Umewahi kusikia hii? JKT Ruvu haijawahi kufunga Yanga katika mechi za Ligi Kuu Bara kwa miaka mitano sasa.
Mara ya mwisho maafande hao waliwazima Jangwani mwaka 2011.
Yanga imekuwa ikijipigia JKT inavyotaka na mbaya zaidi, wanaipiga mabao mengi balaa. Kipigo cha mwisho JKT kutoka Yanga kililikuwa wiki iliyopita, ambapo walichakazwa kwa mabao 4-0. Ikumbukwe pia kuwa mzunguko wa kwanza, Septemba 19 mwaka jana, JKT walikula kichapo cha mabao 4-1.
Takwimu za Nipashe zinaonyesha kuwa mara ya mwisho Maafande hao kupata ushindi dhidi ya Yanga ilikuwa Agosti 20, 2011, waliposhinda bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti dakika ya 22 na Kessy Mapande.
Mwandishi wa makala haya amekusanya rekodi za mechi zote za Yanga dhidi ya JKT Ruvu.
Rekodi hiyo inaanzia pale JKT Ruvu ilipopata ushindi kwa mara ya mwisho.
1. Yanga 0-1 JKT Ruvu (2011)
Ilikuwa ni mechi ya mwisho JKT Ruvu kupata ushindi kwani baada ya hapo si tu kwamba haipati ushindi, bali haina ubavu wa kutoka hata sare.
Ilikuwa ni Ligi Kuu msimu wa 2011/12 iliposhinda bao 1-0 likifungwa na Kessy Mapande kwa penalti dakika ya 22, mechi ikichezwa Agosti 20, 2011.
2. Yanga 3-1 JKT Ruvu (2012)
Ilikuwa ni mechi ya msimu huohuo wa ligi, ikiwa ni mzunguko wa pili, Yanga ilipoanza ubabe wake kwa kuitwanga JKT Ruvu mabao 3-1 Januari 28, 2012.
Yalikuwa ni magoli ya Hamisi Kiiza, straika ambaye kwa sasa anaichezea Simba, akifunga magoli mawili, Stephano Mwasika akifunga moja, huku Amosi Mgisa akiifungia JKT bao la kufutia machozi.
3. Yanga 4-1 JKT Ruvu (2012)
Dhahama iliendelea kuikumba JKT Ruvu msimu uliofuata wa 2012/13, ilipopokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Yanga, mechi iliyochezwa Septemba 22, 2012.
Wafungaji kwa washindi walikuwa ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Didier Kavumbagu anayeitumika Azam FC kwa sasa akifunga mawili na Simon Msuva moja, Credo Mwaipopo akifunga bao la kusawazisha kwa upande wa JKT.
4. Yanga 3-0 JKT Ruvu (2013)
Kama kawaida, Yanga iliendelea kujipigia JKT Ruvu inavyotaka, kwani Aprili 21 kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa ligi msimu huo, ilishinda mabao 3-1 yaliyofungwa na Msuva, Kiiza, na Nizar Khalfan ambaye kwa sasa yupo Mwadui FC.
5. Yanga 4-0 JKT Ruvu (2013)
Mambo yaliendelea vilevile, Yanga si tu kwamba ilikuwa ikizolea pointi, bali pia idadi kubwa ya magoli kutoka kwa maafande hao, kwani msimu wa 2013/14 iliifumua mabao 4-0, mechi ikipigwa Novemba Mosi, 2013.
Mabao mawili yalifungwa na Mrisho Ngasa ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa Afrika Kusini, Oscar Joshua na Tegete.
6. Yanga 5-1 JKT Ruvu (2014)
Idadi ya magoli iliongezeka mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu huo, kwani JKT Ruvu ilikubali kipigo cha ambao 5-1 kutoka kwa wababe wao.
Ilikuwa ni 'hat-trick' ya Ngasa, Kavumbagu na Hussein Javu, huku Idd Mbaga akiifungia JKT bao la kufutia machozi, mechi ikichezwa Aprili 6, 2014.
7. Yanga 2-1 JKT Ruvu (2014)
Hii ndiyo mechi pekee ambayo JKT Ruvu ilifungwa idadi ndogo ya magoli.
Ilikuwa ni Oktoba 5, 2014 msimu wa Ligi Kuu 2014/15.
Mabao ya Yanga yakifungwa na Kelvin Yondani na Haruna Niyonzima, Jabir Aziz akiifungia JKT Ruvu bao.
8. Yanga 3-1 JKT Ruvu (2015)
Mzunguko wa pili wa ligi msimu huo, Yanga ilirudia kama kawaida kutoka kichapo cha mabao 3-1 Machi 25, 2015, Msuva akifunga magoli mawili, Danny Rwanda anayeichezea Majimaji akifunga moja, Samuel Kamuntu akiifungia JKT.
9. Yanga 4-1 JKT Ruvu (2015)
Msimu huu wa ligi 2015/16 kwenye mzunguko wa kwanza, mechi ikichezwa Septemba 19 Yanga iliisulubu kama kawaida yake JKT Ruvu mabao 4-1 yaliyofungwa na Donald Ngoma, Amissi Tambwe aliyefunga mawili na Thabani Kamusoko akifunga moja. Michael Aidan aliifungia JKT bao.
10. Yanga 4-0 JKT Ruvu (2016)
Mechi hii ilichezwa Februari 7, mwaka huu, bado JKT Ruvu iliendelea kutoa takrima kwa Yanga baada ya kucharazwa mabao 4-0, yaliyofungwa na Msuva akifunga mawili, Isofou Boubacar na Ngoma pia akifunga bao moja.










