Zipo sababu zinazotolewa katika hilo, hata wakahisi tiba za asilia ni muhimu kwao kuliko rasmi ya hospitalini. Hapo inajumuisha mambo kadhaa, ikiwemo elimu duni kuhusiana na hitaji la vipimo vya matibabu hospitalini na uduni wa maisha unaofanya watu wakimbilie kwenye tiba asilia, wakiamini kuna matibabu ya kila aina huko. Ushuhuda wa jamii hiyo, uko kwa kijana Almachius Barongo (20), mkazi wa kijiji cha Maiga, Kata ya Maruku, wilaya ya Bukoba Vijijini, ambaye alipata ajali ya pikipiki na kuamua kwenda kwa mganga wa tiba asilia kusaka matibabu. Mara tu baada ya ajali iliyomkuta, alianza safari kwenda Muleba, kusaka matibabu kwa njia hiyo ya asili. Barongo anasema kuwa, mwaka mmoja uliopita wakati amepanda pikipiki kama abiria kutokea kijiji cha Katoma, wanapata ajali na akavunjika mikono yote miwili. Anasema kuwa, hali mbaya kifedha mfukoni ndiyo iliyomfikisha katika hatua ya kaumua kwenda kutafuta tiba, kwa mganga wa kienyeji. Barongo anasema kuwa, alipata tiba mahali hapo kwa miezi miwili mfululizo na hata akafanikiwa kupona mkono wa kulia. Pamoja na kuwa ni mkono mmoja tu uliopona na mwingine umepata ulemavu na kupooza, kijana huyo bado ana imani kubwa na tiba hiyo na anaongeza: “Nilikuwa narudi nyumbani, baada ya kupata ajali dereva wa pikipiki alikimbia nikawa nimevunjika mikono yote. Nimepata matibabu kwa miezi miwili mfululizo mkono mmoja ulipona, lakini huu wa kushoto umepooza.” Anasimulia kuwa, alipokwenda kwa mtaalam wa tiba za asili, hakupata kuchukuliwa picha ya ‘X-Ray’ ambayo muhimu sana kwa mtu aliyevunjika au kuteguka. Barongo hivi sasa ndiyo yuko katika harakati za kusaka michango kutoka kwa wasamaria wema, ili akatibiwe hospitalini mkono ambao haukupona. Imani ile ile ya kupata matibabu kwa dawa za asili, baada ya kuvunjika, nayo imemfanya Mzee Komanya Makwi (75) asafiri kutoka kijiji cha Bwongera, kata ya Muganza mkoani Geita, ili kupatiwa matibabu na mtaalam huyo wa asili aliyemtibu kijana Barongo. WENYE HOSPITALI WAFUNGUKA Kwa miongo kadhaa sasa, kitongoji cha Kazilantemwa katika kijiji hicho cha Buleza kimekuwa maarufu Kwa kupokea wagonjwa kutoka maeneo tofauti nchini, wanaotafuta matibabu ya asili. Kwa wenyeji wengi wa mkoa wa Kagera wanalifahamu eneo hilo kwa jina la “Kayunga Magufa” jina linalobeba tafsiri ya muungaji wa mifupa. Hiyo ndiyo sababu ya wagonjwa waliovunjika kufika kijijini hapo. Ni mahali ambako kila wakati kufika katika kitongoji hicho kila siku, hata baada ya kufariki kwa mama wa mtaalam wa sasa wa kuunga mifupa, aliyeitwa Thereza Mushwahili. Mama huyo anayedaiwa kumrithisha mtaalamu wa sasa, alifariki miaka mitatu iliyopita huku akiwa tayari kisharithisha watoto wake utaalam huo. Mwanamke huyo inaelezwa alipewa ujuzi huo na mama mkwe wake, katika zama hizo ju ya namna dawa zinazotumika imebaki kuwa siri ya matabibu hadi sasa. Inaelezwa katika siku za mwisho wa uhai wake aliawaandaa watoto wake kwa ajili ya kazi hiyo, kwa kuwatuma kupeleka dawa na kutoa matibabu kwa wagonjwa waliokuwa sehemu za mbali. Ongezeko la wagonjwa waliovunjika na mahitaji ya msaada wa matibabu ya asili katika kitongoji hicho, yamesababisha tabibu aliyepo sasa kujenga wodi katika makazi ya wataalam hao, ili kuwasaidia wagonjwa wanaotoka maeneo ya mbali. Mmoja wa watoto waliorithishwa ujuzi huo, Deusdedith Mushwahili, anasema amezunguka katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kwenda kutoa huduma hiyo na hata nchi jirani za Uganda, na ndio ilikuwa hatua yake ya awali kupata uzoefu. “Hata watoto wetu tumeanza kuwafundisha jinsi ya kutoa matibabu. Wakati mwingine, mgonjwa anakuja akiwa na majeraha ya kawaida na wengine huwa wanahitaji kuvutwa ili mifupa irudi ndani, ndipo waendelee kupata