MUSWADA BIMA AFYA KWA WOTE

09Feb 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
MUSWADA BIMA AFYA KWA WOTE
  • Salamu na rai yake Rais mwaka jana, msimu wake ukiwa umetimu

“Mfuko huu utahakikisha mtu anapata matibabu yote anayopaswa kupata. Huu ni kama upatu ambao Watanzania wote tunakwenda kucheza na kati yetu atakayepatwa na shida, upatu huo unamsaidia,”

MUSWADA wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote uko mezani kuwasilishwa kwa mara ya pili kwenye kikao cha Bunge kinachoendelea jijini Dodoma. Matarajio ya kujadiliwa na kupitishwa, utekelezaji wake kuanza Julai Mosi mwaka huu. Ni taarifa ya neema kiafya kwa Watanzania wote. 

Katika rai yake kwa umma mwaka jana, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akiwasilisha hoja akatamka: “Niwaombe tutakapopitisha sheria hii Watanzania tukajiunge na mifuko ya bima.”

Ni kauli ya Dk. Samia akiwa kwenye mkutano na viongozi wa dini katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) mjini Dodoma.

Rais akabainisha kwamba, anaufahamu udhaifu uliopo kwenye mifuko ya bima na hatua zinazochukuliwa, hivyo akaahidi na kutoa rai kwamba, itakapoanzishwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, itakuwa madhubuti, pamoja na kanuni zitakazowezesha watu wote kutibiwa kwa ufanisi.

“Mfuko huu utahakikisha mtu anapata matibabu yote anayopaswa kupata. Huu ni kama upatu ambao Watanzania wote tunakwenda kucheza na kati yetu atakayepatwa na shida, upatu huo unamsaidia,” akatamka.

Rais Dk. Samia akaendelea:“Ni kupitia Bima ya Afya kwa Wote ndipo tutaweza kutoa matibabu kwa kila Mtanzania anayeishi ndani ya nchi yetu.

Kimsingi, ni nukuu nzito kwa kiongozi mkuu wa nchi, kwa namna alivyojipanga na serikali yake kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za matibabu.

Ikirejewa tamko hilo la mkuu wa nchi, inahamasisha umuhimu wa kila Mtanzania kujiunga na bima hiyo, kwani inaelezwa ugonjwa hauchagui umri, siku na wakati na bima ndiyo mwokozi wakati wowote.

Hadi sasa serikali iliyopo madarakani inaendelea na uwekezaji wa mahitaji ya miundombinu katika matibabu, katika maeneo mbalimbali nchini, ikisimamiwa kwa karibu na mwongozo wa kisera na Mpango wa Taifa wa Afya ya Msingi (MAM), wenye miaka 15 sasa.

Ikirejewa takwimu ni kwamba, hadi sasa asilimia 85 ya Watanzania hawana bima za afya, huku kukishuhudiwa matukio ya baadhi ya kaya zinazoelemewa na mahitaji ya kitabibu, kulazimika kuuza rasilimali zake, kupata fedha za kugharamia tiba.

Tafsiri ya Bima ya Afya kwa Wote, msingi wake ni utaratibu wa kuwezesha wananchi kupata huduma za matibabu kwa urahisi bila kikwazo cha fedha kwa kuchangia huduma hizo kabla ya kuugua.

Hivyo, basi dhana ya bima ya afya inajengwa katika misingi ya mshikamano wa kijamii katika kugharamia huduma za matibabu kwa makundi na hata atakapougua, anapata huduma bila ya kikwazo cha fedha.

MCHAKATO ULIKOTOKA

Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Afya Maandalizi ya Kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote yalianza tangu mwaka 2012 na kutokana na umuhimu wake, ililazimika kuchukua muda mrefu kuiandaa.

Ni hali inayotokea, huku kukishuhudiwa ongezeko la magonjwa na hasa yasiyoambukiza, ikiendana na gharama kubwa ya matibau. Inarejewa mfano wa magonjwa kama saratani, figo na moyo yako juu.

Kutokana na gharama kubwa za matibabu, baadhi ya wananchi wanashindwa kuzimudu na kupata athari za kiafya na wakati mwingine, hata kupoteza maisha kwa kukosa huduma bora za afya.

