Nyota wakubwa Kombe la Dunia 2022

31Oct 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe
Nyota wakubwa Kombe la Dunia 2022

KOMBE la Dunia ni onyesho la wanasoka bora zaidi duniani, lakini michuano ya Qatar inaweza kuwa ya mwisho kwa kundi la nyota mashuhuri, pamoja na kuibuka kwa kizazi kipya cha kuvutia cha vipaji.

Lionel Messi na Cristiano Ronaldo huenda hii itakuwa michuano ya mwisho kwa nyota hao.

Hata hivyo, pamoja na Messi na Ronaldo wanaowania taji lao la kwanza la dunia, mabingwa watetezi Ufaransa kwa mara nyingine wataongozwa na nyota wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe.

 

Linaanza lini?

Michuano ya Kombe la Dunia itaanza katika hatua ya makundi kuanzia Novemba 20, mwaka huu, huku wenyeji Qatar wakifungua pazia la michuano hiyo kwenye Uwanja wa Al Bayt katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Ecuador wa Kundi A na fainali yake itafanyika Uwanja wa Lusail, Desemba 18, mwaka huu.

 

Ratiba

Desemba 2: Michezo ya Mwisho ya Makundi

Desemba 3-6: Raundi ya 16, Desemba 9-10 Robo fainali, Desemba 13-14: Nusu fainali,  Desemba 17: Mechi ya Nafasi ya Tatu, Desemba 18: Fainali.

 

Nyota wakubwa

Michuano iliyopita ya Kombe la Dunia ilitoa majina ya wachezaji wakubwa na hapa tunawaangalia nyota wakubwa zaidi kwenye mashindano haya.

 

Kylian Mbappe (Ufaransa)

Mbappe alikuwa bora kwa Ufaransa wakati kikosi cha Didier Deschamps kikinyakua taji la dunia mwaka 2018, lakini nyota huyo wa PSG amepanda kiwango kingine katika misimu miwili iliyopita na atakuwa mmoja wa wachezaji bora kwa mabingwa hao watetezi.

 

Lionel Messi (Argentina)

Mazungumzo ya kufifia kwa uwezo wa Messi ulikuwa mjadala katika miaka michache iliyopita, huku Muargentina huyo akionyesha vipaji vyake kule PSG. Macho yote yataelekezwa kwake huku akitarajia hatimaye kuongeza Kombe la Dunia kwenye orodha yake ya mataji.

 

Kevin De Bruyne (Ubelgiji)

De Bruyne atapewa jukumu la kuisaidia Ubelgiji kuwa na nafasi kubwa kule Qatar. Hata hivyo, Mchezaji huyo wa Manchester City ataazimia kujidhihirisha kama kiungo namba moja katika soka la dunia.

 

Cristiano Ronaldo (Ureno)

Licha ya wakati wa taabu ndani ya Manchester United, matarajio bado yatakuwa makubwa kwa Ronaldo huko Qatar, wakati anashiriki katika fainali ya tano, lakini Ureno ililazimika kufanya kazi ya ziada kupitia mchujo wa kufuzu. Hatimaye waliifunga Macedonia Kaskazini na kujihakikishia nafasi yao kwenye michuano hiyo na mabingwa hao wa Ulaya wa 2016 wataangalia tena uwezo wa Ronaldo wa kuongoza safu yao ya ushambuliaji kama nguzo kuu.

 

Vinicius Jr (Brazil)

Licha ya shinikizo la kujiweka kama mchezaji muhimu kwa Real Madrid na Brazil katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Vinicius Jr amepanda changamoto hiyo kwa njia ya ajabu. Ushirikiano wake na Karim Benzema kule Madrid pia ana uwezo wake wa kiwango cha juu kumfanya kuwa mmoja wa majina ya nyota wa Qatar 2022.

 

Takefusa Kubo (Japan)

Akiwa na umri wa miaka 21 pekee, Takefusa Kubo tayari amejitengenezea jina lake kabisa - baada ya kuibuka na lebo ya 'wonderkid' kwenye LaLiga akiwa na Barcelona na kisha Real Madrid. Kiungo huyo wa Kijapani alihamia Real Sociedad katika dirisha la usajili la majira ya joto mwaka huu (ingawa Real wamebakisha umiliki wake kwa asilimia 50, na wanaweza kumrejesha kwenye mji mkuu wa Hispania hadi 2025) na anathibitisha mara kwa mara uwezo wake wa mchezaji muhimu kwa Japan.

 

Virgil van Dijk (Uholanzi)

Licha ya kucheza nafasi ya safu ya ulinzi ya Liverpool, Van Dijk hajawahi kushiriki Kombe la Dunia akiwa na taifa lake. Waholanzi wana nguvu zaidi kwenye safu ya nyuma na katikati kuliko ilivyokuwa miaka ya hivi karibuni, Van Dijk atakuwa na lengo la kuimarisha kundi la wachezaji bora katika nafasi yake kwenye soka duniani.

