Wanawake Uganda wanavyohadaiwa na wenzao kuingia kwenye biashara ya ng

06Feb 2016
Nipashe
Wanawake Uganda wanavyohadaiwa na wenzao kuingia kwenye biashara ya ng

MARA ya kwanza, Sarah Nakintu alimshukuru rafiki yake kwa kumjulisha kuwepo kwa nafasi za kazi kwenye masoko na maduka huko Dubai.

Nakintu, mwanamke mwenye umri wa miaka 27 kutoka mji mkuu wa Uganda wa Kampala, alimuamini rafiki yake huyo ambaye aliwahi kufanya kazi Umoja wa Falme za Kiarabu na kuonekana kuwa na fedha nyingi.
Nakintu alifuata maelekezo yote ya rafiki yake huyo. Kuwasilisha pasipoti halali kwa mtu anayeshughulikia ajira hizo ambaye ataandaa mipango ya tiketi ya ndege na viza.
Mara baada ya nyaraka hizo kukamilika, Nakintu alilipa kiasi kilichopendekezwa cha ‘fedha ya asante’ kwa rafiki yake huyo – dola za Kimarekani 200 (takriban sh 440,000) taslimu.

Nakintu (ambaye aliomba jina lake halisi lisitumike) alishauriwa kuonyesha tu kibali cha kuingilia ndani ya ndege kwa safari ya Kigali, Rwanda, na afiche kibali chake cha kumuwesha kuunganisha safari kwenda Dubai kwa vile maofisa wa uhamiaji wanazuia wahamiaji ambao hawakutumia mashirika ya ajira ya serikali kwenda kutafuta ajira nje ya nchi.
Lakini wakati Nakintu alipopokelewa na mwanamke mmoja wa Kiganda ajulikanaye kama Jane Saad kwenye uwanja wa ndege wa Dubai, aliambiwa kumkabidhi hati yake ya kusafiria na kisha akafahamishwa kwamba atakuwa akifanya kazi ya ukahaba.
"Kuanzia mwanzo nilikuwa na uoga na nikajaribu kupinga lakini mwanamke huyo alitutishia na kusema kulikuwa hakuna njia nyingine yoyote kwa vile alikuwa amewekeza fedha nyingi kwenye safari yetu," Nakintu alikaririwa akilieleza shirika la habari la Thomson Reuters Foundation.
"Taratibu tulikata tamaa na kuanza kufuata maelekezo yake."
Nakintu ni mmoja tu kati ya maelfu ya wanawake ambao kila mwaka wanasafirishwa kwenye utumwa wa ngono, huku kundi la kampeni ya kupinga utumwa ya Walk Free lenye makao makuu yake nchini Australia likikadiria kwamba kuna watu milioni 36 walionaswa kwenye utumwa wa kisasa kote duniani.

KUTOSWA NA WANAWAKE WENGINE
Kama ilivyokuwa kwa wengine wengi, Nakintu alisema alikuwa hategemei kwamba rafiki yake au wanawake wengine kutoka nyumbani kwao mwenyewe wangemdanganya kuingia kwenye kazi ya ukahaba na kwa maana hiyo hakuwa amejiandaa kwa lolote.
Taarifa moja ya kila mwaka kuhusiana na biashara ya usafirishwaji wa binadamu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ya mwaka 2015 ilizungumzia juu ya mtandao wa wanawake wa Uganda unaoratibu upelekwaji wa wanawake wa Uganda kufanyishwa biashara ya ngono nje ya nchi.

