Kauli za wadau kuhusu ofisi mpya za TBS

01Mar 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Kauli za wadau kuhusu ofisi mpya za TBS

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linakusudia kufungua ofisi zake sehemu mbalimbali mikoani, kwa lengo la kudhibiti uingizaji wa bidhaa hafifu nchini unaofanywa na wajanja wachache. Wadau wanasemaje kuhusu hatua hiyo?

Herry John ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Kilimanjaro Creameries.
Hatua zinazochukuliwa na Shirika la Viwango Tanzania za kufungua ofisi zake kila mkoa nchini, sisi kama wamiliki wa kampuni ya Kilimanjaro Creameries ya Sanya Juu Moshi mkoani Kilimanjaro, tunaziunga mkono, kwa sababu lengo ni kutaka kuwadhibiti wafanyabiashara wenzetu wanaoingiza nchini bidhaa zisizo na ubora na itasaidia kuhakikisha soko la bidhaa zetu.

Kwani hao ndio wamekuwa wakituharibia soko, kwa sababu wanauza bidhaa kwa bei nafuu na kutufanya tukose wateja, huku wakiuzia watu vitu ambavyo havifai kuingia sokoni na ndio maana wamekuwa wakiviingiza nchini kwa njia za panya.

Kampuni yetu inatambua umuhimu wa ubora wa bidhaa na ndio maana hivi karibuni TBS ilitutunukia vyetu vya ubora kwa kutambua kile tunachokizalisha kuwa kinafaa kwa walaji.

Kwa maana hiyo, tunapoona shirika hilo likipanga mikakati ya kukabiliana na bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu, hatuna budi kuliunga mkono kwa sababu lina lengo la kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama, pia kulinda soko la bidhaa zetu sisi ambao hatujihusishi na uzalishaji wa vitu visivyofaa.

Labda na mimi nitoe wito kwa wafanyabiashara wenzangu wanaozalisha bidhaa halisi, kuunga mkono kile ambacho TBS inakifanya kwa ajili ya Watanzania wote, wakiwamo walaji na wafanyabiashara wadogo na wenye viwanda vikubwa, ili kuhakikisha kwamba Tanzania bila bidhaa hafifu inawezekana.

Tukiiachia TBS pekee, hali itaendelea kuwa mbaya kadri siku zinavyokwenda.

Roida Andusamile (Ofisa Uhusiano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
Ni kweli licha ya jitihada zinazofanywa na TBS za kukomesha uingizwaji wa bidhaa hafifu nchini, bado kuna changamoto ya kuendelea kuwapo bidhaa hizo zinazoingizwa nchini na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwa kutumia njia zisizo halali.

Mwaka huu 2016 shirika limejipanga kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati mbalimbali, ikiwamo ya kufungua ofisi kwenye mipaka ya Kasumulo, Tunduma na Bandari ya Mwanza.

Hiyo ni mbali na ofisi za mipakani zilizofunguliwa awali za Namanga, Holili, Horohoro, Sirari, Bandari ya Tanga, Mutukula na Rusumo. Tunatarajia kufungua ofisi za kanda katika mikoa ya Mbeya, Arusha na Mwanza.

Tutafanya hivyo, ili kusogeza huduma karibu na wazalishaji na wafanyabiashara na katika mikakati hiyo, tutakuwa tunafanya ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje kupitia bandari ya Dar es Salaam na ofisi za mipakani, zitakuwa wazi kwa saa 24 na kufanya ukaguzi sokoni mara kwa mara.
Hivyo, tuna uhakika kwamba tutapunguza kasi ya uingizwaji wa bidhaa hizo kama sio kumaliza tatizo kabisa, kwa maana hiyo wale wote wanaouza bidhaa hafifu waziondoe mara moja sokoni, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kuteketeza au kuwaamuru wazirudishe walikozitoa.

Pia wazalishaji wa nchini, wahakikishe wakati wote wanazalisha bidhaa zenye ubora unaostahili, wananchi nao watoe taarifa mara moja wanapobaini uwapo wa bidhaa hafifu sokoni.

Lutgard Kagaruki (Murugenzi wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania)

Mimi kwa maoni yangu ni kwamba, hilo suala la kufungua ofisi kila kona ya nchi, bali ni kufanya kazi kikamilifu kwa kuwa na wakaguzi wake watakaokuwa na jukumu la kuzunguka maeneo yote nchini kukagua bidhaa zinazoingizwa, ili kubaini kama zina ubora au la.

