Nancy Sumari kufungua Tanzania Fashion Festival 2023

27Sep 2023
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nancy Sumari kufungua Tanzania Fashion Festival 2023

MREMBO wa Tanzania na 'Miss World Africa' mwaka 2005 Nancy Sumari anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kufungua Onesho la Mitindo la 'Tanzania Fashion Festival 2023' Septemba 30 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Nancy Sumari.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, Mwanzilishi na mratibu wa onesho hilo, Deogratius Kithama, alisema kuwa huu ni mwaka wa sita tangu kuanzishwa kwa onesho hilo ambapo kwa mwaka huu wameandaa burudani kubwa na ya kuvutia kwa watu watakaoshiriki.

"Ni heshima kubwa kwetu kwa Nancy kukubali kufungua tamasha la mwaka huu kama mgeni rasmi, huku tukifahamu nguvu yake ya ushawishi kwenye mitindo na urembo Tanzania. Katika onesho la Jumamosi hii mbali na kuwa na maonesho ya mavazi, pia kutakuwa na burudani za muziki pamoja na dansi," alisema Kithama.

Alisema kuwa tamasha hilo ni nafasi muhimu kwa vijana wanaochipukia katika tasnia ya mitindo pamoja na wale waliopo kuja kuona mitindo mipya na kujifunza ili kuboresha kazi zao na kuweza kushiriki katika maonesho mbalimbali hata nje ya Tanzania.

Aliongeza kuwa tamasha hilo lilianzishwa mwaka 2018 ambapo Nancy anaungana na orodha ya wanamitindo wengine wa kimataifa waliowahi kufungua onesho hilo akiwamo Millen Happiness Magesse na Miriam Odemba.

Akizungumzia tukio hilo, Nancy alisema...“Kwangu ni furaha kubwa kuungana na vijana wenzangu wengi Kwenye tasnia ya mitindo. Napenda mitindo ya Tanzania na nadhani kupitia jukwaa hili tunaweza kuibua vipaji vingi zaidi Kwenye tasnia ya mitindo," alisema Nancy.