Diamond, Wiz Khalifa jikoni kuachia albam

07Jul 2021
WAANDISHI WETU
Dar es Salaam
Nipashe
Diamond, Wiz Khalifa jikoni kuachia albam

MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul, maarufu Diamond Platnumz, yuko Marekani kwa ajili ya kutengeneza albamu yake mpya, akimshirikisha msanii mkali Wiz Khalifa.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram jana, Diamond aliweka picha  yake akiwa na Wiz khalifa, ikisindikizwa na ujumbe uliosomeka "Wasafi × Taylor Gang".

Miaka sita iliyopita, Wiz Khalifa, msanii anayekimbiza kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa na wafuasi wengi zaidi duniani, aliachia 'ngoma' aliyoiita 'See You Again' ambayo ilitazamwa na takribani mara bilioni tano kwenye mtandao wa YouTube.

Mbali na picha ya Wiz Khalifa, siku nne zilizopita, Diamond aliweka kipande kifupi cha video kwenye mtandao wa Instagram akiwa studio na msanii Busta Rhymes na baadaye alionekana kwenye picha na mtayarishaji wa muziki, Swizz Beats, mume wa msanii mkali Alicia Keys.

Julai 3, mwaka huu, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond alitangaza kuwa Rapa Swae Lee atahusika pia kwenye albamu yake hiyo anayoisuka.