Kitaalamu inafafanuliwa kuwa ugonjwa wa kudumu unaosababishwa na bakteria. Huwa, baada ya maambukizo kuna kipindi kati ya miaka mitano hadi 20 dalili hazionekani wala mtu kuzisikia. Pale dalili zinaonekana, huwa kwa mfumo wa kupumua, ngozi na macho.
Dalili zinapoanza kuonekana, mgonjwa hasikii tena, baridi, joto au maumivu. Kwa hiyo, hatambui kirahisi kuwa na jeraha, vidonda kuuma wala kufahamu uchafu na bakteria kuingia mwilini.
Mara zote, vidonda vinaweza kuwa vikubwa kwa sababu havitibiwi au vinachelewa kutibiwa. Ndiyo sababu wenye ukoma hupoteza viungo mwilini kama vile vidole mguuni, kutokana na majeraha yanayojirudia na kuugua muda mrefu.
Pia, kuna macho kutoona, kunakomuathiri mgonjwa. Imekuwa kawaida, baadhi ya familia zina wagonjwa wa ukoma na wanashindwa kuwapeleka hospitalini, hata kuwasababishia ulemavu wa viungo. Katika kukabiliana na changamoto ya ugonjwa wa ukoma, jamii sasa inatakiwa kutoa taarifa mapema, ili aliye mgonjwa atibiwe mapema.
Vilevile kwenye kinga, inashauriwa kupatikane elimu sahihi ya kukabiliana na ukoma, serikali ikibeba mikakati ya kuutokomeza ukoma.Tayari Wizara ya Afya, imebainisha stahiki itayosaidia katika kutokomeza ugonjwa ukoma nchini, ifikapo mwaka 2030.
Hapo inajumuisha kutoa mafunzo elekezi kwa watoa huduma hasa katika maeneo yenye wagonjwa, pia elimu kwa jamii juu ya ugonjwa huo.
Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel anasema hayo jijini Dodoma katika tamko lake, Siku ya Ukoma Duniani akiwa na kaulimbiu "chukua hatua sasa, kutokomeza ukoma nchini."
"Serikali yetu imeendelea kuchukua hatua muhimu, ili kufikia malengo ya ‘Utokomezaji Ukoma katika Taifa Letu’ na tayari tumetengeneza mkakati wa kufikia visa sifuri vya Ukoma ifikapo mwaka 2030," anasema.
Anaongeza kwamba, kuna mkakati wa kutoa mafunzo elekezi kwa watoa huduma, hasa katika maeneo ambayo maradhi ukoma bado ni tatizo kwao.
Naibu Waziri Dk. Mollel anasema kupitia wataalamu katika maeneo ya kutoa huduma za ukoma, wizara inalenga kufanya uchunguzi katika kaya zote zenye wagonjwa, kuwabaini kuwaanzishia huduma mara moja wataogundulika kuugua.
Anaeleza kuwa, wizara inalenga kuongeza uwezo wa ufuatiliaji mwenendo wa ugonjwa ukoma katika vituo vyote vya kutoa huduma za afya nchini, ili kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Pia, Dk. Mollel ananena kwamba wizara inaendelea na juhudi kitafiti kuibua mbinu za kuharakisha kasi ya utokomezaji ugonjwa, kuona inaongezeka kwa kutambua mbinu mbalimbali za mapambano dhidi ya ukoma.
Hapo anawaelekeza Waganga Wakuu wa Halmashauri, kuhakikisha wanajumuisha shughuli za kutokomeza ukoma, sambamba na mikakati ya afya katika maeneo yao ya kazi.
Rai yake ni kwa mamalaka za mikoa kuhakikisha kila mgonjwa anayeibuliwa, anatambuliwa makazi yake, kijiji na kata anakotoka, iwe ndani au nje ya wilaya, hata mkoa.
Msisitizo wa waziri ni kwamba, kama mgonjwa atatokea nje ya mkoa husika, inapaswa kuhakikishwe taarifa zake zinapelekwa alikotoka, ili kusaidia ufuatiliaji na uchunguzi wa maambukizi, hata kuwezesha tiba na kinga ya maradhi husika.
Dk. Mollel anaagiza kwamba kila halmashauri kuhakikisha wanafuatilia mwenendo wa ukoma katika ukanda wao, wanakuwa na takwimu sahihi za wagonjwa kulingana na maeneo,vijiji au mitaa wanakopatikana.










