Janet Magufuli: Shule ya Mbuyuni imebeba historia yangu.

01Mar 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Janet Magufuli: Shule ya Mbuyuni imebeba historia yangu.

ILIKUWA ziara ia aina yake. Mke wa Rais Dk. John Magufuli, mwalimu Janet Magufuli, aliporudi kwa mara ya tatukatika Shule ya Msingi Mbuyuni, iliyoko eneo la Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Mwalimu Janet Magufuli

Inaelezwa kwamba ni mara ya tatu kwa tafsiri alishawahi kusoma, kufundisha na safari hii alikuwa mgeni rasmi.
Katika safari yake hiyo, usoni alionyesha wazi kwamba anahuzunika kuiacha sehemu ambayo ana uhusiano nayo wa ‘chanda na pete’ na sasa anafika kuaga, kwa maana anaondoka mahali hapo.

Mwalimu Janet aliyekuwa amezoea maisha ya kawaida shuleni, kuchanganyika katika maisha ya kawaida na kula mihogo ya kukaanga na walimu wenzake ofisini, safari hii si yule tena waliyemzoea… ni mtu wa heshima.
Alifika hapo akiwa katika msafara wa magari, akiwa chini ya ulinzi wa hali ya juu na hadhi zote za ‘first lady.’

Shule ya Msingi Mbuyuni iliyopo umbali wa wastani wa kilomitatano kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam, imekuwa shule ya kipekee na kupata umaarufu,ambayo ndiko alikotokea mke wa rais aliyemtangulia,Mama Salma Kikwete, ambaye naye alilazimika kuuacha ualimu baada ya mumewe Jakaya Kikwete, kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, mwaka 1995.

Mara baada ya kufika shuleni hapo na kuolewa fursa ya kuzungumza anatamka huku akitokwa na machozi: “Inaniwia vigumu kuwaaga, kwani kwa sasa nitakuwa na majukumu zaidi katika kumsaidia mume wangu, Rais John Pombe Magufuli katika shughuli zake za kuwatumikia Watanzania.”

Alipokuwa shuleni hapo ambako kuna wanafunzi 1,000 kati yao 51 ni wanafunzi wenye ulemavu na walimu ni 31.

Mara zote akiwa shuleni hapo katika hali inayoonyesha kumzoea mgeni huyo, wanafunzi na walimu walionyesha kujiamini na kutokuwa na hofu juu ya ujio wake kama kiongozi mwandamizi wa kiataifa.

Tofauti kama ilivyozoeleka awapo “first lady” mahali fulani watu wengi huwa na shauku kubwa ya kumuona, huku wengine wakisukumana kumuona.

Wanafunzi nao walionyesha haiba pekee ya kufahamu vilivyo mwalimu wao huku baadhi ya walikuwa wakimtafisri katika kauli; ”Tulikuwa tunakunywa naye chai ya saa nne
pamoja na kitafunio cha aina yoyote hata mihogo.”

MBUYUNI KWA MARA YA PILI

Mama Janet kabla ya kusoma risala yake, aliomba kufanyika kitendo kilichozoeleka shuleni aliomba hadhira yote kusimama na kusali sala iliyozoeleka na kufahamika kwa walimu na wanafunzi wote.

Wanafunzi, walimu na wageni wengine walisimama kusali pamoja, huku kukiwapo wa mvuto wa pekee kwamba ni sala inayofahamika vyema shuleni Mbuyuni, wanafunzi wote wakiwamo wadogo wa darasa la kwanza, waliimudu vyema.

Anasema, amekuwa shuleni hapo kwa kipindi cha miaka 17, Mama Janet hadi mwaka jana, taratibu za itifaki zilimfanya aondoke mwaka jana, mumewe alipochaguliwa kuwa Rais.

Licha ya kulazimika kuachana na chaki, Mama Janet anasema: “Mimi bado ni mwalimu wa shule hii na tuliishi kwa upendo kama familia moja na ni mkazi wa Mbuyuni, nimesoma hapa miaka hiyo, hivyo mimi ni wa hapa hapa.”

MBUYUNI KWA MARAYA KWANZA

Kwa mara ya kwanza, Mama Janet alifika shuleni Mbuyuni akiwa mwanafunzi, wakati huo alikuwa anaishi katika nyumba za Polisi Oysterbay, umbali mfupi kutoka shuleni hapo.

