Msanii Kusah apagawisha wanafunzi Green Acres

23Sep 2023
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Msanii Kusah apagawisha wanafunzi Green Acres

MSANII wa nyimbo za Bongo fleva Salmin Ismail maarufu kama Kusah, amezitaka shule nchini kutenga muda wa kutosha wa michezo ili waweze kuibua vipaji mbalimbali vya wanafunzi.

MSANII wa nyimbo za bongo fleva Salmin Ismail maarufu kama Kusah, akisalimiana na meza kuu kwenye mahafali ya 23 ya shule ya msingi na sekondari Green Acres ya Mbezi Beach Salasala jijini Dar es Salaam.

Aliyasema hayo Leo mara baada ya kutumbuiza kwenye mahafali ya 23 ya shule ya awali, msingi na sekondari ya Green Acres ya Mbezi Beach Salasala jijini Dar es Salaam.

Amesema sanaa ni muhimu kwani baadhi ya watu duniani wamefanikiwa kuwa maarufu na kupata utajiri mkubwa kutokana na vipaji vyao vya muziki, mpira, kuogelea na michezo mbalimbali.

“Kuna mwanafunzi mwingine anaweza asiwe vizuri sana darasani lakini akawa mzuri sana kwenye kuimba au kucheza mpira kwa hiyo lazima kipaji chake kiibuliwe mapema na kikuzwa kwasababu unaweza kukuta hiyo ndiyo thawabu yake aliyopewa na Mungu,” amesema na kuongeza

“Kuna wanafunzi ni wazuri sana kwenye masomo ya kawaida tuwaache waendelee na mkondo huo lakini siyo lazima kila mwanafunzi aende kwenye mkondo wa masomo kuna wengina kama sisi tumebahatika vipaji vya kuimba tu na tunavitumia kuishi,” amesema

Amesema yeye binafsi hakufanikiwa kufika mbali kimasomo lakini baada ya kubaini ana kipaji cha kuimba alifanikiwa kukiendeleza na kwa sasa ndicho kinamsaidia kuendeleza maisha yake kwa ujumla.

“Haiwezekani wanafunzi wote waje kuwa wahandisi, wanasheria, wahasibu kuna wengine vipaji vyao vitajielekeza kwenye mpira wa miguu, muziki kama mimi, maigizo na kadhalika kwa hiyo serikali na wadau wengine tuweke umuhimu kwenye kuendeleza vipaji vya wanafunzi,” amesema