Mpoto: Wasanii kataeni kufungwa pingu za akili

29Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mpoto: Wasanii kataeni kufungwa pingu za akili

MOJA na mambo ambayo baadhi ya wasanii wakongwe wa muziki wa kizazi kipya wamekuwa wakilalamikia ni wenzao wanaochipukia sasa kuacha vionjo vya muziki wa Tanzania na kuiga vya nje.

MRISHO MPOTO

Mbali na kuiga vionjo vya nje, wamekuwa wakidaiwa pia wakikumbatia tamaduni za kigeni na kusahau za kwao.

Kwa upande wake msanii na mtaalam wa kughani ushairi, Mrisho Mpoto naye amepigilia msumari na kuwataka wasanii wanaopenda kuiga vya nje kuachana na umagharibi na kukumbusha kuwa kufanya hivyo ni sawa na 'kupigwa pingu za akili'.

Mpoto alisema hayo wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na Nipashe na kuongeza kuwa umefika wakati wasanii kuwa na vitu vyao wenyewe, sio kuiga.

"Sio vibaya kuiga ubunifu katika kazi, lakini ni vyema wasanii wakaepuka kuiga tamaduni za nje ambazo mimi ninaziona ni kama kupigwa pingu za akili," alisema Mpoto na kuongeza:

"Wasanii wawe na wasimamizi wa kazi zao, wasitegemee kufanikiwa kwa kuiga mambo yaliyo nje na utamaduni wetu."
Msanii huyo alisema anatambua kuwapo wasanii waliowahi kutamba, lakini kwa sasa hawasikiki tena kwa sababu mbili alizozitaja awali.

Mpoto ambaye ni maarufu kwa jina la Mjomba, kwa sasa ana wimbo mpya alioupa jina la 'Sizonje' ulioingizwa kwenye tuzo za Kora na sasa anataka mashabiki wamuunge mkono ili aibuke na ushindi.