Jambo kubwa ni kushinikiza Spika Dk. Tulia Ackson, kuwaondoa wabunge hao ambao wameshafukuzwa uanachama CHADEMA na kupoteza sifa ya kuwa wabunge.
Hata hivyo, maandamano hayo yaliyoishia viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, yaliwakera wana CCM na Jumuiya ya Wanawake (UWT), ikiwakosoa hasa ujumbe ulioandikwa na BAWACHA kwenye mabango yao.Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, anasema baadhi ya kauli na mabango yenye ujumbe uliomhusisha Rais Samia Suluhu Hassan, hazikuwa za kiungwana hivyo anajitokeza kuwakemea.
"Siko hapa kupinga maandamano hayo lakini kutoa masikitiko ya UWT na wanawake wengine kutokana na baadhi ya kauli na mabango yenye ujumbe uliomuhusisha moja kwa moja Rais Samia,"anasema Mary, jijini Dodoma, wiki iliyopita.
Analitaja bango lilikuwa na ujumbe: “Samia tulikukaribisha Moshi kwa heshima, wewe umetulipa dharau, akisema mambo hayo UWT haiwezi kuyavumilia na kuongeza:" BAWACHA ndiyo waliomuomba Rais kuwa mgeni rasmi, katika maadhimisho ya kilele cha siku ya Wanawake Duniani Machi 8 mwaka huu, ndio waliomhitaji, kuliko yeye alivyowahitaji."
Anaendelea kumpongeza Rais kwa kukubali mwaliko wa BAWACHA, na kwamba kupitia utayari wake huo, dunia ilishuhudia uungwana wake, akifafanua kuwa mara nyingi ni vigumu kiongozi wa juu wa serikali wa chama kinachotawala kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi kutoka chama cha upinzani.
"Lakini Rais wetu ni mwanamke shupavu, msikivu na mkarimu ndiyo maana alikubali mwaliko huo, kuonyesha kwa vitendo kuwa amedhamiria kuliunganisha taifa bila kujali tofauti za kiitikadi,"anasema.Anafafanua kuwa BAWACHA inapaswa kuendelea kuheshimu na kuenzi uamuzi wa Rais Samia kukubali mwaliko na kujumuika nao jambo ambalo pia liliyapa heshima na hadhi kubwa maadhimisho hayo kuliko wakati wowote waliowahi kuandaa maadhimisho ya aina hiyo.
UWT inaheshimu maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa mpaka sasa, uhuru wa kuendesha shughuli mbalimbali za kisiasa na uhuru wa kujieleza ambao unalindwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata ukosoaji kwa serikali yetu," anasema.
HOJA YA BAWACHA Anafafanua kuwa katika mkutano wao, BAWACHA waliwasilisha jambo lao kwa Rais la kutaka wabunge wao waondolewe bungeni, akawaeleza wazi kuwa lipo mahakamani, hivyo wasubiri uamuzi wa mahakama.
Mary anasema kitendo hicho hakiendani na heshima aliyowapa ya kukubali mwaliko wao mila na desturi za Watanzania za kuheshimu viongozi wao na hata wale waliotuzidi kiumri.
Anasongeza kuwa baada ya CHADEMA kumaliza mkutano wao, UWT nao waliandaa mkutano mkubwa wa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam wa kumpongeza Rais Samia kwa kutimiza miaka miwili madarakani uliohudhuriwa na wanawake kutoka sehemu mbalimbali."Maelezo yaliyotolewa na Catherine Ruge, Katibu wa BAWACHA alipoulizwa kuhusu tafsiri ya maneno “Samia tulikukaribisha Moshi kwa heshima wewe umetulipa dharau hayana mashiko,"anasema akimkosoa Catherine.
Katika ufafanuzi wake anasema madai kwamba Rais ndiye mwajiri, akiacha kuwalipa wabunge hao hawatakuwapo bungeni, si sahihi, kwa kuwa Sheria ya Fedha mwaka 2001 iko wazi na kifungu 6 (7), kinaeleza kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ndiye mlipaji mkuu wa serikali na pia mwajiri wa wabunge wakiwamo wa viti maalum wanaopatikana kwa mujibu wa ibara 66(b) sio Rais, anasema.
Aidha, anawataka viongozi wa BAWACHA na wanachama wao kurejea ibara 107A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosema; “Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa idara ya mahakama na idara ya mahakama ya Zanzibar, hivyo hakuna chombo cha serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki," anasema.
Anasema, BAWACHA kundelea kufanya maandamano na kutoa kauli za kebehi kwa Rais na Spika haitawasaidia, na kwamba waichie mahakama ikamilishe kazi na kutoa uamuzi juu ya maombi ya wabunge wao 19.
"Wametumia haki kikatiba kwenda mahakamani kupinga kufukuzwa uanachama, kwa kufanya hivyo watakuwa wanaheshimu mhimili wa mahakama, hivyo ni muhimu kwa chama kinachojinasibu kuwa kina nguvu na kipo tayari kushika dola kuheshimu mahakama," anasema.










