndoto zangu, alirejea Dar es Salaam, kisha baadaye alinipigia simu na kunieleza naweza kutimiza ndoto za kucheza soka la ushindani bila unyanyasaji baada ya Tanzania kuanzisha soka la Watu wenye Ulemavu," anasema Ally.
Mechi ya kukumbukwa
"Mechi ambayo sitaweza kuisahau ni wakati nipo Negro fc dhidi ya Mgeni Haji, ilikuwa mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na ligi ndio mechi yangu ya mwisho wakati tunarudi nyumbani nikapata ajali na kusababisha ulemavu huu nilio nao hadi sasa," anasema kipa huyo.
Anasema ndoto zake kubwa ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na kuendelea kupambania nafasi ya kipa namba moja wa Tembo Warriors kwa mafanikio makubwa zaidi ya msimu huu.
Kombe la Dunia Uturuki
"Ilikuwa ni ngumu sana hasa ukizingati ugeni niliokuwa nao katika mashindano kwani ilikua mara yangu ya kwanza kushiriki Kombe la Dunia, nilikosa uzoefu.
"Nashukuru Mungu makocha waliweza kunisaidia kwa kunipa moyo na kunipa ujasiri kwamba naweza kufanya vizuri zaidi ya makipa wa timu zilizopo hapo hali hiyo imenisaidia na kufanikisha Tembo Warriors kufika hatua ya robo fainali lakini pia Tanzania kuwa nchi ya saba katika viwango ubora vya dunia kwa timu za watu wenye ulemavu," anasema Ally.
Ushauri kwa wazazi
Anasema kuzaliwa na ulemavu au kupata ulemavu haimanishi huwezi kufanya vitu vikubwa. Naamini mtu mwenye ulemavu anaweza akafanya vitu vikubwa kuliko hata asiye na ulemavu.
"Nawashauri wazazi na walezi wasiwafungie watoto wenye ulemavu, wawape elimu watambue vipaji vyao na waviendeleze maana ulemavu ni hali ya kawaida tu kwa kipindi hiki," anasema kipa huyo wa Tembo Warriors.










