Hadi anakasimiwa madaraka ya sasa, Rais Dk Samia akitoka nafasi ya awali miaka miwili iliyopita, kutoka Makamu wa Rais nchini, ilikuwa marufuku kwa binti aliyepata mimba kurejea darasani.
Ni hali iliyochukua nafasi wakati huo, huku Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya ukaguzi wa hesabu wa miaka minne kati ya mwaka 2018 na 2021, akitumia vigezo vya halmashauri 27, amebaini idadi kubwa ya mabinti shule za msingi wanakatisha masomo kwa mimba.
Kwa mujibu wa CAG, hali ni mbaya zaidi ikiongozwa na Halmashauri ya Wilaya za Bunda (Mara), ikifuatiwa na Urambo (Tabora), kisha Tarime (Mara), huku Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ni kinara wa kunusuru wanafunzi wabaki masomoni kitaifa.
Mnamo mwaka 2019, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na kingine, Centre for Reproductive Rights, kiliwasilisha malalamiko kwa Kamati ya Wataalamu ya Haki na Ustawi wa Mtoto Afrika ((ACERWC)), kupinga kufukuzwa na kutengwa kwa wasichana wajawazito kutoka shule za umma nchini.
Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Fulgence Massawe, akihimiza haki ya wasichana wanaopata ujauzito kupata elimu na wanapaswa kuungwa mkono wasalie shuleni.
Pia, hata kabla ya hapo kwa miongo mingi, kumekuwapo nyendo za namna hiyo kusaka haki ya masomo kwa mwanafunzi anayeacha masomo
Mfano mojawapo ni mwaka 2013, asasi ya Centre for Reproductive Rights ilitoa chapisho inayoitwa ‘Forced Out: Mandatory Pregnancy Testing and the Expulsion of Pregnant Students in Tanzanian,’ mabinti wajawazito wakiangukia kwenye mimba. Pia, kuna kesi zilizofunguliwa mahakamani na wanaharakati kutetea mabinti shuleni kuhusu hali hiyo, pasipo mafanikio.
UAMUZI MGUMU
Mnamo Novemba mwaka juzi, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akatangaza rasmi uamuzi mgumu kuhusiana na hoja hiyo, sasa mabinti wanaopata mimba watawezeshwa kuendelea na masomo.
Salamu hizo zinazobeba mageuzi ya Rais Dk. Samia, katika miezi mitatu ya uongozi wake kitaifa, ilianza pale serikali ilipotangaza dhamira ya mageuzi kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa sababu ya mimba, sasa wajiandae kurejea masomoni kwenye Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
Ni hoja iliyoibua chereko kutoka kwa wanaharakati waliokuwa wakipaza sauti na kuishinikiza haki hiyo, sasa ‘kufumba na kufumbua’ imechukua nafasi yake.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk, Leonard Akwilapo, akawaambia wakuu wa vyuo tajwa, akiwataka kuhakikisha wanafunzi wa kike walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo mimba, wawape fursa warudi darasani. Akawaeleza wakuu wa vyuo hivyo, kutekeleza agizo hilo la kuwadahili wanafunzi hao kupitia alichotaja ‘Mpango wa Elimu Haina Mwisho ifikapo Mwaka 2022.’
Pia, Dk. Leonard Akwilapo akavitaka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, viwe vimesajiliwa vituo vya kufanyia mitihani ya kidato cha pili na nne, kuwezesha kurejesha wanafunzi wa kike waliokatiza masomo.
Katibu Mkuu anafafanua: “Tulikuwa na mabishano mazungumzo marefu kwenye mpango wa kuimarisha na kuboresha elimu ya sekondari hapa nchini, moja ya makubaliano ilikuwa kutoa fursa kwa wasichana ambao wamekatiza masomo kwa njia yoyote ile.
“Wapate fursa ya kurudi na kuendelea na masomo.Tukasema tutatumia vyuo vya maendeleo ya wananchi, lazima tuanze hatuna uwanja, sio suala la kujadiliana, mambo mengine ya walimu mtatuachia sisi.”
Kwa mujibu wa Dk. Akwilapo, wanafunzi hao watakaporejea masomoni ni katika vyuo 54, kuanzia mwaka 2022.
KUTOKA KWA WAZIRI
Akitangaza uamuzi wa maelekezo ya Rais Dk. Samia, waziri mwenye dhamana wakati huo miezi mitano baadaye, Novemba 24, 2021 jijini Dodoma, Prof. Joyce Ndalichako akasema wanafunzi wa shule za msingi na sekondari watakaokatisha masomo kutokana na sababu kama utoro, pia mimba watapewa fursa kurejea shule.
Waziri Prof. Ndalichako anatamka: “Leo natoa Waraka wa elimu ambao utaelezea ni lini wanafunzi watakaokatisha masomo kwa sababu ya mimba na changamoto nyingine watapaswa kurejea shuleni, leo leo natoa waraka hakuna kupoa zege halilali.”Anasema, serikali imefikia uamuzi huo kuwanusuru wapatao ujauzito watarudi darasani na kuendelea ma michakato ya kitaaluma kama walivyo wanafunzi.
SAMIA AWAINUA
Pale inaporejewa madai mbalimbali ikiwamo angalizo la CAG na ustawi wa mabinti masomoni kwamba sababu kuu za kuacha shule kwa wasichana zilihusiana na ujauzito uliochangiwa na umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni, asili ya familia na masuala ya binafsi, rais akachukua hatua.
Katika uamuzi unaohusiana na mtazamo huo, Rais Samia, mbali na kuelekeza wanaojifungua kurejea masomoni, Desemba mwaka jana akaelekeza Sh. Milioni 960 zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za Uhuru, zitumike kujenga mabweni ya shule nane za msingi, zenye wanafunzi walio na mahitaji maalum.
Hizo zinajumuisha Buhangija (Shinyanga), Goeko (Tabora), Darajani (Singida), Mtanga (Lindi), Songambele (Manyara), Msanzi (Rukwa), Idofi (Njombe), na Longido (Arusha).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, George Simbachawene, katika hilo anafafanua kuwa shule hizo zimekwishagawiwa fedha za kujenga mazingira rafiki kuwakimu wanafunzi hao wenye mahitaji maalumu.
“Ikiwa ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwajali na kuwajengea mazingira rafiki watu wenye mahitaji maalum hapa nchini, hili ni jambo kubwa na la kishujaa na la kupongezwa sana,” anasema.
Mnamo Oktoba mwaka jana katika azma ileile ya kujenga mazingira wezeshi kwa wanafunzi, Rais Dk. Samia akatoa Sh.bilioni mbili, kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa hizo, kuongeza kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuhakikisha wanafunzi wote wanaofaulu wanapata nafasi ya kuendelea na masomo.
Top of Form