Mgendi aelimisha kwa nyimbo, filamu

15Feb 2016
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mgendi aelimisha kwa nyimbo, filamu

MMUIMBAJI nyimbo za Injili, Jeniffer Mgendi ambaye pia amejikita Bongo Movies amesema amejikita zaidi katika filamu zinazoelimisha ili kusaidia jamii kuzingatia maadili mema.

Jeniffer Mgendi

Alisema kama ilivyo kwenye nyimbo zake za Injili ndivyo anavyofanya pia filamu kwa kuwa anaamini kwamba kama Mtanzania huo ndio mchango wake kwa taifa lake.

"Nimeamua kushiriki kutengeneza filamu huku nikiendelea na kazi ya kumuimbia Mungu wangu kwa sababu ninaamini kwamba nina nafasi ya kuelimisha kwa njia ya nyimbo na filamu, ndio maana kazi zangu zimejikita katika kuelimisha umma," alisema Mgendi.

Alifafanua kuwa hata filamu yake ya 'Chai Moto' inaelezea misukosuko ya kimaisha inayozidi kuongezeka miongoni mwa jamii ya Watanzania na ameonyesha ni namna gani watapata suluhisho.

Muimbaji huyo alisema kuwa Mungu amemjalia kuwa na kipaji cha kuimba na kuigiza, hivyo hana budi kukitumia ipasavyo kipaji chake ili kuisaidia jamii ili pale inapokuwa imekosea iweze kurudi kwenye mstari.