Taarifa hiyo iliorodhesha nchi zinazojulikana kuhusika zaidi kuwa ni Kuwait, Muungano wa Falme za Kiarabu na Kenya.
Kwenye siku yake ya kwanza mjini Dubai, Nakintu alielezwa kwamba alikuwa ana deni la Saad la dola za Kimarekani 8,000 kama ada za kupatiwa kwake kazi ambazo itabidi zilipwe kwa awamu pamoja na gharama za malazi na chakula.
Gharama hizo zilikuwa ni za juu sana kwa mhamiaji ambaye ndiyo kwanza anawasili. Kitanda kwenye chumba kimoja chenye wanawake hadi watatu kwa kawaida kinagharimu Dh 1500 (takriban shilingi 880,000).
Kufikia lengo hilo kimapato, Saada alimwambia Nakintu kwamba itambidi awaburudishe kingono wanaume takriban 10 kwenye siku mbili za kwanza.
Mbali na kukabidhi hati yake ya kusafiria, Nakintu alipaswa kufanyiwa ‘tambiko la ndumba’ ambapo alitakiwa kuapa kwamba atakuwa akikabidhi mapato yake kwa makuwadi huku akipewa kitisho cha kuuliwa ndani ya siku 10 kama amri hiyo haitatekelezwa.
Ripoti ya Usafirishwaji wa Watu ya mwaka 2014 ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilieleza kwamba watu wanaosafirisha wanawake kwa ajili ya biashara ya ngono walikuwa wakitumia matambiko na ubabe kuwashinikiza wanawake wa Uganda kuingia kwenye biashara hiyo.
"Makuwadi hao walikuwa wanawake katili ambao waliuza hati zetu za kusafiria na tiketi za kurudia kwa changudoa wazee waliokuwa wakitaka kustaafu na kurudi Uganda," said Nakintu.
Nakintu alihamishwa na Saad hadi Abu Dhabi ambako wafanyakazi za ngono wanaweza kupata dau kubwa zaidi kwa vile walikuwa wanachukuliwa kama mauzo mazuri kwa wateja wa hali ya juu.
Huko alikutana na mwanamke mwingine Mganda, aliyetambuliwa kama Maydina, ambaye alipanda kutoka kuwa changudoa wa klabu ya usiku mjini Abu Dhabi hadi kuja kuwa kuwadi aliyeolewa na mtendaji mmoja kwenye biashara moja ya kiwango cha juu.
KUWADANGANYA WATEJA
Maydina alimueleza Nakintu kwamba siri ya utajiri kwenye kazi ya ngono mjini Abu Dhabi ilikuwa ni kunasa wanaume wateja wazungu – na kuhakikisha anapata namba zao za simu kwa ajili ya kuendeleza nao biashara hiyo.
Siku chache baada ya kukutana mara ya kwanza, mfanyakazi huyo atampigia mteja huyo na kusema kwamba alikuwa na mimba, akitaka fedha kuficha utambulisho wake au dola 10,000 kwa ajili ya kurudi Uganda kwenda kutoa mimba.
Wafanyakazi hao wa ngono baadaye wanaweza kuendelea kudanganya, wakiwaomba wateja wao fedha zaidi kwa sababu ya matatizo ya kimatibabu.
Nakintu alisema wafanyakazi wapya kwenye biashara hiyo ya ngono walikuwa wakitegemewa kuwalenga wanaume watatu katika mwezi wao wa kwanza kwa mtindo huo na ni wachache miongoni mwao ambao walikataa kwa sababu hiyo mara nyingi ndiyo ilikuwa njia pekee wanayoweza kutumia kulipa madeni yao.
"Kwa kweli tulikuwa na wasiwasi," alisema Nakintu.
Nakintu alifanikiwa kuondoka Abu Dhabi Mei mwaka jana baada ya kuwa huko kwa karibu mwaka mmoja na kuwa amelipa sehemu kubwa ya madeni yake.
Mwanamke huyo alirudi Uganda, akiwa ‘amechoka’ kwa jinsi alivyodanganywa na kufanyiwa mambo ambayo hakuyategemea.
Baadhi ya wenzake aliokuwa nao chumba kimoja baada ya kurudi nyumbani wao wenyewe hawakuchukua muda kuingia kwenye shughuli za kudanganya wenzao kwenda kufanya kazi hiyo ya ngono, wakiwalenga wanawake wengine vijana nchini Uganda waliochoshwa na mishahara midogo na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira.
"Ukuwadi ilikuwa rahisi kwa vile mtu atauliza marafiki kutafuta wahanga na kumlipa huyo rafiki dola 100 kwa kila muhanga waliyemuingiza mkenge. Mimi nilikataa kufanya hivyo," Nakintu alisema wakati wa mahojiano kwenye duka moja dogo ambalo hivi analiendesha mjini Kampala akiuza vitu vya nyumbani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inaiorodhesha Uganda kama taifa la Kiwango cha Pili kwenye ripoti yake ya kila mwaka ya usafirishaji wa binadamu, ikimaanisha haijakidhi kikamilifu viwango vya chini kabisa vya Sheria ya Kulinda Wahanga wa Usafirishwaji ya Marekani lakini inafanya juhudi kubwa kufikia hatua hiyo.
Moses Binoga, kamishna wa polisi anayeongoza kikosi kazi cha kukabiliana na biashara ya usafirishaji binadamu nchini Uganda, alisema serikali ilikuwa imeongeza umakini kwenye njia zote za kutokea nchi kulinda wanawake vijana ambao ni rahisi kwao kudanganyika kama Nakintu dhidi ya usafirishwaji wa kingono.
Mwaka jana, serikali hiyo ilizuia wanawake vijana takriban 300 kuondoka nchini humo baada ya kubainika kwamba walikuwa wakipelekwa nje mahususi kwa biashara ya ngono.
Binoga, ambaye Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetambua juhudi zake katika kupambana na usafirishwaji wa binadamu, alisema serikali pia ilikuwa imewafungulia mashtaka na kuwapata na hatia wasafirishaji kadhaa lakini ni kazi ngumu kupambana na tatizo hilo.
"Changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba japokuwa tunaweza kuwafungulia mashtaka wasafirishaji kwenye ardhi ya Uganda hatuna uwezo kisheria wa kuwafungulia mashtaka wale walio kwenye mataifa yanayowapokea," alisema.
"Vile vile wakati tunawafungulia mashtaka inabidi tutenganishe kati ya wahanga waliodanganywa na wale waliokubali wenyewe mpango wa kwenda mataifa ya Kiarabu na kufanya kazi kama changudoa."