Ili kutatua changamoto hiyo, serikali ikadhamiria kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ili kuimarisha mfumo wake kwa kuwezesha wananchi kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua kwa kupitia bima, kuwawezesha kupata huduma bora za afya wakati wote wanapozihitaji karibu na maeneo wanakoishi.

Bado kumekuwapo magumu kwenye mifumo ya kugharamia, kama vile wananchi kukosa fedha za matibabu ya papo kwa hapo, idadi ndogo ya wananchi kujiunga na bima na hiari ambayo imesababisha wengi kujiunga na bima wakiwa wagonjwa.

Chimbuko la kuandaliwa kwa muswada huo, ni kutimiza wajibu wa serikali kikatiba wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya pasipo kikwazo.

Sheria iliyopo inaweka hiari wa umma katika kujiunga na bima ya afya, hatua inayotajwa kusababisha wengi kujiunga wakiwa tayari na matatizo ya kiafya.

MANUFAA YA BIMA

Yapo manufaa ambayo wananchi wamekuwa wakiyapata na watayapata , endapo sheria hiyo itapitishwa na bunge na kuanza kutekelezwa, kwa kundi kubwa la wananchi kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila ya kikwazo cha fedha.

Wizara ya Afya katika taarifa yake inahimiza kuwapo ustahimilivu wa mfuko huo katika kutoa huduma, kwa sababu wengi watachangia na sio wote wataugua; pia kutakuwapo uboreshaji huduma katika vituo vya kutoa huduma za afya vya umma.

Hapo panatajwa kuimarika upatikanaji dawa na vifaa tiba, kuanzia zahanati hadi hospitali ngazi ya taifa; kuna kuimarika usimamizi na udhibiti katika utoaji wa huduma kwenye mfuko wa bima za afya wa umma na binafsi.

Manufaa mengine yanatajwa ni kuimarishwa hali ya kipato kwa wananchi na kuwaondolea umasikini wananchi kutokana na gharama kubwa za matibabu na kuwawezesha kupanga mipango ya maendeleo.

SURA YA MUSWADA

Kupitishwa muswada huo, utawagusa zaidi walioko kwenye sekta binafsi na waliojiajiri, ikiwamo mashambani waliko Watanzania wengi zaidi.

“Watu walio katika sekta isiyo rasmi watajiunga kwa kaya au mtu mmoja mmoja, kaya itakuwa na watu sita, akiwamo mchangiaji na mwenza mmoja, pamoja na wategemezi wengine wanne.

“Wategemezi wa mchangiaji wanaweza kuwa baba, mama, wakwe, watoto wa kuzaa na kambo na ndugu wa damu mwenye umri usiozidi miaka 21. Kaya yenye wategemezi zaidi ya wanne itakuwa na fursa ya kuanzisha kaya nyingine,” inafafanua Wizara ya Afya, katika dodoso lake la maudhui ya muswada.

Inaelezwa, wanaojiunga na bima ya Afya kwa Wote, watanufaika na huduma ikiitwa “Kitita cha Mafao ya Huduma Muhimu (Standard Benefit Package) na kila skimu ya bima ya afya italazimika kuitoa, ikiwa ni haki ya kila mwanachama.

Kitita hicho kinatajwa kuzingatia huduma zote zilizopo katika mwongozo wa tiba, Orodha ya Taifa ya Dawa Muhimu (NEMLIT) na aina ya magonjwa kama ilivyoainishwa katika Miongozo ya Tiba ya Kimataifa.

Hapo kuna mambo kama vile: Ada ya uandikishaji na kumuona daktari; gharama za vipimo; dawa aina zote (NEMLIT); upasuaji mdogo na mkubwa; kulazwa; afya ya kinywa na meno, matibabu ya macho; vifaa saidizi (l na mazoezi ya viungo (physiotherapy), huduma  zikipatikana kuanzia ngazi ya zahanati, hospitali maalum hadi Hospitali ya Taifa na vituo vya umma, pia binafsi vilivyosajiliwa na skimu husika nchi nzima. Kwa mujibu  wa Wizara ya Afya, bima za afya,  zitasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) itakayokuwa na jukumu la kuhakikisha kila skimu inatimiza vigezo na wanachama watakuwa na nafasi ya kutoa malalamiko wanapoona hawaridhishwi  na huduma.