Tatizo la bidhaa hafifu kwa kweli ni kubwa na limeonekana kuwa sugu, hivyo TBS hawana budi kuangalia uwezekano wa kuwa na wakaguzi wao badala ya kutumia polisi kukabiliana na wale wanaoingiza bidhaa hafifu. Mbali na hilo, wananchi wapewe elimu ya kutambua bidhaa hizo ili nao waweze kutoa ushirikiano pale wanapogundua kuna bidhaa za aina hiyo kwenye maeneo yao.

Nirudie tena kusema kuwa wakaguzi, ni watu muhimu sana katika vita hii na pia ikibidi hata kama wamo wafanyakazi wa TBS wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ili kuingiza bidhaa hizo nchini wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Nasema hivyo, kwa sababu kwenye msafara wa mamba, kenge nao wamo. Inawezekana wakawamo baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu, ambao wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara kuingiza bidhaa hafifu.

Binafsi naweza kusema kuwa, kufungua ofisi kila kona ya nchi, inaweza isiwe suluhisho la tatizo hili iwapo shirika halitakuwa na wakaguzi wake, pia kama wananchi hawataelimisha jinsi ya kutambua bidhaa hizo.

Charles Hamkah (Mkurugenzi wa kampuni ya CXC Africa)

Utaratibu huo ni mzuri, lakini utakuwa mzuri na wenye mafanikio makubwa, iwapo utashirikisha wananchi ambao ndio watumiaji wakubwa wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa kutoka nje.

Ushirikishwaji ninaoueleza ni ule wa kupewa elimu ya kutambua bidhaa zisizo na ubora, ili pale wanapoiona waweze kutoa taarifa kwa mamlaka husika, ili hatua za kuwakamata wahusika zichukuliwe haraka.

Ninaamini hatua hiyo itasaidia kukabiliana na uingizwaji bidhaa hizo nchini, ambao umekuwa ukiibuka kama uyoga, licha ya shirika hilo kufanya jitihada za kila aina ili kukomesha kuwapo kwa bidhaa hafifu nchini.

Hivyo, TBS inapokuja na mkakati wa kufungua ofisi kila mkoa, ikumbuke kwamba elimu ni muhimu kwa wananchi wa maeneo husika, ili wasaidie katika vita hiyo.

Vinginevyo, Tanzania itaendelea kuwa jalala la bidhaa hatari kwa afya zetu, kwani kuna watu ambao ni kama wameweka pamba masikioni, hawasikii licha bidhaa zao ambazo hazifai kuteketezwa, bado wanaendelea kuingiza nyingine kila uchao.

Hapa inaonyesha kuna tatizo sehemu fulani ambalo halijapatiwa ufumbuzi. Mojawapo ni la wananchi kutokuwa na elimu ya kutambua bidhaa halisi na zisizo na ubora, hivyo siyo rahisi kwao kutoa taarifa kwa kitu ambacho hawana uhakika iwe kinafaa au hakifai.

Arafa Said (Mkazi wa jijini Dar es Salaam)

Binafsi huwa inaniuma sana, ninapoona mambo mengi nchini yakiwa yanaenda kienyeji sana, kama vile hakuna mamlaka zinazotakiwa kusimamia mambo yanyooke. Kikubwa ninachodhani kinachosababisha mambo kwenda ovyo, ni kukosekana ushirikiano miongoni mwa wizara na taasisi zake.

Kwa mfano, TBS iko chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, lakini katika jukumu hili la kudhibiti uingizaji bidhaa hafifu siyo ya wizara hiyo na taasisi yake, bali kuna wizara nyingine na taasisi zake nazo zinahusika kuhakikisha vita hivyo vinakuwa na mafanikio.

Hivyo, maoni yangu ni kwamba
wadau wote waungane na TBS inapofungua ofisi zake kila mkoa kufanikisha kile ilichokusudia kukifanya kwa ajili ya usalama wa Watanzania.

Kinachotakiwa kila upande unaohusika kusimamia kikamilifu na kuhakikisha hakuna mtu anayeingiza bidhaa zilizopigwa marufuku nchini.

Imekuwa kawaida kusikia TBS inafanya msako, lakini cha ajabu ni kwamba zinaendelea kuingizwa kama kawaida. Hiyo ni dalili kwamba kuna haja ya wadau wote kuungana na shirika hilo linapofungua ofisi zake kila mkoa nchini, kwa lengo la kukabiliana na uingizwaji bidhaa kwa njia za magendo, ambazo ni maarufu kama njia za panya.