matibabu,” anasema Mushwahili. Hata hivyo jambo kubwa linalozingatiwa kabla ya mgonjwa kupewa matibabu ni kuwa na picha ya X-Ray, ambayo huwa inaonyesha sehemu yenye tatizo, ingawa pia suala hilo haliwezi kuzuia matibabu kwa mgonjwa ambaye hana picha hiyo. “Ni kama tunashirikiana na hospitali katika kutoa huduma, wagonjwa wengine wanafika hapa wakitokea hospitalini, na wengine hutuomba tuwafuate hospitali kwa ajili ya kuwapatia huduma ya matibabu ya kuvunjika,”anafafanua. Pia anarejea ajali mbaya ya mwaka 1982 maarufu sana mkoani Kagera kama “Safari Leo” iliyohusisha basi lililoua abiria wengi baada ya dereva kushindwa kulimudu na kupinduka wakati likiteremka katika mlima wa Nyangoye ulioko katika manispaa ya Bukoba. Anasema kuwa, alitumwa na mama yake kuwafuata wagonjwa waliovunjika, baada ya kunusurika katika ajali hiyo na kuwapa matibabu na kuwa hata baadhi ya wachezaji wa mpira hufika kupata huduma wanapovunjika. “Wapo wachezaji wengi maarufu wa mpira kama Sanifu Razaro mchezaji wa zamani wa Yanga ambao wamewahi kupata huduma yetu baada ya kuvunjika wakati wakicheza mpira,”anabainisha. Kwa wastani kwa mwezi mmoja wanapokelewa wagonjwa wapya sita, huku idadi kubwa wakiwa ni wale waliovunjika kutokana na ajali za pikipiki, kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya mkoa wa Kagera. Idadi kubwa ya wagonjwa ni wale wanaoendelea na matibabu hivyo hufika kuchukua dawa na kuondoka kutoka kwa wataalam hao ambao ni Deusdedith Mushwahili na ndugu yake Dominick Mushwahili, ambao wanatoa huduma hiyo bila malipo makubwa. Matibabu yanayofanyika katika kitongoji cha Kazilantemwa pia sio habari mpya kwa baadhi ya wataalam wa afya mkoani Kagera, ingawa wanaonyesha wasiwasi wa uhakika wa matibabu hayo. Daktari Bingwa wa upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera Dk.Bakamanya Milanga, anasema pamoja na wananchi kuwa na imani kuhusu matibabu ya dawa za miti shamba, wakati mwingine huleta madhara zaidi kwa mgonjwa. “Kuna aina nyingi za mivunjiko na jinsi ya kuitibu na kuna chembe chembe zinazojenga mfupa, huyo anayetibu kwa dawa za asili ni hatari kumhudumia mwenye vidonda na aliyevunjika misuli,” anabainisha. Dk. Milanga anasema kuwa, mara nyingine hupokea wagonjwa waliovunjika awali na kutumia dawa za asili wakiwa wameanza kupata usaha katika maeneo waliyowekewa dawa na kulazimika kuwafanyia upasuaji. Mtaalam mwingine katika kitengo cha upasuaji kwenye hospitali hiyo Dk. Martine Rwabilimbo, anasema mwili una tabia ya kuota huku ukipigana na magonjwa na baadhi ya wagonjwa hupata matatizo na kukaa wakitibiwa nyumbani na baadaye kufikiri wamepona. “Mwili una tabia ya kupigana na magonjwa, mtu anaweza kupata mvunjiko rahisi ambao mfupa haujahama na akapata matibabu nyumbani, anakuwa anatibiwa isivyotakiwa na atakuwa na ulemavu wa aina fulani,” anasema Ili kuhakikisha huduma zinasogea karibu na wananchi na kuwafanya kutumia huduma hizo badala ya kutegemea tiba za asili kwa kiwango kikubwa, serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuongeza zahanati, vituo vya afya na hospitali. Katika mkoa wa Kagera mwaka 2005 kulikuwa na zahanati 206, vituo vya afya 21 na hospitali 13, lakini hadi kufikia mwaka 2014 zahanati zimeongezeka na kufikia 246, vituo vya afya 31 na hospitali 14.
Tabibu Muleba anayehudumia tiba za mifupa zipatikanazo Moi
04Feb 2016
Nipashe
Tabibu Muleba anayehudumia tiba za mifupa zipatikanazo Moi
WAKATI serikali ikiendeleza Mpango wa Maendeleo ya Serikali (MMAM), inayohimza ujenzi wa zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata, ikiwa ni namna ya kusogeza huduma karibu na wananchi, bado kuna kundi kubwa la wananchi wanaoamini na kukimbilia tiba za asili.










