ZEC ina uhalali kisheria kurudia Uchaguzi wa Zanzibar?

06Feb 2016
Nipashe
ZEC ina uhalali kisheria kurudia Uchaguzi wa Zanzibar?

Zanzibar ni miongoni mwa Nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zanzibar ni Nchi ambayo eneo la mipaka yake linajumuisha eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya kuzaliwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 1 na ya 2 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Zanzibar kama vile ilivyo kwa upande wa Tanzania Bara, kama nchi, huongozwa na Katiba yake na Sheria zake nyingine mbalimbali kusimamia mambo kadha wa kadha, (ambayo si ya muungano), yakiweno na yale ya uchaguzi.
Hivyo basi, ili kung’amua ’Uhalali wa Agizo la Kufutwa kwa Uchaguzi wa Zanzibar’ lililotolewa na Tume Uchaguzi, (ZEC), visiwani humo, ni vema kwanza tukianza kwa kutafakari kwa kina masuala ya msingi yafuatayo:
Taratibu za Usimamizi wa Uchaguzi Zanzibar
Kwa mujibu wa Ibara ya 119 (1)-(2) ya Katiba ya Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, (ZEC), ndiyo Mamlaka pekee yenye Dhamana ya Kuratibu na Kusimamia Masuala yote ya Uchaguzi Zanzibar.
Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake, Tume ya Uchaguzi, (ZEC), itakuwa ni Idara inayojitegemea na mtendaji mkuu wake atakuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na kufanya kazi kwa mujibu wa masharti ya Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Zanzibar, Tume ya Uchaguzi, (ZEC), haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au Idara yoyote ya Serikali, au maoni ya chama cha siasa.
Hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi, (ZEC), katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Zanzibar. Haya yote kadhalika ni kwa mujibu wa Ibara ndogo ya (9);(12); na ile ya (13) zote za Ibara ya 119 tangulia kutajwa hapo awali.
Na kwa upande wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, (The Zanzibar Election Act of 1984), haya yote kwa upana wake yanaonekana tena kupitia Kifungu cha 4;5(a)-(b);7(1)-(4);12(1)-(9);14(1)-(6);16;38(1)-(5) na kile cha 39(1)-(3).
Muhimu: Kwa mujibu wa Kifungu cha 42 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ambacho kinazungumzia ’Utaratibu wa Kuhesabu Kura na Kutangaza Matokeo ya Urais’, ... Mtu au Taasisi yoyote ile itakuwa inafanya Kosa kwa mujibu wa Sheria ikitangaza Matokeo ya Urais kabla Matokeo hayo kutangazwa na Tume yenye Dhamana na kwa kufanya hivyo basi, mara baada ya kupatikana na hatia, atatakiwa kulipa fidia ya Tshs. 500,000/= au kifungo cha miaka mitano jela au ikibidi vyote kwa pamoja.

Ukomo wa Mamlaka ya Rais wa Zanzibar
Kwa mujibu wa Ibara ya 28(1) ya Katiba ya Zanzibar: mtu ataendelea kuwa Rais mpaka Rais anayefuata atakapo kula kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar.
Halikadhalika, Kifungu chake kidogo cha 2 kinasema: Kufuatana na maelezo ya kijifungu (1) cha kifungu cha 28, Rais ataacha madaraka yake mara baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe, ambapo: kama yeye ni mtu ambaye kwa mara ya kwanza amechaguliwa kuwa Rais chini ya Katiba ya Zanzibar alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais; na kwa sababu nyenginezo ni mtu wa mwisho kushika madaraka hayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais, au pasingelikuwa na sababu ya kifo chake, basi angalikula kiapo hicho.
Na kama haitoshi, Sheria hiyo hiyo kupitia Ibara yake ya 31(1) inatujuza kwamba, Mtu anayechukua Madaraka ya Urais, kabla ya kuanza wadhifa huo, atakula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kazi kama kitavyowekwa na Baraza la Wawakilishi lakini kwa hali yoyote itabidi ashike madaraka hayo kabla ya kupita siku saba mara baada ya kuchaguliwa; Kifungu kidogo cha (2): Viapo hivyo vilivyotajwa vitaendeshwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar au iwapo hayupo, vitaendeshwa na mtu anayeshikilia nafasi hiyo.

