Ukweli wa mafunzo hayo ambayo kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1960 jeshi hilo lilipoanzishwa hadi mwaka 1992, vijana wanaopata mafunzo ya mwaka mmoja au zaidi baada ya kidato cha nne, walilazimika kuhudhuria mafunzo ya mwaka mmoja kwa mujibu wa sheria.
Mbali na wanaohudhuria kwa mujibu wa sheria, pia wapo vijana waliojiunga na mafunzo kwa kujitolea na baadhi kuendelea kutumikia kwa utaratibu wa kujtolea hadi sasa.
Dhana kuu iliyomo ndani ya mafunzo ya JKT ni kujifunza mambo mbalimbali, yanayombadili kijana wa Kitanzania kupitia mitazamo mbalimbali.
Ushuhuda wa nini kinafanyika JKT, jeshi lililoanzishwa kwa ajili ya kufunza ulinzi, ukakamavu na uzalishaji, ni ushuhuda wa hivi karibuni vijana zaidi ya 1,000 kutoka mikoa mbalimbali wamefanikiwa kumaliza mafunzo ya miezi sita katika kambi ya Ruvu.
Ni mafunzo yaliyowatia hamasa vijana, baadhi wakitoka jamii za wafugaji, waliomba mafunzo hayo yangeongezwa muda hata kufikia miaka miwili. Kilichowavuta ni namna mafunzo yalivyotolewa kuwawezesha katika ustawi wa maadili kama vijana wa Kitanzania.
Miongoni mwa waliofaidika nayo wanayataja kupitia risala ya kuhitimu mafunzo
kwa kipindi chote cha miezi sita, walipata stadi za maisha kwa nadharia na vitendo.
Wanataja stadi hizo kuwa ni ujasiriamali wa kufuga kuku na bata, kilimo cha bustani kama vile nyanya, tikiti maji, vitunguu, mboga na ufugaji wa samaki na ng'ombe.
Wanasema kwamba sasa wamefunguliwa milango ya kujiajiri na kuwapa uwezo wa kuongeza kipato, jambo linalowakwamua mbali na umaskini.
Jingine walilojifunza ni mbinu za ulinzi katika kuwa na ujasiri, ukakamavu na usalama, kupitia mafunzo ya silaha za kivita, hali inayowapa utayari kupambana na adui, wanapojitoa kulinda nchi yao dhidi ya adui wa nchi.
KAULI YA MKUFUNZI MKUU
Mkuu wa Mafunzo na Utendaji wa Kivita katika Jeshi la Nchi Kavu la Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Brigedia Jenerali Fa Njau, anawaunga mkono vijana hao waliohudhuria mafunzo ya JKT kwa kujitolea, katika mafunzo ya Operesheni Kikwete. Anasema, sasa wako tayari kulitumikia taifa lao kiaskari kwa ari na ushupavu.
"Nina imani katika kipindi chote cha mafunzo, mmepata nafasi ya kujifunza mambo ambayo yatakuwa na faida kubwa kwenu binafsi, vyombo mbalimbali vya ulinzi, usalama, JKT, JWTZ na taifa kwa ujumla,” anasema Brigedia Njau.
Anaongeza kuwa, uwepo wao kumewafanya washirikiane katika mambo mbalimbali bila ya kujali tofuati zao kama vile elimu, kabila, dini, itikadi za siasa na maeneo waliyotoka.
Brigedia Njau anasema mafunzo waliyoyapata kambini Ruvu ni ya kuwajengea uzalendo kila mahali watakapokuwapo na anaongeza: “Mtu awe tayari kurudi nyumbani amalizapo mkataba wake na JKT.”
"Nimeamua kunukuu Ibara hiyo ya 3d katika fomu ya JKT, ili vijana mfahamu kwamba unapojiunga na JKT hakuna sehemu inaposema utapata ajira bali umalizapo mkataba na JKT uwe tayari kurudi nyumbani,'' anasema.
Anaongeza kuwa mafunzo hayo yanawasaidia vijana kujiajiri na anatoa mfano wa uzoefu alioushuhudia hivi karibuni kwa baadhi ya vijana wahitimu wa JKT kuandaa makundi ya kudai ajira, jambo analolisema ni utovu wa nidhamu na ukiukwaji wa kiapo cha utii, pamoja na mkataba waliotia saini.
FAIDA ZA JKT
Brigedia Njau anaorodhesha faida za vijana kujiunga na JKT ni kuwa wazalendo na wako tayari kuijenga nchi yao, kuulinda na kuitetea nchi kwa kutumia akili, nguvu na maarifa waliyo nayo kupitia mafunzo hayo.
Anataja faida nyingine ni vijana kuwa waadilifu na wanaoweza kufanya kazi mbalimbali, hasa za mikono kwa ufanisi, pia kuwa na taifa lenye watu wachapa kazi na wenye nidhamu ya utendaji.
Brigedia Njau anasema mafunzo ya JKT yanatoa vijana wajasiriamali kwenye nyanja kama vile kilimo, ufugaji na stadi za maisha.
Faida nyingine ni kuwa na taifa lenye upendo, uadilifu na mshikamano uliotukuka, ikiwamo na kuandaa viongozi wa baadaye ambao ni waadilifu wasiopenda rushwa na ubadhirifu.
Kamanda huyo mwandamizi wa jeshi anaeleza matumaini yake kwa vijana wa kujitolea wanaohitimu mafunzo hayo, kwamba watadumisha nidhamu, maarifa, ujuzi na weledi waliouopata katika kipindi chote.
Pia anawasihi vijana wanaomaliza mafunzo, endapo watakosa nafasi za kujiunga katika vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama, wasigeuke chanzo cha utovu wa nidhamu uraiani.
Bgrigedia Jenerali Njau anaelekeza rai kwa wazazi nao watoe mchango wa hali na mali kwa kuwahamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea, badala ya kuchagua kazi za ofisini.
MKUU WA KIKOSI
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Ruvu JKT, Meja Charles Mbuge, anasema kuwa mafunzo hayo yameondoa matabaka na kuwafanya kuwa kitu kimoja.
Anasema vijana hao wamejifunza mambo mbalimbali katika miezi hiyo sita. Wamejifunza kilimo, ujasiriamali, ufugaji, uvuvi, mafunzo ya kijeshi jambo linalowajengea mazingira ya kujiajri baada ya hapo.
Meja Mbuge anasema kuwa,
wameweza kulima hekari 96 zilizopandwa mazao ya aina mbalimbali na kuboresha miundombinu katika kikosi hicho.
Pia, vijana hao wameweza kupanda ekari saba za miti, lengo ikiwa ni kutunza vyanzo vya maji katika kikosi hicho.
Meja Mbuge anatoa wito kwa jamii kuachana na tabia ya kubeza mafunzo ya JKT na kinachotakiwa ni kujiunga nayo, ili jamii inufaike.










