Kila mchezaji amepata gari aina ya Toyota Prado, lenye thamani zaidi ya milioni 120, pamoja na medali.
Katika mchezo wa fainali DRC iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mali.
Hii ni mara ya pili kwa Kongo kushinda kombe hilo. Mara ya kwanza ililinyakua wakati tu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 2007.
Sishangazwi na uamuzi wa Serikali ya Kabila kuwazawadia wachezaji hawa magari na medali za heshima.
Tulitaka afanye nini tena zaidi ya kuwapa wachezaji zawadi hiyo baada ya kuandika historia ya kutwaa taji la kwanza, lakini pia historia nyingine ya kuwa timu ya kwanza kutwaa taji mara mbili.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ilitolewa kwenye hatua za awali kuingia kwenye fainali hizo zilizofanyika nchini Rwanda, ilipochapwa mabao 3-0 na Uganda mjini Zanzibar na kulazimishwa sare ya bao 1-1 nchini Kampala Julai mwaka jana.
Wadau wengi wa soka wamekuwa wakijiuliza ni kwa nini nchi kama Kongo ambayo haitofautiani sana na Tanzania kiuchumi, huku ikiwa kwenye migogoro wa kisiasa kwa muda mrefu, baadhi ya maeneo kukiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini imekuwa iko vizuri linapokuja suala la soka?
Na kwanini Tanzania inashidwa kupiga hatua ikiwa imeizidi Kongo vitu kadhaa ikiwemo amani na utulivu?
Wala haiitaji elimu kujua kuwa tatizo kubwa ni uongozi, lakini pia Watanzania kuwa na tabia ya kuingiza siasa kwenye mambo ya yanayoitaji utaalamu.
Wabongo hata mashabiki wa soka tu tumekuwa na mitazamo myepesi linapokuja swali ni kwa nini soka linaporomoka kila kukicha.
Kwenye bayana hatupataki, ila tunakuwa na majibu mepesi kwenye maswali magumu.
Hadi leo wapo wanaoamini kuwa soka la Tanzania halisongi mbele kwa sababu Ligi ya Tanzania ina wachezaji wengi wa kigeni.
Wanataka wapunguzwe kutoka saba waliopo, hadi matatu na wengine hawataki kabisa kusikia habari ya wachezaji kutoka nje ya nchi.
Kisa eti wanasababisha soka la Bongo kudidimia kwa sababu wanawanyima nafasi wachezaji wazawa.
Wakongo wametuumbua. TP Mazembe ina robo tatu ya wachezaji kutoka nje ya nchi, wakiwemo Watanzania kina Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Lakini wachache waliobaki, wakiungana na wa timu nyingine wamekwenda nchini Rwanda na kutwaa kombe la CHAN.
Uwepo wa wachezaji wa kugeni kwenye Ligi ya Kongo hakukuwazuia wachezaji waliobaki kuwa wa viwango vya kufanya vizuri kwenye mechi za kimataifa.
Tena wachezaji wa kigeni Kongo ni wengi zaidi kuliko saba wa hapa Bongo ambao sana sana wapo kwenye timu tatu tu za Simba, Yanga na Azam.
Timu zilizobaki zenye wachezaji mmoja mmoja au wawili, ukiwachanganya sidhani kama wanafika 10.
Katika timu kama Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, JKT Ruvu na Mwadui FC, hakuna mchezaji wa kigeni.
Wanazuiwa na nani kucheza na kuonyesha uwezo wao utakaowafanya kuchaguliwa timu ya taifa ili soka letu liinuke?
Ukiangalia kwa sasa hata kwenye mbio za ufungaji bora, wageni Hamisi Kiiza wa Simba na Amissi Tambwe wa Yanga wanafukuzana kila kukicha kwa kupachika mabao.
Si kama hakuna mastraika wa Kitanzania la hasha. Wapo na wanafunga, lakini mara nyingi wamekuwa hawana muendelezo. Wakifunga mechi tatu watacheza mechi nne mfululizo bila kufunga goli.
Hata wanaowika na kufunga kwa sasa, hakuna uhakika wa kuwa wataendelea kufunga mechi zijazo, ndiyo maana inakuwa shida hata kuwachagua timu ya taifa.
Wako wapi kina Malimi Busungu, Rashid Mandawa, Simon Msuva ambao walitisha kwa kufunga magoli msimu uliopita?
Hawako kwenye kiwango kile, lakini Tambwe aliyekuwa Simba msimu mwaka juzi ni yuleyule wa Yanga. Bado anaendelea kufunga anavyojisikia.
Kiiza aliyekuwa Yanga misimu kadhaa iliyopita, ndiye huyuhuyu ambaye yupo Simba. Kiwango chake cha kutupia ni kilekile kila anapopata nafasi.
Tatizo la kuporomoka soka la Tanzania ni pana na wala si la kuliangalia juu-juu na kutoa uamuzi.
Kwanza kabisa tatizo linaanzia kwa wachezaji wenyewe ambao pamoja na kuwa na vipaji, lakini hawavitunzi wala kuvifanyia kazi kwa kujituma kama wenzetu Wakongo.
Wenzetu wana sifa moja. Kama akiwa mwanamuziki anakuwa mwanamuziki kweli. Akiwa mshonaji anakuwa mahiri. Mpambaji utampenda. Mchezaji kikapu anakuwa wa ukweli.
Akiwa mcheza soka ndiyo usiseme. Hii ni kwa sababu ya kujituma, kujitambua na kuthamini kile alichojaaliwa na Mungu na kukifanya kuwa ni kazi na si burudani au kumfurahisha mtu.
Wachezaji wetu Tanzania wana cha kujifunza kwa wenzao wa Kongo.
Ligi dhaifu na ya kubebana ya Kibongo nalo ni jipu. Imekuwa ikizalisha mabingwa wepesi kwa sababu kwanza kabisa inacheza na timu nyingi dhaifu.
Lakini pia hata hizo timu dhaifu, bado zinakandamizwa na baadhi ya waamuzi wabovu na wala rushwa ili timu kubwa zishinde.
Kongo kuna ligi ndefu inayoanza kuchezwa kwanza kwa mfumo wa majimbo, lakini timu nyingi ni ngumu zisizokubali kufungwa kirahisi, pia waamuzi wanaojua vema majukumu yao.
Yoyote anayekuwa bingwa nchini humo anakuwa ameiva kucheza mechi za kimataifa, pia anayechaguliwa kuunda timu ya taifa anakuwa mchezaji aliyekamilika, kucheza mechi nyingi na kukomaa kimashindano.
Kilichotokea kwa wenzetu Kongo nadhani linaweza kuwa somo na hakuna ubaya kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi yake ya Ligi kuangalia uwezekano wa kuomba ziara ya kwenda kujifunza ni jinsi gani anavyoendesha soka nchini humo.