Anasema walifikishwa mahali hapo na baba yake anayemtajakuwa Mzee Mbizo, kwa ajili ya kuandikishwa. Alikuwa na mdogo wake na baba yao alikuwa na mzoea ya kuwapeleka shuleni kila siku.

“Nakumbuka baba yangu Mzee Mbizo alinileta hapa kuniandikisha na Mwalimu Mkuu wakati huo alikuwa Mama Khatibu aliniandikisha. Nilihitimu na nilirudi tena shuleni hapa mwaka 1997 kama mwalimu. Hata watoto wangu wote wamesoma na kuhitimu hapa hapa Mbuyuni,’’anasema Mama Janet.

Anasema kutokana na mazingira hayo, anaiona Shule ya Msingi Mbuyuni kuwa na historia kubwa katika maisha yake.

AWAASA WAZAZI

Mama Janet anatoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuacha kubweteka na mazoea ya kuiachia serikali kutekeleza majukumu yote, mara baada ya kuambiwa kuna elimu ni bure.

Anafafanua kuwa majukumu ya wazazi na walezi, ni kuhakikisha watoto wana na sare za shule, pia wafuatilie maendeleo ya masomo yao na kuwapatia mahitaji muhimu kama vile chakula.

“Hakuna haja ya kubwetekana kuiachia serikali, licha ya kusema elimu ni bure. Kuna baadhi ya majukumu ni yetu wazazi na walezi kama chakula, sare za shule, kufuatilia maendeleo yao, kwani majukumu hayo ni mahitaji muhimu na hayakwepeki,” anasema Mama Janet.

Pia anaelekeza kauli kwa wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo na kuacha mambo ambayo hayana msingi kwa wakati wao kwa sasa.

WALIMU NA WANAFUNZI

Josca Kamazima mwalimu aliyepo shuleni hapo tangu mwaka 1989, anamuelezea Mama Janet kama ni mwalimu aliyekuwa na juhudi shuleni hapo, ambaye alishirikiana na walimu wenzake katika kutekeleza majukumu yao.

“Tuliishi kwa upendo, amani na anapenda kusaidia watoto.Alimpatia baiskeli maalum mtoto ambaye ni mlemavu, Elisha, hivyo ni mtu mwema,” anasema mwalimu huyo.

Mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo, Mateo Mathias anamtaja mwalimu Janet aliwafundisha kwa umahirimkubwa na aliupenda ufundishaji wake.

“Nampenda MwalimuPombe (Janet Magufuli). Alitufundisha vizuri nakumbuka alinifundisha nikiwa darasa la tano mwaka jana masomo ya Historia, Stadi za Kazi, Haiba na Michezo pamoja na Tehama. Nilikuwa namuelewa vizuri, ni mwalimu mzuri,” anasema mwanafunzi Mathias.

AJIITA DADA MKUU

Mama Janet anasema yeye akiwa ni Dada Mkuu wa Shule ya Mbuyuni, atahakikisha changamoto mbalimbali za shuleni hapo na shule nyingine nchini zinatatuliwa, kwa kuwa anazifahamu vizuri.

Anasema yeye ni mwalimu na anazifahamu changamoto za kazi hiyo, akitaja baadhi ni maslahi madogo, ucheleweshaji wa malipo ya madai mbalimbali, ikiwamo walimu kupandishwa madaraja.

“Tuna majukumu makubwa na ualimu ni wito. Utakuta siku umefika shuleni, mtoto unamuona ana njaa, utoe fedha yako ale chakula au anaumwa akatibiwe kwa wakati huo kwa fedha zako. Sisi tuna majukumu makubwa na nitazifikisha changamoto zenu na za walimu nchi nzima kwa shemeji yenu,” anasema Mama Janet.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Doroth Malecela, naye katika risala yake hakusita kutaja changamoto zinazowakabili walimu shuleni, ikiwamo kutopatiwa fedha za likizo kwa wakati, mafao baada ya kustaafu, upungufu wa walimu na nyumba za walimu.

Doroth anataja changamoto nyingine ni madawati, matundu ya vyoo na anaiomba serikali kuwatatulia changamoto hizo.
Mama Janet alikabidhiwa zawadi ya saa ya ukutani, huku nayeakiwakabidhi baadhi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum vifaa vya shule.