Ulinzi Hifadhi ya Selous ulivyogeuka vita vya askari na wakazi jirani

24Mar 2016
Abdul Mitumba
Liwale
Nipashe
Ulinzi Hifadhi ya Selous ulivyogeuka vita vya askari na wakazi jirani

KATIKA baadhi ya maeneo nchini, kuwapo kwa hifadhi za misitu na wanyama kumesaidia kuchochea ukuaji uchumi kunatokana na matumizi bora ya rasilimali ardhi na watu, ikiendana na usimamizi bora wa sheria zinazosimamia haki na rasilimali hizo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mvumili, Albilahi Njonjo, ambaye amekatika mkono, akieleza yaliyomkuta. (PICHA NA ABDUL MITUMBA)

Miongoni mwa maeneo ambayo uwepo wa hifadhi za taifa zimechangia kuwepo migogoro katika jamii husika ni Wilaya ya Liwale, mkoa wa Lindi, nayozingirwa na Hifadhi ya Pori la Akiba la Selous wilayani hapo.

Tayari kuna malalamiko kwamba wananchi wanaoishi katika Kata za Likulyungu na Kichonda wilayani humo, wakidai askari wa wanyamapori wa hifadhi hiyo wanawanyanyasa kayika nyendo zao za kudhibiti ujangili.

Ni malalamiko yaliyopo katika kona nyingi za wilaya nzima, ingawaje katika vijiji vya kata za Kikulyungu na Kichonda, zinazopakana na hifadhi hiyo kwa karibu, ndiyo kuna sauti kubwa zinazopazwa. Ni umbali wa kata kilomita 12 kutoka Liwale mjini.

Pia, umbali kutoka ziliko kata hizo zilipo na mto Matandu ambako ndiko kwenye mpaka rasmi wa pori hilo, ni umbali wa kilomita 80.

Malalamiko yanayozua mgogori baina ya askari hao na wananchi, ni kuwekewa vizuizi vya barabara wakati wote katika barabara zinazounganisha vijiji hivyo na pori husika.

“Matokeo yake ni kuzuka migogoro isiyokwisha kati ya wananchi na askari hao na tayari imesababisha madhara makubwa, ikiwamo watu kuuawa na wengine kujeruhiwa kwa risasi, hadi kukatwa viungo vyao,” anasema Sofia Giza, mkazi wa kitongoji cha Mvumili, kilichopo katika kijiji cha Kichonda.

Mkazi mwingine wa kijiji cha Kikulyungu, Jafari Matimbwa, anadai kuwa hali ya askari hao kuweka vizuizi kila sehemu nje ya mpaka wa hifadhi hiyo, ni kinyume na sheria zilizopo na wanakitafsiri kuwa aina Fulani ya unyanyasaji unaofanywa na wananchi.

“Kuna sheria gani inayowaruhusu askari hao kukamata watu na kuwapiga bila kuwaambia nini makosa yao na wakati wingine wakiwaambia ni uongo,” anasema.

Diwani wa kata ya Kichonda, Hassan Makwendo, analalamika kuwa kuna wakazi wake wanaoonewa na askari wanyamapori na matendo hayo yamekuwa yakiongezeka kila kukicha.

Anataja tukio mojawapo ni la Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mvumili, Albilahi Njonjo aliyepigwa risasi na askari hao.
Diwani hiyo anasema, mwenyekiti huyo alipigwa risasi asubuhi ya Septemba 8 mwaka jana, alipofika nyumbani kwa jirani yake ambako askari wanne wa wanyamapori walipovamia kwa ajili ya kufanya upekuzi.

“Alipojaribu kuhoji kwa nini askari hao hawakupitia kwanza ofisi ya serikali ya kijijim kabla ya kufanya upekuzi huo kama sheria inavyoelekeza, mmoja wao alimwambia mwenzake kuwa asiwapotezee muda, ndipo alipofyatua risasi na kumpiga mkononi,” anasema diwani huyo.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mkazi mwingine, Abilahi Njonjo, anayetamka: “Kibaya zaidi askari hao wamekuwa wakituambia kuwa, sisi binadamu hatuna faida mbele ya wanyama, kwa sababu tukifa tunafukiwa ardhini, wakati wanyama wanaliwa baada ya kuuzwa na wakiwa hai wanatumika kwa ajili ya utalii."

