Uchunguzi wa Nipashe uliofanywa katika Jiji la Dar es Salaam umebaini kuwa tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipotokea mwaka 2019, kuna baadhi ya wafanyabiashara jijini Dar es Salaam waliokuwa na kipato kikubwa cha maisha wamerudi katika hali ya umasikini.
Pia, limebaini kuna baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakimiliki maduka mawili hadi matatu lakini kwa sasa wanamiliki duka moja, huku wengine wakibadili aina ya biashara na kujishughulisha na ujasiriamali.
WAFANYABIASHARA WAELEZA
Isaak Barnabas aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa wa kuuza nguo za watoto katika mtaa wa Kongo anasema ugonjwa wa corona umempa hasara ambayo hatakuja kuisahau.
“Hali haikuwa nzuri kwa kweli, mambo yalivurugika, tulikuwa hatujui tushike lipi tuache lipi, kila kitu kilikuwa shaghalabaghala. Wateja hawakwepo wala bidhaa hazinunuliki” anasema Isaak.
Anasema alipata hasara ya Sh. milioni 14 baada ya mzigo alioagiza China kukwama kufika Tanzania, kwamba hata nguo alizokuwa nazo akiuza zilikuwa haziuziki.
“Nakumbuka niliagiza balo 10, kila moja likiwa thamani ya Sh. milioni 1.4, ghafla nikasikia kwenye taarifa ya habari kwamba kuna ugonjwa umeingia China unaitwa corona na umesababisha meli na ndege zisitoke nchini humo, kwa kweli niliishiwa nguvu, nikikumbuka nalia sana, hadi leo sijapata mizigo yangu,”alisema.
Anasema wakati huo alikuwa anategemea mzigo huo akiuza alipie kodi ya pango la biashara Sh. milioni tisa kwa muda wa miezi sita, hivyo alikwama na kuamua kufunga biashara na kurudi nyumbani.
Rahabu Mbinga muuza duka la jumla la vitenge katika Soko la Kariakoo analieleza Nipashe kwamba mwaka 2019 wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa corona biashara yake ilikwama.
Anasema alishindwa kuuza bidhaa zake kutokana na wateja kuogopa kufika Kariakoo kutokana hofu ya kuambukizwa ugonjwa huo, kwamba alikaa na mzigo kwa muda mrefu pasipo kuuzwa.
Anasema kabla ya mlipuko wa ugonjwa huo mauzo ya siku yalikuwa ni Sh. milioni tano lakini yalishuka hadi Sh. 400,000.
“Yaani acha tu, Mungu ni mkubwa kwa kweli, ametusaidia, hali haikuwa nzuri, tumepitia magumu sana, dunuI nzima ilikuwa katika wakati mgumu,” alisema.
Filipo Mallya aliyekuwa muuzaji wa vifaa vya simu za mkononi eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam kwa sasa ni baba wa nyumbani anaeleza kuwa aliagiza boksi 15 za vifaa mbalimbali vya simu kutoka China lakini ulikwama na hakuweza kuupata.
“Niliweka mtaji wangu wote huko, niliagiza mzigo wa Sh. milioni 20 kwa sababu awali niliagiza mzigo wa Sh. milioni 7 nikapata faida ya Sh. milioni 13, hivyo nikaagiza mzigo mkubwa zaidi lakini nilichoambulia Mungu ndiye anajua, kwa sasa niko tu nyumbani,” anasema.
Baadhi ya wafanyabiashara, hasa kinamama na wasichana kwenye maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam yakiwamo Tegeta, Wazo Hill, Kunduchi na Ununio walilieleza Nipashe juu ya yale waliyoyaona kwenye kipindi hicho.
Zainabu Almasi (58), mkazi wa Wazo Hill anayeuza chakula Tegeta Sokoni, alisema kwa kuwa corona ilikuja bila taarifa, yeye na wenzake hawakuwa wamejiandaa.
Hatua hiyo, anasema ilisababisha kula hata mtaji wake wa kununulia chakula kwa ajili ya biashara kwa maana ya mchele, unga, sukari, mafuta ya kupikia na viungo.
Khadija Ulanga, ambaye ni mama lishe, naye alikiri kuwa corona ilisababisha kuishiwa fedha kwa sababu wateja wake wengi walipotea na wengine akikutana nao walimuambia “janga hili linapenda mtu aache tabia ya kulakula kila wakati".
Tutindaga Mwakipesile (38) anayeishi Boko ambaye hufanya kazi ya kuuza vyakula na kupamba wakati wa sherehe na misiba, alisema biashara hiyo iliporomoka katika kipindi cha janga la corona.
"Huwezi kuamini nilikuwa na wasichana tisa nafanya nao hizo kazi ilibidi kuwaachisha kazi kwa sababu tulikuwa hatupati tenda tena kwa kuwa shughuli hizo zilisitishwa rasmi na serikali kuzuia mikusanyiko ya watu", alisema.
SERIKALI YAELEZA
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, anakiri ugonjwa wa vizuri vya corona ulileta athari katika sekta ya biashara, uwekezaji na viwanda.
Anasema mwaka 2022 thamani ya mauzo ya bidhaa kwenda Soko la Ulaya ilipungua hadi Dola za Marekani milioni 955.6 kutoka Dola za Marekani milioni 1,346.1 mwaka 2021, sawa na upungufu wa asilimia 29.1.