Sababu za ZEC kufuta Matokeo
Hizi ndizo sababu nane zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, (ZEC), Jecha Salim Jecha kuhusiana na kufutiliwa mbali kwa Matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar. Ambazo ni:
Makamishna wa uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, (ZEC), waliripotiwa kupigana kutokana na tofauti zao; makamishna hao hawakufanya kazi kwa mujibu wa Kiapo chao cha kazi, kwani walionyesha dhahiri kuwa na upendeleo fulani; katika vituo vyengine, hususan kisiwani Pemba, ambacho ni miliki ya Zanzibar, kura zilizopigwa zilikuwa zaidi ya zilizosajiliwa; masanduku ya kupigia kura hayakupewa ulinzi wa kutosha na maajenti/mawakala pamoja na maafisa wa uchaguzi; maajenti/mawakala wa vyama nao waliripotiwa kufukuzwa katika baadhi ya vituo; baadhi ya vijana walivamia vituo vya kupigia kura wakiwa na lengo la kuzua ghasia; vyama vya siasa vilishutumiwa kuingilia tume hiyo; sanjari na kuharibika kwa Kura hususan zile kutoka Pemba.

Sehemu ya Maazimio ya CUF
Toka kipengele cha tatu (3): KWAMBA, Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi linatoa wito kwa Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao na ambao wanaamini katika utawala wa sheria, demokrasia na kuheshimu Katiba na Sheria za nchi yetu kutoshiriki katika uchaguzi huo usio halali wa marudio.

Toka kipengele cha nne (4): KWAMBA, sababu kuu ya Baraza Kuu kufikia maamuzi haya ni kutokana na matamko yote mawili ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, kutokuwa halali na kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Namba 11 ya mwaka 1984.

Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio.

