‘Siyo bure, kuna mkono wa mtu’

15Feb 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
‘Siyo bure, kuna mkono wa mtu’

KAMA haya yanayotokea kwenye mechi za Ligi Kuu Bara kati ya Mtibwa na Stand United, yangetokea pia kwenye mechi kati ya Simba na Yanga, mashabiki wangesema: ‘Siyo bure, kuna mkono wa mtu’.

WACHEZAJI WA STEDI UNITED

Unajua kinachozikuta timu za Mtibwa na Stand United katika mechi zao tatu sasa? Ni kutomalizika mechi zao kutokana na mvua kunyesha, hivyo kulazimika kuendelea kwa dakika zilizobaki siku inayofuata.

Hii ni ajabu katika mechi za ligi. Tuanze na mechi ya wiki iliyopita baina ya timu hizo. Mechi ilivunjika kutokana na mvua kubwa kunyesha na kurudiwa tena kesho yake asubuhi kwenye Uwanja wa Manungu mjini Morogoro, ikiwa ni mara ya tatu kwa timu hizo kurudiana baada mechi zao kuvunjika kwa mvua.

Msimu uliopita wa Ligi Kuu 2014/15, mechi zote mbili za nyumbani na ugenini baina ya timu hizo zilivunjika kutokana na mvua kubwa na kusababisha uwanja kutochezeka.

Ajabu nyingine ni kwamba mechi zote za Ligi Kuu zilizovunjika msimu uliopita ukichilia mbali baina ya timu hizo mbili, pia zinaihusisha timu hizo mbili dhidi ya Kagera Sugar.

Pia mechi zote tano za msimu uliopita na huu, zimevunjika kwenye viwanja viwili tu ambavyo ni Manungu na Kambarage mjini Shinyanga.

Mechi zote zilizovunjika zililazimika kuchezwa asubuhi, hivyo kuzifanya timu hizo kuwa 'wazee wa asubuhi'.
Kwa uthibitisho wa hili, mwandishi wa makala haya amekusanya mechi zote za msimu uliopita na huu zilizovunjika kutokana na mvua kubwa kunyesha, akianza na mechi zote tatu baina ya Mtibwa Sugar na Stand United.

1. Mtibwa Sugar 1-1 Stand United (Manungu)

Mechi hii ilichezwa mara ya kwanza Desemba 27, 2014 Ligi Kuu msimu uliopita wa 2014/15 kwenye Uwanja wa Manungu Turiani mjini Morogoro.

Mechi hiyo ilichezwa kwa dakika 28 tu kabla ya kuahirishwa kutokana na mvua kubwa kunyesha na maji kujaa uwanjani.
Wakati mechi inavunjika Stand United ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Shaaban Kondo dakika ya 22.

Hata hivyo, ulivyorudiwa kesho yake asubuhi Desemba 28 kwa dakika 84, Mtibwa ilifanikiwa kusawazisha bao lililofungwa na Said Mkopi dakika ya 86.

Kwa hali hiyo ni kwamba Stand ilifunga bao na Mtibwa ikarudisha kesho yake.

2. Stand United 1-0 Mtibwa Sugar (Kambarage)

Hali iliendelea hivyo kwenye mechi ya marudiano ya mzunguko wa pili Ligi Kuu msimu uliopita 2014/15 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mvua kubwa ilinyesha na kwa mara nyingine tena mechi hiyo kuvunjwa dakika baada ya 33 tu.
Mechi hiyo ilichezwa Aprili 4 mwaka jana.

Wakati mvua ikivunja mechi hiyo, Stand ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 12 na Haruna Chanongo.
Mechi ilirudiwa keshi yake asubuhi Aprili 5 kwa dakika 57 zilizobaki na hakukuwa na bao lolote lililoingia, hivyo dakika 90 zikamalizika kwa Stand kushinda bao 1-0 lililofungwa jana yake.

3. Mtibwa Sugar 1-0 Stand United (Manungu)

Hii ndiyo mechi iliyochezwa Januari 30 kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Kama msimu uliopita mechi hiyo tena ikavunjika tena, ikiwa ni mara ya pili baina ya timu hizo kwenye uwanja huo, pia ni mara ya tatu tangu msimu uliopita.

Mvua kubwa kama kawaida ikanyesha na kusababisha mechi kushindwa kuendelea baada ya dakika 45 za kwanza kumalizika.

Wakati huo tayari Mtibwa Sugar ilikuwa imeshafunga bao 1-0 lililotiwa kwenye kamba na Mudhamir Yassin dakika ya 22.
Mechi ilirudiwa kesho yake Januari 31 asubuhi kwa dakika zingine 45, lakini matokeo yakabaki kama yalivyo.

4. Mtibwa Sugar 1-1 Kagera Sugar (Manungu)

Achilia mbali mechi tatu baina ya timu hizo, Mtibwa kama kawaida yake ni timu ambayo inaongoza kwa mechi zake kuvunjika kutokana na mvua, kwani Novemba 8, 2014 mechi yake dhidi ya ndugu zao wa Kagera Sugar pia haikumazika.
Mvua kubwa ilinyesha kwenye Uwanja wa Manungu na kusababisha mechi hiyo kuchezwa kipindi kimoja tu kwa dakika 45.

Wakati ukivunjwa Mtibwa ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Ame Ally, ambaye kwa sasa yupo Azam FC dakika ya 43, lakini uliporudiwa kesho yake Novemba 5, Kagera ilisawazisha dakika ya 56 kupitia kwa Rashid Mandawa ambaye kwa sasa anaichezea Mwadui FC.

5. Stand United 2-0 Kagera Sugar (Kambarage)

Kama nilivyosema ni kwamba mechi zote zilizovunjika inazihusu timu hizo tatu tu.
Mechi kati ya Stand United na Kagera Sugar nayo ilivunjika Februari 28 mwaka jana baada ya kuchezwa kwa dakika 80.
Mvua kubwa ilisababisha mechi hiyo isiendelee na kuchezwa tena Machi Mosi kwa dakika 10 zilizobaki.

Wakati inavunjika Stand ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Abasirim Chidiebere ambaye kwa sasa yupo Coastal Union, na uliporudiwa tena kesho yake kwa dakika 10, Chidiebere alifunga tena bao la pili dakika ya 85.