Bashungwa aipongeza DStv kukuza filamu

07Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bashungwa aipongeza DStv kukuza filamu

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amewahakikishia wadau wa sekta zilizo chini ya wizara yake ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha ukuaji thabiti wa sekta hizo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kushoto), akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Jacqueline Woiso.MPIGAPICHA WETU

Bashungwa ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Ofisi za MultiChoice Tanzania - DStv, ziara ambayo ilikuwa na lengo la kufahamu zaidi utendaji wa kampuni hiyo katika kukuza sekta ya sanaa hususan tasnia ya filamu hapa nchini.

Katika ziara hiyo Waziri Bashungwa aliambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa, Dk. Emmanuel Ishengoma na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk. Kiagho Kilonzo.

Akizungumza na uongozi wa MultiChoice Tanzania pamoja na baadhi ya wazalishaji wa filamu nchini, Bashungwa ameipongeza Kampuni ya MultiChoice kupitia chaneli zake za DStv kwa kuwa kinara katika kukuza tasnia ya filamu nchini.

Waziri huyo alisema kitendo cha DStv kuwa na chaneli maalum kwa ajili ya maudhui ya Tanzania – Maisha Magic Bongo, ni ishara tosha kuwa kampuni hiyo inatilia maanani maudhui ya ndani na kwamba serikali iko tayari muda wote kutoa ushirikiano unaohitajika kwa wadau ili kuhakikisha kuwa tasnia ya sanaa nchini inakuwa chanzo muhimu cha ajira na kukuza uchumi kwa ujumla.

Aidha, Bashungwa alikemea vikali vitendo vya uharamia wa maudhui (content piracy) na kusema kuwa atashauriana na mamlaka na idara nyingine zinazohusika ili kuhakikisha kuwa suala hilo linashughulikiwa.

Bashungwa pia amekiagiza Chama cha Haki Miliki Tanzania (COSOTA), kuhakikisha kuwa wanaongeza nguvu katika mapambano dhidi ya uharamia wa maudhui na wote wanaobainika kufanya vitendo hivyo wachukuliwe hatua kali.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Jacqueline Woiso, alitoa shukrani za kampuni hiyo kwa wizara na waziri binafsi kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa kampuni hiyo na kwamba kitendo chake cha kufanya ziara hiyo ni ishara tosha kuwa serikali inaheshimu sana mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya sekta ya habari nchini.

Woiso amemhakikishia waziri huyo na Watanzania kwa ujumla kuwa, DStv itaendelea kuimarisha maudhui ya Tanzania katika chaneli zake huku ikihakikisha kuwa inatoa mchango mkubwa katika uboreshaji na uimarishaji wa maudhui ya ndani ili yawe katika viwango vya kimataifa na kuweza kushindana katika soko la maudhui.