Kilomita za mraba 10,017 za ziwa hilo ambalo limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo vitendo vya uvuvi haramu, ziko katika Mkoa wa Kagera.
Pamoja na athari nyingine, vitendo uvuvi haramu husababisha kuvuliwa kwa samaki wachanga, kuharibu mazalia ya samaki na kusababisha aina nyingi za samaki kutoweka.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la utafiti wa mazingira la (Accord-Tanzania), lenye makao makuu yake jijini Mwanza, kuna hatari ya kutoweka kwa aina zote za samaki katika Ziwa Victoria katika kipindi cha miaka 30 ijayo, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na vitendo vya uvuvi haramu.
Katika utafiti wa Accord, mwaka 2048 kutakuwepo na upungufu mkubwa wa samaki katika ziwa hilo, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo uvuvi haramu.
Utafiti wa Accord unafanana na wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO), uliofanyika mwaka 2005, ukiwa na kichwa cha habari ‘Hali ya raslimali za uvuvi za ziwa Victoria’ ambayo unaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, takriban aina 200 za samaki wametoweka.
Kwa mujibu wa utafiti huo, katika miaka ya 1920, Ziwa Victoria lilikuwa na takribani aina 400 za samaki, hata hivyo umebainisha kwamba hivi sasa kuna aina tatu pekee za samaki wanaovuliwa kibiashara ambao ni sangara, sato na dagaa.
Pamoja na tatifi kuonyesha samaki kupungua katika ziwa hilo, wavuvi wanaotegemea kupata kipato kutokana na shughuli za uvuvi, sasa wanakabiliwa na tatizo la kuvamiwa na wavuvi wanaotajwa kuwa ni kutoka nchini Uganda.
Wavuvi hao kutoka katika nchi hiyo jirani, wanadaiwa kuwateka nyara wavuvi wa Tanzania, kuwapiga na kuwajeruhi na kisha kuwanyang’anya mali zao ikiwamo samaki wanaokuwa tayari wamevuliwa.
Vitendo vya wavuvi wa Uganda kuingia katika eneo la Tanzania na kuendesha shughuli za uvuvi bila kuchukuliwa hatua, vinathibitishwa na wavuvi wanaotumia mwalo wa Malehe ulioko kijiji Kyamalange kata Rubafu Bukoba Vijijini, mkoani Kagera.
Mmoja wa wavuvi hao, Joseph Elias, anasema eneo hilo ni kama mpakani maana kuna mitumbwi inayoingia kutoka Uganda na kwamba kutokana na mwingiliano huo eneo hilo linahitaji uongozi na usimamizi thabiti muda wote.
Elias anasema vitendo vya kuvamiwa na kupigwa na wavuvi kutoka Uganda vimekithiri, lakini anaona pamoja na serikali kuwasaidia wavuvi wa eneo hilo kukabiliana na changamoto hiyo, kupigwa na kunyang’anywa mali zao, pia isimamie mapato yanayopotea kutokana na uvamizi huo.
“Hapa pia mapato yanapotea, maana Waganda wanavuna na kuondoka bila kutozwa kitu chochote, serikali ipo, lakini haichukui hatua, eneo hilo likisimamiwa vizuri hata uchumi wetu utaongezeka, majengo yataboreshwa na mji utakua haraka,” anasema Elias.
Anasema wavuvi kutoka nje wanapokamatwa wanawahonga maofisa wanaohusika na shughuli za uvuvi bila kuwashirikisha viongozi wa eneo hilo na kusababisha vitendo vya wavuvi hao kufika kila mara, wanavua na kuondoka bila kuguswa.
“Inavyofahamika mtu akikamatwa kinyume cha taratibu anapaswa kunyang’anywa mali anazokutwa nazo ndipo ataelewa kuwa alichokifanya ni haramu, lakini akikamatwa akatoa kitu kidogo na kuachiwa, siku nyingine atarudi kufanya kosa lile lile,” anasema.
Naye, Katibu Kiongozi wa mwalo huo, Shaffy Omary, anasema kuwa amekuwa akipokea malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wavuvi wao, kuwa wavuvi wa Uganda wanavua samaki katika eneo lao kinyume cha sheria.
Omary anasema kuwa wavuvi wa nchi hiyo wanapokamatwa wakatozwa faini wanalipiza visasi kwa wavuvi wa Tanzania kwa kuwasubiria majini na kuwakamata, kuwapiga na kisha kuwanyang’anya samaki.
“Wavuvi wetu wakilalamika kwa nini wanakamatwa na kupigwa, hujibiwa na wavuvi wa Uganda kuwa na wao huwa wanakamatwa kwa hiyo wanalipiza visasi,” anasema Omary.
Anatumia fursa hiyo kuiomba serikali kusimamia na kuhakikisha kamati ya usimamizi wa rasrimali za ziwa (BMU), inakuwApo na kuchagua viongozi imara, ili kwa kushirikiana na mamlaka zilizopo kudhibiti vitendo hivyo.