 

Neymar (Brazil)

Mbrazil huyu anaendelea kubeba mzigo wa matumaini ya nchi yake kwenye hatua kubwa zaidi na Qatar 2022 haitakuwa tofauti. Taifa linatarajia wakati wowote Neymar atakapovaa jezi na atakuwa na hamu ya kuwaongoza 'Selecao' hao kutwaa taji lao la kwanza la dunia tangu mwaka 2002.

 

Pedri (Hispania)

Nyota wa 'La Roja', Pedri ndiye kiungo bora zaidi kwenye safu ya kiungo ya Hispania, ambayo hapo awali imewatoa Sergio Busquets, Andres Iniesta na Xavi. Lakini, kuna maoni kule Camp Nou kwamba, Pedri siku moja anaweza kuwazidi watangulizi wake wa Barcelona na atatafuta kuendeleza mafanikio mazuri kwenye Euro 2020.

 

Karim Benzema (Ufaransa)

Uamuzi wa Deschamps wa kumwondoa Benzema kwenye michuano ya Euro 2020 ulikabiliwa na jibu tofauti la umma nchini Ufaransa, 'Les Bleus' walipotoka katika michuano hiyo katika hatua ya 16-bora. Na sasa ana nafasi kubwa kwenye michuano ya Kombe la Dunia.

 

Luka Modric (Croatia)

Modric ana uwezekano wa kuwafuata wachezaji kama Ronaldo, Messi na Benzema katika kumaliza muda wa kucheza soka la kimataifa baada ya Kombe la Dunia, lakini kiungo huyo mwenye umri wa miaka 37, atadhamiria kuiongoza Croatia kupata mafanikio pale Qatar, na licha ya umri wake kuwa mkubwa, anabakia kuwa nyota muhimu kwa nchi hiyo.

 

Alphonso Davies (Canada)

Canada wamefuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu nchini Mexico mwaka 1986. Mwitikio wa kihisia wa mchezaji huyo wa Bayern Munich kwenye mitandao ya kijamii kwa Canada kupata nafasi yao Qatar ulionyesha umuhimu wake na atakuwa na hamu ya kung'ara kwenye hatua kubwa zaidi.

 

Christian Pulisic (Marekani)

Kama Marekani itahitaji kufika mbali zaidi katika mashindano hayo, watamhitaji Pulisic kuwaongoza. Mchezaji huyo wa Chelsea amekuwa kinara wa kampeni zao za kufuzu, na atatumaini kuchukua uzoefu wake wa mechi kubwa katika ngazi ya klabu hadi kwenye hatua ya dunia akiwa chini ya Kocha Gregg Berhalter.

 

Son Heung-min (Korea Kusini)

Son ameonyesha mara kwa mara katika maisha yake yote akiwa na Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England, kwamba ana uwezo wa kuwa na kipaji cha kipekee, akifunga baadhi ya mabao ya kuvutia zaidi kwenye ligi. Katika kiwango cha kimataifa ana mabao zaidi ya 30 kwa jina lake, na atakuwa miongoni mwa washambuliaji wanaotarajiwa kung'ara.

 

Harry Kane (England)

Nahodha wa England Kane atakuwa mtu muhimu kwa kikosi cha kocha, Gareth Southgate huku 'Simba Watatu' hao wakipania kuendeleza kiwango chao. Kane alijiimarisha katika kiwango cha juu katika kipindi cha pili cha msimu wa 2021/22 wa Ligi Kuu England.

 

Nyota watakaokosa Kombe la Dunia

Wakati Messi, Neymar, Kane na wengine wote watakuwa kwenye ndege kuelekea Mashariki ya Kati, majina kadhaa ya nyota yatalazimika kuridhika na kutazama mchezo huo yakiwa nyumbani.

Italia ilishindwa kufuzu mbele ya Macedonia Kaskazini na hiyo inamaanisha kwamba, Jorginho, Marco Verratti na wachezaji wenzao walioshinda Euro 2020 hawatakuwapo Qatar.

Mohamed Salah hatakuwapo pia, kwani nyota huyo wa Liverpool na Misri alishindwa katika mechi yao dhidi ya Senegal ya kuwania kufuzu katika Kanda ya Afrika, kwenye marudio ya fainali ya AFCON 2022.

Orodha ya waliothibitishwa kutokuwapo pia inajumuisha majina mengine kama Erling Haaland (Norway), Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon), Naby Keita (Guinea) na Edin Dzeko (Bosnia), wote wakibakia nyumbani baada ya nchi zao kushindwa kufuzu.