Wimbo wamfanya Msaga Sumu aijue nchi

21Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wimbo wamfanya Msaga Sumu aijue nchi

MTAALAM wa nyimbo za uswahilini, Seleman Jabir, maarufu kwa jina la 'Msaga Sumu' amesema kuwa wimbo wake wa 'Lowassa Chaguo la Wengi' umesaidia kufika mikoa mbalimbali hapa nchini, ambayo alikuwa hajawahi kuikanyaga.

Msaga Sumu

Msanii huyo aliitaja baadhi ya mikoa aliyofanikiwa kufika wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana kuwa ni Mwanza, Mbeya, Tabora na mingineyo ambayo katika maisha yake hakutarajia kufika.

Aliiambia Nipashe kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa wimbo huo umemnufaisha.

"Wimbo haukuninufaisha sana kama baadhi ya watu wanavyosema...nilichopata ni fedha ya kawaida na kufahamu baadhi ya mikoa ya Tanzania ambayo sikuwahi kufika," alisema Msaga Sumu.

Wakati huohuo, msanii huyo alisema yupo mbioni kuachia wimbo wa timu anayoipenda ya Yanga Africans ili kulipa fadhila ya wimbo aliowaimbia mashabiki wa Simba.

"Mimi ni mwana Yanga, lakini niliimba wimbo wa Simba kwa kuwa Simba walikuwa bora kwa kipindi kile na sasa nimeandaa wimbo mpya wa Yanga ambao utakuwa mkali kuliko ule wa Simba," alisema.