Anasema kuwa vitendo vya wavuvi kuvamiwa, kupigwa na kunyang’anywa mali zao mbali na kuwasababishia majeraha wavuvi, pia vinachangia kushusha uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Maana wavuvi wa Uganda wanavua na kunufaika sisi tunaangalia tu, lakini mvuvi wa Tanzania hawezi kwenda kuvua katika eneo la Uganda akaachwa bila kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kutozwa faini.” anasema.
Mkuu wa Kikosi cha Polisi Wanamaji wilayani hapa, SP. Msabila Bundala, anathibitisha kupokea taarifa kuhusu vitendo vya wavuvi kuvamiwa ziwani na kisha kuporwa mali zao. Kikosi hiki ndicho chenye jukumu kuangalia usalama wa wavuvi na mali zao.
“Ziwani kuna uharibifu wa aina mbalimbali, kuna wizi wa injini za boti, wizi wa nyavu, kuwanyang’anya wavuvi samaki wakiwa ziwani, kwa hiyo tunaendelea kushirikiana nao ili kukabiliana na changamoto hizi,” anasema Bundala.
Anasema amekuwa akiwaelimisha wavuvi umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwa kikosi hicho uvamizi unapotokea, ili ufanyike ufuatiliaji wa haraka utakaowezesha kuwanasa wahusika, lakini mara nyingi taarifa zimekuwa zikichelewa.
“Kipo kituo chetu pale Malehe, lakini pia tumekuwa tukifanya doria za mara kwa mara, ili kuhakikisha usalama unakuwapo ziwani, wanaokamatwa huchukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani,” anasema.
Anasema ili kukabiliana na vitendo hivyo ipasavyo, wanastahili kuwa na vitendea kazi vya kisasa zikiwamo boti na kuwa sasa zinafanyika jitihada za kuhakikisha wanapata vifaa.
Changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi, zinasababisha wadau mbalimbali wakiwamo maofisa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Idara ya Uvuvi na Kikosi cha Polisi Wanamaji, kuwatembelea wavuvi katika maeneo mbalimbali.
Pamoja na kutoa elimu kwa wavuvi namna ya kufanya uvuvi endelevu na kwa kufuata sheria na taratibu za nchi, ziara hiyo inalenga kuzichukua changamoto hizo na kuzipatia ufumbuzi, ili watu wanaotegemea ziwa hilo wafanye shughuli zao katika mazingira salama.
Japhet Loysimaye, ni Meneja wa Mafunzo ya Mabaharia kutoka Sumatra Makao Makuu, anasema wameamua kuendesha kutembelea na kuzungumza na wavuvi, ili kuendelea kuwaelimisha juu ya usafiri wa majini, lakini pia kujua changamoto zinazowakabili.
Loysimaye anasema wamebaini pia kuwa wavuvi wanalalamikia malipo ya leseni kufanywa kwa dola ya Marekani badala ya Shilingi ya Tanzania; na kufanya gharama kubadilika kila wakati kulingana na thamani ya dola wakati husika.
“Changamoto hii ilikwishapokelewa na inaendelea kufanyiwa kazi na mamlaka yetu hasa kwa wavuvi wenye vyombo vidogo ambavyo haviko katika itifaki ya kimataifa, maamuzi yatakayofikiwa wataelezwa,” anasema.
Anasema kuwaelimisha wavuvi ni jukumu endelevu na litafanyika nchi nzima kwenye maeneo yote yenye vyombo vya majini ikiwamo visiwani, huku akiendelea kuwahimiza wamiliki na watumiaji wote wa vyombo vya majini kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
“Kupakia abiria kuzidi uwezo wa chombo, kutoacha kumbukumbu za chombo kabla ya kuanza safari ikiwamo orodha ya majina ya abiria, kuchanganya mifugo na abiria, kuchanganya abiria na vitu vya milipuko, vyombo kutokuwa na vifaa vya kujiokolea ni kinyume cha sheria, na yeyote atakayekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria,” anasema.
Anasema isichotaka kusikia serikali ni watu kupoteza maisha ziwani kutokana na uzembe wa wamiliki au wanaohusika kuendesha na kusimamia vyombo hivyo, maana wengi wanaopotea ni vijana ambao bado wana nguvu za kuzalisha na kuinua uchumi wao na wa taifa.
Aidha, anawataka maofisa uvuvi kuhakikisha hakuna chombo chochote kinachoruhusiwa kuingia majini kama hakijapata leseni ya ubora kutoka kwa mamlaka hiyo.
Mbali na wavuvi wa mkoa wa Kagera kulitegemea ziwa hilo kwa kiwango kikubwa katika kujiingizia kipato, pia yapo maeneo mengine ya uvuvi ikiwamo ziwa Burigi, Ikimba, Rushwa na Rumanyika. Lakini pia ipo mito inayotumika kwa shughuli hizo ambayo ni Kagera, Ngono na Ruvuvu.










