Ila halikuwa jambo la ajabu kwani wapo viongozi wa kisiasa na wasomi wanaofahamika vyema walioondoka duniani wakiwa vijana hata zaidi, iwe ni kwa ajali au ni maradhi yaliyowashambulia ghafla. Ni vihatarishi vya kibinadamu ambavyo kimsingi havizuiliki, na ndiyo mustakabali mzima wa masuala ya imani.
Maisha ya Membe katika siasa hayakuwa na 'mikiki wala makeke,' wengi wakimwona kama mpendwa wa mfumo wa siasa wakati wa awamu ya nne, kama wanadiplomasia watangulizi awamu zilikuwa enzi za Ali Hassan Mwinyi na Baba wa Taifa Julius Nyerere.
Mwalimu Nyerere alitaka nafasi yake itwaliwe na mwanadiplomasia Salim Ahmed Salim, lakini akakwamishwa na Kamati ya CCM, lakini akafaulu awamu iliyofuata, akawezesha kuchaguliwa kwa Benjamin Mkapa na Waziri wa Mambo ya Nje mwenye kuheshimika.
Aliyekuwa mwanadiplomasia nguli wa awamu ya tatu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete, akawa ndiye mteule wa CCM, naye akataka iwe vivyo hivyo kwa Membe.
Licha ya kuwa viongozi wakuu wa nchi siyo lazima watoke miongoni mwa wanaoongoza Wizara ya Mambo ya Nje, kuna jambo ambalo wanadiplomasia wanaongeza katika uongozi, yaani umuhimu wa kusikiliza na kujali kila sauti inayoongea. Katika diplomasia kila siku unatafutwa muafaka, maelewano yenye tija kwa kiasi fulani kinachokubalika kwa pande zinahusika. Mwanadiplomasia lazima awe mvumilivu, msikivu na pia mnyenyekevu, anayeepusha shari hata wakitofautiana.
Wanaomfahamu kwa karibu wanasema hizo ndizo zilikuwa sifa za hayati Membe, na kwa maana hiyo raisi wa awamu ya nne unaweza kusema aliitakia mema nchi kuwa na kiongozi msikivu kama yeye alivyokuwa, kwamba hataingia katika kishawishi cha udikteta wala kuwaburuza Watanzania.
Hata Mwalimu Julius Nyerere alikiri mara kwa mara kuwa mfumo wa katiba unamruhusu rais kuwa dikteta akitaka, hivyo kuwa msikivu na mpole au kutoonea watu ni tunu ya mtu binafsi katika mfumo huu, kuwa si kukosa madaraka ila kutoyatumia vibaya. Ulazima wa madaraka hayo ni suala jingine, na unaweza kusema hata wanaotaka kuyaondoa wanajua umuhimu wake.
Kimsingi mwanadiplomasia huyo aliona kuna nafasi ya yeye kuwa kiongozi mkuu wa nchi, na kwa vile ilikuwa dhahiri anaungwa mkono katika ngazi za juu sana, yeye mwenyewe na watu wake wa karibu wangeamini hilo linatosha kumpa nafasi hiyo ya kuongoza taifa.
Tatizo ni kuwa kutangaza nia hakutokei hivi hivi ila katika mazingira mahsusi ya kisiasa, ambako wafuasi wa vyama huangaliana wao kwa wao kujua nani anaweza kukubalika kwa upana zaidi.
Kwa kuinuliwa ndani ya CCM kama mgombea mtarajiwa halafu ACT-Wazalendo, kukubalika kwa Membe kulidhihirika kama ilivyokuwa kwa hayati Augustine Mrema au Edward Lowassa, ila mazingira ya kampeni yake mwaka 2020 yalikuwa ya kushtukiza na yalishangaza pia.