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kichonda, Bashiri Lichunda, naye ana ufafanuzi kuwa: "Kila siku ni kesi tu za malalamiko zinazowahusu askari hao kuwanyanyasa wananchi. Hatuwezi kuendelea kukaa kimya huku wananchi wakilalamikia ukatili wa kutisha wanaofanyiwa na askari wachache tena tunaowamudu.”

Kiongozi hiyo wa kijiji anawasihi askari wenye tabia hizo kuacha mara moja, kabla mambo hali haijawa mbaya.

Mzazi wa Abilahi aliyepigwa risasi na kusababisha mkono wake kukatwa, Mzee Ali Njonjo, anelekeza malalamiko ya familia yake kwa kile anachokiita kuwa 'msiba' kwani kijana huyo alikuwa nguzo kuu ya familia kiuchumi na masuala mengine ya kijamiii.

“Sina cha kufanya mwanangu, kutoka kuwa nguzo ya familia hadi kuwa tegemezi. Hawezi tena kufanya kazi, hasa ikizingatiwa sisi ni wakulima tena wa jembe la mkono,” anasema Mzee Njonjo.

UFAFANUZI WA VIONGOZI
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Mohamed Mtesa, anaagiza kuwa matukio hayo anayoyataja ya ‘kikatili’ yaachwe mara moja, kwani ni kinyume na hali za binadamu.

“Haiwezekani watu waanze kujuta kwa nini walizaliwa na kuishi Liwale, kwa sababu ya askari wachache wa pori la akiba 0la Selous. Naomba wajirekebishe haraka,” anatamka Mtesa, katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Liwale.

Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Ephraim Mbaga, anakiri wilaya yake kukumbwa na matukio hayo anayayoyataka kuwa ‘si ya kawaida’ yanayowahusisha askari wa Pori la Akiba la Selous, dhidi ya wananchi.

Kiongozi huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo, anathibitisha tukio la mwenyekiti wa kitongoji kujeruhiwa kwa risasi na anafafanua hatua inayochukuliwa kuwa iko katika anachokitaja kuwa “mamlaka nyingine za maamuzi.”

Mbaga anasema amelazimika kuunda kamati ya watu watatu kuchunguza chanzo cha matukio hayo na kusisitiza kwamba ikibainika kuwepo kasoro zinazohusiana na uwajibikaji, serikali itachukua hatua kali.

Mkuu wa Kanda ya Kusini Mashariki ya Pori la Akiba Selous wilayani Liwale, Salum Kulunge, naye kama walivyo watangulizi wake, anathibitisha kuwapo matukio hayo, lakini anawaetea askari wake kwamba walifanya hivyo kutokana na wananchi kuwavamia.

Anaongeza kuwa, katika harakati za kujitetea, ndiyo bunduki ya askari mmoja ilifyatuka kwa bahati mbaya na risasi ilimpiga mwenyekiti huyo mkononi.

Kuhusu askari wake kuweka vizuizi nje ya mpaka wa pori, Kulunge anasema inatokea katika mazinguira ambayo raia wema kuwapigia simu askari juu ya kuwepo majangili katika maeneo yao.

Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka, anasema umefika wakati wa askari hao waacha vitendo vya kinyama dhidi ya raia, kwani Liwale inahitaji amani, ili kuwawezesha watu kupatumia vyema katika uzalishaji mali na maendeleo mengine.

“Ni wakati wa kila mwana Liwale kutimiza wajibu wake. Sisemi haya kwa kuwalinda au kuwatetea wanaofanya ujangili katika hifadhi, lakini haki ichukue nafasi yake. Kama kuna anayejihusisha na ujangili akamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria na siyo kumchukulia sheria mkononi,” anasema Kuchauka.