Dimpoz ajivunia kibao cha Achia Body

29Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Dimpoz ajivunia kibao cha Achia Body

MWISHONI mwa mwaka jana nyota muziki wa kizazi kipya, ‘Ommy Dimpoz’, alizindua video ya wimbo wa 'Achia Body' ambao anasema kuwa sasa inazidi kukata mawimbi kwa kurushwa katika televisheni za nje, ikiwamo Trace TV ya Nigeria na Ufaransa.

Ommy Dimpoz

Ommy Dimpoz ambaye jina lake halisi ni Omary Nyembo, alisema kuwa Trace Urbun walishatangaza kurusha video ya wimbo huo mfululizo kwa wiki nzima kitu ambacho kinaonyesha luninga hiyo imeikubali kazi yake hiyo.

"Wimbo huo kama zilivyo nyingine nilizowahi kutoa, ulianza kukubalika taratibu na sasa unazidi kufanya vizuri hadi kupenya katika televisheni za nje ya nchi...hii ni fahari kwangu na kwa mashabiki wangu," alisema Dimpoz alipozungumza na Nipashe juzi.

Lakini akasema kuwa bahati mbaya wapo baadhi ya mashabiki wenye mtindo wa kuhukumu nyimbo mpya kwa muda mfupi kabla ya kuzipa muda na kuzielewa vyema.

Alitolea mfano wa wimbo wake wa ‘Wanjera’ kwamba baadhi ya mashabiki waliuponda, lakini baadaye wakauelewa na wakaupenda, hivyo akawaomba wawe wanajipa muda wa kutosha wa kusikiliza nyimbo kabla ya kutoa hukumu.