Uwepo wa Membe katika uwanja wa siasa, kama ilivyo hivi sasa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ni kielelezo kimojawapo cha uwazi wa mfumo wa sasa wa siasa, na kuwa kama una mtaji wa kukubalika unaweza kugombea popote. Ila tofauti na wapinzani wa mfumo huo wanavyosema, nguvu zote haziko tu katika mikono ya rais kwani naye pia anategemea uongozi wa pamoja, kwa kujali wananchi wanataka nini.
Ndiyo maana baadhi yawapinzani walioandika kitabu hivi karibuni (Rais aliyenong'oneza Mimi Ndiye Dola kutoka Chato) hawakuliona hilo. Alitumia nguvu ya umma, watu wakawa nyuma yake, alipoanza kutumbia majipu na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali sasa zinaonyesha kuwa majipu yamerudi.
Kama ambavyo wachambuzi tofauti wamemtaja, Membe alipata ubunge katika eneo lake la kuzaliwa la Mtama hasa kutokana na kukubalika serikalini, hakuwahi kutajwa kuwa na sifa ya mtu aliyevuna mapesa huku na kule kwa njia yoyote ile, iwe ni biashara au miradi serikalini.
Kwa vile alikuwa waziri kwa muda mrefu miaka tisa haielekei kuwa alikuwa na uhabawa fedha, ila hakuwahi kuwa na sifa ya utajiri kama wenzie kadhaa.
Ambacho hatuwezi kujua, na hasa baada ya kuondoka waziri huyo wa siku nyingi, ni tofauti ambayo ingekuwepo endapo Membe angepita kama mgombea wa CCM, ukiuliza swali hilo ni wazi utavuna makundi mawili ya majibu, na hapa hakuna cha upinzani na CCM ila kuchukulia poa na mabadilikoo ya kina. Wanaomfahamu Membe, na hasa ukaribu wake na uongozi wa awamu ya nne, wangetazamia kiongozi mpole, mwanademokrasia ambaye Baba wa Taifa angesema 'wala rushwa hawatamwogopa.' Ndiyo hapo kuna kujikanganya katika lugha rasmi hasa miongoni mwa makundi huria yasiyo ya kiserikali na mtazamo wa kina miongoni mwa jamii.
Mtawala anayependwa na makundi ya kiraia na sehemu kubwa ya watawala serikalini ni yule asiyeogopwa na walarushwa, ila wananchi wanamtaka huyo ambaye watamwogopa, ajikusanyie madaraka ayatumie kuwanyoosha watawala, alete maendeleo.
KUGOMBEA MARA 2
Ina maana kuwa Membe aligombea mara mbili na vipindi vyote viwili ila wakati haukuwa wake, kwani mwaka 2015 hisia za kisiasa zilikuwa za kuhitajika mabadiliko na siyo mwendelezo wa moja wa moja wa awamu ya nne, aliokuwa akisimamia Membe.
Licha ya kugombea 2015 akiwa nafasi yatano bora , alishindwa na nafasi ya mgombea uchaguzi kupewa JPM, hata hivyo mwaka 2020 aligombea kupitia ACT –Wazalendo.
Inaelekea kufika mwaka 2020 kwanza hakuwa na msingi au mtaji wa kutosha kumyumbisha JPM na kwa hali yoyote ile mabadiliko ambayo punde yalitazamiwa kuja ilikuwa ni mabadliko ya dira ya uchumi na ushirikiano na nchi nyingine kukuza uchumi, siyo kurudi tulipokuwa mwaka 2015
Buriani Komredi Membe, ulisimamia taswira iliyofifia, pengine ya kutobadilika kisera maana watu walitaka mabadaliko pengine ingekuwa ni kuendeleza furaha iliyokuwepo mwaka 2015 ambayo ni uwazi wa serikali , uelewano bungeni, uhuru wa kutoa maoni na kukosoa. Hakuna majibu rahisi kwa hilo iwapo angekuwa Rais Bora wa Tanzania, ila cha muhimu ni Membe alikuwa kiongozi mwenye utulivu, mwenye kupenda uelewano na mwanadiplomasia wa kimataifa.