Kauli ya Waziri mwenye Dhamana
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba aliliripotiwa kusema haya kuhusiana na uhalali wa kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar:
“Hakuna mwenye uhalali kikatiba wala mahakama yoyote inayoweza kupingana na Tume kwa kuwa Katiba ya Zanzibar imeipa meno ya kufanya hayo ambayo yalifanyika,” alisema Makamba.
Na kwamba, uchaguzi huo ulifutwa kwa kutumia Katiba ya Zanzibar Ibara ya 119 inayoipa Tume, (ZEC), uhuru mkubwa wa kuamua, pamoja na Sheria Namba 5 ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo inampa mwenyekiti mamlaka ya kufuta uchaguzi kama ataona kuna dosari. Alitaja dosari nane ambazo ni pamoja na malalamiko kutoka kwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo pamoja na mmoja wa wagombea kujitangazia matokeo.
Hivyo basi, kulingana na kile ambacho kimetangulia kuelezwa hapo juu. Kwanza kabisa, kwa mujibu wa Ibara ya 7(1)-(4) ya Katiba ya Zanzibar ili uchaguzi utambulike kuwa ni halali, ni lazima kanuni, vigezo na masharti yote yaliyoelekezwa na Ibara husika tangulia kutajwa hapo yatimizwe kwa ukamilifu wake. Hii ikiwa na maana kwamba, ili uchaguzi uhesabike/kutambulika ni halali ni lazima uwe ulifanyika kwa kuzingatia na kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria. Tofauti na hapo, uchaguzi huo utahesabika kuwa ni batili na si vinginevyo.
Dhana hii pia inaweza kuonekana kupitia Kifungu cha 39(1)-(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Na kama haitoshi, kwa mujibu wa Ibara ya 28 ya Katiba ya Zanzibar. Ili kupata tafasiri sahihi ni lazima masharti ya Ibara husika yatazamwe kwa upana wake bila ya kuyatenganisha, lengo na dhumuni likiwa ni kupata tafasiri sahihi ya uwepo wa Ibara yenyewe katika Katiba ya Zanzibar.
Kwa kuanza na sharti la kwanza linalosema: kutoka Ibara ndogo ya kwanza (1), ... mtu ataendelea kuwa Rais mpaka Rais anayefuata atakapo kula kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar. Na ile Ibara ndogo ya pili (2), ambayo inasema: Kufuatana na maelezo ya kijifungu (1) cha kifungu cha 28, Rais ataacha madaraka yake mara baada ya kumalizika miaka mitano...
Muhimu: Uwepo wa maneno: "kufuatana na maelezo ya kijifungu (1) cha kifungu cha 28..." inaonyesha dhahiri kwamba, ili kupata tafasri sahihi ya Ibara husika ni lazima masharti yote toka Ibara zote ndogo mbili yasomwe kwa pamoja.
Sanjari na Ibara ya 31(1) ..., mtu anayechukua Madaraka ya Urais, kabla ya kuanza wadhifa huo, atakula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kazi kama kitavyowekwa na Baraza la Wawakilishi....
Kwa kulingana na tafasri inayopatikana hapa, ni kweli kabisa Dk. Ally Mohamed Shein toka ale kiapo cha uaminifu na kiapo cha kazi mwaka 2010 tayari miaka mitano imeshapita. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ndogo ya pili (2). Lakini, kwa mujibu wa Ibara ndogo ya kwanza (1), Dk. Shein anapata uhalali wa kuendelea kuiongoza Zanzibar. Hii ni kutokana ukweli kwamba, mara baada ya Tume, (ZEC), kufuta uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, hali hiyo imepelekea kutofanyika zoezi lolote la kiapo cha uaminifu na kiapo cha kazi anachotakiwa kuchukua/kula mshindi wa uchaguzi wa Rais kwa mujibu wa sheria.
Vile vile, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, (ZEC), kwa mujibu wa Ibara ya 119(9) ya Katiba ya Zanzibar, kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake, itakuwa ni Idara inayojitegemea na mtendaji mkuu wake atakuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na kufanya kazi kwa mujibu wa masharti ya Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
Halikadhalika, kwa mujibu wa Kifungu cha 38(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, (The Zanzibar Election Act of 1984), inaipa mamlaka kamili Tume, (ZEC), ya kuteua siku itakayofanyika uchaguzi wa Rais kwa majimbo yote. Na tena haishii hapo tu.
Kwa mujibu wa Kifungu chake kidogo cha pili (2): Tume, (ZEC), inaweza kupanga siku tofauti ya kufanyika kwa uchaguzi wa Rais kwa majimbo tofauti na hata inapobidi kutengua maamuzi yake, yenyewe, kuhusiana na uteuzi wa siku ya kufanya uchaguzi wa Rais na kisha kupanga siku nyingine tofauti na ile ya awali.
Kwa mantiki hiyo basi, kama Sheria inaipa mamlaka Tume, (ZEC), kuwa huru na kufanya kazi zake kwa kuzingatia masharti ya Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi, yakiwemo na mamlaka ya kupanga siku ya uchaguzi wa Rais katika mazingira yote tuliyotangulia kuyaona hapo awali, hiyo dhana iliyojengwa ya kuwepo "ukakasi wa kisheria" uliopelekea ujenzi wa hoja kwamba: "Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio" ni dhahiri haina tija kwa mujibu wa Sheria kama inavyoendelea kudaiwa.
Kwani kama Tume, (ZEC), ina mamlaka ya kutengua maamuzi yake, yenyewe, kuhusiana na uteuzi wa siku ya kufanya uchaguzi wa Rais na kisha kupanga siku nyingine tofauti na ile ya awali kwa ngazi ya majimbo, kivipi basi ishindwe kufuta uchaguzi wote kwa Zanzibar nzima?!