Anabainisha kwamba kupungua huko kulisababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa corona.
CHAMA CHA W/BIASHARA
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA), Nebart Mwapwele, anasema biashara nyingi ziliathirika wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo.
Anasema kulikuwa na hofu hali iliyosababisha biashara ndogo na kubwa kudorora, kampuni zilipunguza wafanyakazi ili zijinusuru na hali mbaya ya kiuchumi.
Anasema nchi nyingi zilifunga mipaka hali iliyosababisha wafanyabiashara wa Tanzania kushindwa kwenda kuuza bidhaa zao na kushindwa kupata wateja.
Viwanda vya ujenzi vilisimamisha uzalishaji kutokana na kukosa malighafi ya uendeshaji walizokuwa wanaagiza kutoka nje za nje.
“Kwenye viwanda viliathirika kwa kukosa masoko, masoko makubwa ya nchi jirani walikuwa wamefunga mipaka. Viwanda vingi vilipunguza uzalishaji kwa kukosa malighafi na vilijiendesha kwa hasara,” alisema.
JUMUIYA YA W/BIASHARA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Abdallah Libembe, anasema mlipuko wa ugonjwa wa corona uliwaacha asilimia 20 ya wafanyabiashara masikini.
Anasema wafabyabiashara waliokuwa waagiza bidhaa kutoka nje waliathirika sana kwa sababu viwanda vingi vilifungwa, pamoja na nchi nyingi kuweka masharti magumu kwa wageni kuingia.
“Kama unakumbuka kuna baadhi ya nchi waliweka utaratibu kwa mgeni lazima ukae karantine siku 14 hadi 21 ndipo uingie nchini mwao, kutokana na usumbufu wafanyabiashara wengi wa Tanzania waliacha kusafiri,” alisema.
Alisema corona iliathiri mzungumko wa fedha nchini, pia hata wafanyabiashara wakubwa wa maduka hawakupata wateja wengi kwa sababu ya mlipuko huo, mfano Kariakoo.
“Wafanyabiashara 295 wakubwa na wadogo walilazimika kusitisha kufanya shughuli zao kutokana na hasara waliyoipata kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona,” anasema
Alisema idadi kubwa ya wafanyabiashara walifunga biashara zao kwa sababu walikuwa wanaogopa kusafiri kwenda kuchukua bidhaa nje ya nchi, hata walioagiza hawakupata mizigo yao.
HATUA ZA BENKI KUU
Kamati ya Sera na Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyokutana Mei, 2020 ilipitisha hatua mbalimbali za kisera zilizolenga kukabiliana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa corona katika uchumi kwa wakati huo.
Mojawapo ni kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa BoT kutoka asilimia saba hadi sita.
Pili, BoT ilishusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa BoT kutoka asilimia saba hadi tano kuanzia Mei 12, 2020 hatua iliyoongeza wigo wa benki kukupa kutoka BoT kwa riba nafuu, kupunga riba ya mikopo kwa wateja.
Tatu, BoT iliongeza unafuu kwenye dhamana na hati fungani za kiserikali zinazotumika na benki kama dhamana wakati wa kukopa kutoka BoT.
Nyingine ni benki na taasisi za fedha kutathmini kwa kina athari zinazotokana na ugonjwa wa virusi vya corona kwenye urejeshaji wa mikopo, kujadiliana na wakopaji namna ya kurejesha mikopo na kutoa unafuu wa urejeshaji wa mikopo inavyoonekana inafaa.
Tano, ni kampuni zinazotoa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka Sh. milioni tatu hadi milioni tano na kiwango cha akiba kwa siku kwa mteja kutoka Sh.milioni tano hadi Sh. milioni 10.
Sita, BoT iliendelea kufanya tathmini ya athari ya ugonjwa wa virusi vya corona katika sekta mbalimbali za uchumi na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza madhara ya athari hizo.
WACHUMI WASHAURI
Baadhi ya wataalamu wa uchumi wametoa ushauri kwa serikali na wafanyabiashara juu ya kuyakabiri majanga ya kidunia pindi yanapotokea ili kunusuru uchumi.
Benjamin Mwamsojo mtaalamu wa masuala ya uchumi anasema serikali inapaswa kuboresha sekta ya kilimo ili taifa liweze kuwa na malighafi ya kutosha kulisha viwanda na kuacha kutegemea kutoka nje.
Anasema pia serikali ijiwekeza katika kuboresha thamani ya shilingi ili iwe na thamani kubwa, sambamba na kuboresha sekta ya fedha.
Mtaalamu wa masuala ya fedha na uchumi, Dk. Steven Mloza anasema wafanyabiashara wanapaswa kuwekeza katika sekta ya mauzo ya moja kwa moja.
Anasema takwimu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinaonyesha uchumi wa ulimwengu ulipungua 4.4% mwaka 2020, lakini wakati huo huo, sekta ya mauzo ya moja kwa moja ilikua kwa takribani 2.3%.
Dk. Mloza anasema kwa sababu hiyo, sekta ya mauzo ya moja kwa moja ndio sekta pekee iliongeza biashara na nafasi za ajira kwa asilimia kubwa kuliko sekta zote katika kipindi chote cha maafa ya Uviko-19.










