Tuipende nchi tuache ushabiki

19Jun 2016
Ibrahim Mkamba
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Tuipende nchi tuache ushabiki

BAADA ya makala yenye kichwa cha habari “Msaliti wa CCM ni Wabunge Wake” iliyochapishwa na gazeti hili Jumapili Juni 5, 2016, kuna msomaji alinitumia ujumbe huu ninaopenda kuwashirikisha wasomaji:

“Hizo ni nasaha au ulitaka utuonyeshe itikadi yako? Unaonaje ukaacha huko kuandika vitu kama hivyo ukabaki unapiga debe la Ukawa bila mafanikio. Kama Ukawa wana watu na CCM hawana kinawashinda nini kuchukua ushindi? Upuuzi mfanye nyie lawama kwa CCM.

Hata kutaja CCM sasa tupumzike uchaguzi ndiyo unaotupa suluhisho kuwa wananchi wengi wana imani na chama gani baada ya kushindanisha sera.

Ijulikane kuwa si busara kukosa kuheshimu demokrasia hata kama wapo wenye uroho na nafasi ya kutawala. Fahamu serikali inaendeshwa na wataalam wenye weledi wa fani mbalimbali si kama sie tunaokosoa kirahisi katika vigazeti.”

Licha ya kuheshimu maoni yake, msomaji amekosea kuniweka kundi la Ukawa ambalo simo, sijawahi na wala sifikirii kuwa huko. Ameniweka huko kwa sababu ya kutoa nasaha kwa CCM kwamba yanayotendeka bungeni yanaongeza umaarufu wa upinzani na kupunguza ushabiki wa watu kwa CCM. Nasaha ililenga kuiasa CCM kujitazama kwenye kwa maslahi yake na kwa mustakabali wa nchi. Hiyo imemfanya msomaji anione Ukawa.Wakati mimi ni mwana CCM lakini zaidi Mtanzania.

Kwa kuamini kwamba mtazamo wa msomaji huyo kunihusu unaweza kuwa ndani ya akili za wasomaji wengi, nimeona ni busara wiki hii nijiweke wazi ili huko mbele tujadili nasaha zangu badala ya uanachama wangu kwa vyama.

Nilijiunga na CCM Oktoba 4, 1982, chama hicho kikiwa na miaka mitano na miezi minane kasoro siku moja kwani siku iliyofuata, Oktoba 5, 1982 kilitimiza miaka mitano na miezi minane.

Nilikuwa mwanachama mtiifu wa CCM kwa miaka 10 mpaka mwaka 1992 nilipoingia jeshini na kuondolewa kwenye uanachama wa chama cha siasa kwa mujibu wa sheria.

Nilimaliza utumishi wa jeshi tarehe 31/12/2004. Baada ya tafakari, nikaona ilikuwepo haja ya kujumuika na wengine ndani ya chama cha siasa ili nipate jukwaa rasmi la kuzungumza kuhusu nchi yangu. Kuanzia mwaka 2005 nikavitazama vyama vya siasa na kujiuliza endapo nirudi CCM au nijiunge na chama cha upinzani.

Miaka sita ya kufanya tathmini ilinifanya nione CCM peke yake kuwa chama chenye mfumo halisi wa kustahili kuwa chama.

Vingine niliviona kuwa si vyama kamili kwa sababu ndani yao walikuwamo baadhi ya watu fulani ama mmoja mmoja waliokuwa maarufu zaidi ya muungano wa watu wengi. Hapo ndipo nilipoamua kurudi CCM kuanzia tarehe 18, Novemba, 2011. Tawi langu ni Kigogo, Kinondoni Dar-es-Salaam na namba ya kadi yangu ni AE. 4995024. Kwa hiyo msomaji wangu na wengine mimi si Ukawa leo, sikuwa hivyo jana na sitazamii kubadilika kesho.

Pamoja na kuwa mwanachama wa CCM lakini nimekuwa Mtanzania zaidi na kwa maana hiyo sitaunga mkono mambo yoyote ya mwana CCM yeyote yenye madhara kwa taifa.

Kwa upande mwingine, nitaunga mkono kwa nguvu zote hoja ya msingi ya kujenga nchi itakayotolewa na mtu asiye mwana CCM. Mimi ni CCM lakini si shabiki wa watu wa chama hicho kwa sababu najua ushabiki ni hasara.

Ushabiki huwa hauoni wala hautaki kuona, hausikii wala hautaki kusikia upungufu wa wale wanaoshabikiwa. Ni kuunga mkono na kutetea tu kwa kila jambo! Mtu akisema serikali ina ubadhirifu na rushwa hata kwa maelezo ya ushahidi mkubwa kiasi gani, shabiki atamlaani aliyesema hivyo na atatoa utetezi mzito kwa sababu tu serikali inaundwa na chama anachokishabikia na viongozi wa serikali ni watu anaowashabikia!Hapo nguvu ya umma ya kuiamsha serikali inakosekana, ubadhirifu na rushwa vinageuka kuwa utamaduni.

Tumeshindwa kupata maridhiano ya kuandika katiba kutokana ushabiki usio na maana wa kila upande kutaka upata yote! Maridhiano ya namna gani hayo. Leo tunakosa bunge makini kwa sababu ya huo huo ushabiki; eti Naibu Spika anawachukia na eti wapinzani wana dharau.

Kwa nini usitafutwe ufumbuzi baina ya “wenye chuki” na “wenye dharau?” Huu ni ushabiki usio na maana.

Unafurahishwa na nini bunge linapojadili mambo mazito bila kujali wachangiaji makini wengi hawapo kwenye mjadala? Unaachaje kumkemea mwakilishi aliyetengeneza mazingira ya kutoshiriki mijadala mizito? Huu ni ushabiki usiojenga.

Upande mmoja umesema unasusia vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika. Kwa kete hiyo ule wa pili unapanga mijadala yote mizito aiongoze kiongozi huyo ikiwa njia ya kuuondoa upande mwingine. Hii yote ni nini kama si ushabiki usio na tija? Ilipoamuliwa wasusiaji wanyimwe posho, wengine tulio nje tulishangilia! Wale wasiosusa wanaopata posho zao zinatusaidia nini sisi tunaoshangilia ushabiki?

Kwa maendeleo ya nchi, tuache ushabiki unaoweza kuligawa taifa. Tuvumilie pale tunaowashabikia wakisemwa kwa faida ya nchi.Tuwe Watanzania zaidi ya watu wa vyama.