K2GA afunguka ukimya Kings Music

05Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
The Guardian
K2GA afunguka ukimya Kings Music

​​​​​​​MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Karim Zuberi, maarufu kama K2GA, ametoboa siri ya wasanii kutoka 'lebo' ya Kings Music, kutotoa nyimbo mara kwa mara.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, msanii huyo ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa 'Ndombolo', alisema wasanii wote wa kundi lao wamezoea kukaa kimya kwa kuwa hawafanyi kazi kwa kukurupuka.

"Kwanza, nishazoea halafu ninaelewa mipango ya uongozi wetu ipoje. Kwa hiyo, haina haja hata kama tukikaa sana lakini tukitoa nyimbo zinabamba," alitamba.

K2GA pia alifichua siri za bosi wake, Ali Kiba kutoa nyimbo mbili mfululizo, akisema kumetokana na ukubwa wake na uwezo wa kufanya hivyo.

Ali Kiba ameahidi kutoa nyimbo bandika bandua, akitekeleza hilo kwa kuanza na 'Ndombolo' ambao K2GA ameshiriki, kisha siku chache baadaye akaachia ‘Salute’.

Kauli hiyo ya K2GA imetoa ishara kwa Kings Music kubadilisha mfumo wao wa kazi, pengine kutokana na lawama zilizoelekezwa kwao na mashabiki kukaa muda mrefu bila kuachia ngoma mpya.