Zulf atamani nyayo za Luiza Mbutu

21Mar 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Zulf atamani nyayo za Luiza Mbutu

MUIMBAJI wa bendi ya Utalii Sound, Zulfa Omar 'Shery Zuu', amesema anatamani kuwa kama Luiza Mbutu wa bendi ya African Stars, kwa madai kwamba mwanamuziki huyo ni mvumilivu, anajali kazi yake na anajua nini anafanya.

Zulfa

Zulfa alisema kuwa Luiza Mbutu miongoni mwa waimbaji wachache wa kike wanaojiheshimu na kujali kazi zao, hivyo na yeye anatamani kufuata nyayo hizo ili afikie malengo aliyojiwekea ya kuwa matawi ya juu.

Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Nipashe kufuatia hatua yake ya kujitosa kwenye muziki wa dansi, huku pia akiandaa albamu binafsi ambayo itakuwa na nyimbo za mitondo mbalimbali ukiwamo mchiriku.

"Malengo yangu ni kutaka kuwa msanii mkubwa kama alivyo Luiza Mbutu, kwani ametokea mbali katika sanaa na ni mtu mvumilivu anayejali kazi yake na anajua nini anafanya," alisema Zulfa na kuongeza:

"Sio Luiza tu bali hata Lady Jaydee naye ni kama kioo kwangu kwani ni miongoni mwa wasanii wachache wa muziki wa bongofleva wanaojiheshimu na kujali kazi zao ninataka kuwa kama hao wawili na ikibiti niwe wa kimataifa."

Alisema kuwa awali alikuwa akiimba taarab lakini sasa amegeukia kwenye dansi na bongofleva ili kuonyesha kipaji chake ambacho anaamini kinaweza kumfikisha mbali katika mafanikio.

Muimbaji huyo kwa sasa ana wimbo wa 'Kubwa Jinga' alioimba katika mtindo wa mchiriku na anaendelea kuandaa mwingine ikiwa ni mwendelezo wa kuandaa albamu yake ya kwanza