Hii ni kwa sababu kwenye makaratasi, Tanzania imejipambanua kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi, vichanga na watoto chini ya miaka mitano, lakini kwenye utendaji ni tofauti.
Wanawake wanapojifungua, wanakumbana na matatizo lukuki ikiwamo huduma zisizoridhisha kutoka kwa wahudumu wa afya na ukosefu wa dawa pale yanapotokea matatizo.
Mratibu wa Mtandao wa Utepe Mweupe (WRA), Rose Mlay, anasema kila saa moja mjamzito mmoja anapoteza maisha wakati wa kujifungua hapa nchini.
Anasema wengi wanapoteza maisha kwa matatizo yanayozuilika na kwamba kama serikali itaamua kuweka mkazo kwa kutenga bajeti stahiki kuboresha vituo vya afya, hali hiyo inaweza kuwa historia.
Anasema bajeti ya kuwahudumia wajawazito na watoto wachanga hasa kwenye vituo vya afya haipewi kipaumbele, hali inayosababisha ukosefu wa dawa, damu salama, vifaa tiba na wahudumu.
Anasema serikali ilikwishaweka mikakati ya kukabiliana na vifo hivyo; kwa kutoa maelekezo kuwa huduma za dharura zipatikane kwenye vituo vya afya, lakini matokeo hayajaonekana.
“Nimesema bajeti ni ndogo na hata inayotengwa haipelekwi kwenye vituo kwa wakati kwa hiyo ni kama jambo hili halijapewa uzito wa kutosha,” anasema Mlay.
Anaongeza kuwa: “Kwa mfano mwaka jana, wilayani Nkasi, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuwapumzisha akina mama wanaofanyiwa upasuaji takribani Sh. milioni 150, zilichukuliwa kujenga maabara za sekondari.”
Anasema maabara ni jambo la msingi, lakini fedha zilizochukuliwa hazikuwa sahihi kwa kuwa zililenga kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Anasema mikakati ya serikali ilikuwa kwamba hadi mwaka jana, nusu ya vituo vya afya nchini yaani vituo 350 vitoe huduma ya dharura ya upasuaji, lakini hadi sasa jambo hilo halijatekelezwa.
“Tuna vituo vya afya 700 na hadi sasa nadhani ni vituo 100 tu nchi nzima vinavyotoa huduma za dharura. Ushauri wetu ni kwamba bajeti iongezwe, itolewe kwa wakati na iwekewe wigo ili isitumiwe kwa shughuli nyingine,” anasema Mlay.
Anasema ili kukakabiliana na vifo hivyo, ni lazima kila kituo cha afya kiwe na chumba cha upasuaji, damu salama, madaktari wa nusu kaputi na wa upasuaji pamoja na wakunga.
“Tunataka kuhakikisha kwamba tunapambana na hali hii na wanawake wanapojifungua wanajione wako salama bila kuhofia kifo kutokana na miundombinu duni, ukosefu wa madaktari au dawa,” anasema.
Hata hivyo, taarifa ya Mtandao wa Utepe Mweupe (WRA), inaeleza kuwa ni vigumu kubaini matumizi ya Halmashauri katika kukabiliana na vifo hivyo na kwamba kampeni ya ‘Wajibika Mama na Mtoto aishi’ inalenga kujenga uwazi wa bajeti kwa watendaji.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ya mwaka 2014 inaonyesha kuwa Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto, lakini wanaharakati wa WRA wanaeleza kuwa vifo 432 kati ya vizazi hai 100,000 ni vingi kwa kuwa vinaweza kuzuilika.
Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa kwa miaka 20 iliyopita, vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga vimepungua kwa kiasi kidogo kutoka vifo 529 vya vizazi hai 100,000 mwaka 1996 hadi vifo 432 vya vizazi hai 100,000 mwaka 2014.










