Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoadhimisha siku hiyo kwa lengo la kuifanya jamii itambue umuhimu wake na kuchukua hatua za uhifadhi.
Kaulimbiu ya siku hiyo nchini mwaka huu ni 'Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa Letu,' imetokana na kukithiri uharibifu wa vyanzo hivyo nchini.
Tathmini ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), imebaini katika miaka 15 ijayo, vyanzo vikuu vya maji viko hatarani kutoweka, iwapo hakuna hatua zinazochukuliwa.
Mito mikubwa ambayo pia ni vyanzo vikubwa vya maji kama vile Pangani, Ruaha, Rufiji, Ruvu, Wami na mingineyo inaelezwa kuwa katika hatari hiyo.
Uharibifu katika vyanzo hivyo, unatokana na shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi.
Kilimo, ukataji miti hovyo, uchomaji misitu ya asili, matumizi makubwa ya nishati ya mkaa na hasa kwa wakazi wa mjini, ni miongoni mwa mambo yanayochangia uharibifu wa mazingira kitaifa.
Inaelezwa kwamba, kila mwaka kuna ekari milioni moja za misitu inayo, jambo linaolosababisha mvua kupungua, ukame, mafuriko na joto kuongezeka.
Taarifa hizo zinasema kuwa, asilimia 10 ya joto hivi sasa limeongezeka, hivyo kushusha asilimia mbili ya ya pato linaloitegemewa kutoka sekta ya kilimo.
Uharibifu wa mazingira unaathiri sekta zote katika uchumi, ikiwamo ufugaji, uvuvi, utalii, nishati, kilimo, maji na afya.
Ili kukabiliana na nchi kugeuka jangwa, hali iliyokwishachukua sura kwa asilimia 61 katika baadhi ya maeneo ya nchi, hali hii imekwishajitokeza hasa kwa mikoa ya kanda ya kati, hatua na mikakati ya muda mfupi na mrefu inahitajika.
Mikakati ya serikali
Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, mkakati wa serikali ni kupanda hekta zaidi ya 185,000 ya miti kila mwaka katika mfululizo wa miaka 17 ijayo.
Jingine ni haja ya kutolewa elimu kuhusu utunzaji mazingira katika jamii, pamoja na kutumika sheria ndogo ndogo za halmashauri kupambana na wanaokinzana nayo kinyume.
Aidha, katika bajeti inayoendelea kujadiliwa bungeni, imetengwa fedha Sh. bilioni mbili kwa ajili ya mkakati wa upandaji miti kitaifa.
Pia, mkakati huo wa muda mrefu na kuanzia mwaka huu hadi 2021, unatarajiwa kutumia Sh. bilioni 105.2 kwa ajili ya upandaji miti.
Matumizi ya nishati mbadala yanasisitizwa na wataalamu, ili kuchukua nafasi ya mkaa unaoharibu mamilioni ya ekari kila mwaka.
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, inasema kuanzia Januari Mosi mwakani, ni marufuku kutumia mifuko ya plastiki. Lengo ni kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.
Utengenezaji, uuzaji, usambazaji, na uagizaji wea bidhaa ya plastiki kutoka nje, pamoja na utumiaji mifuko ya plastiki itakuwa marufuku. Hiyo inagusa hadi mifuko inayohifadhi baadhi ya vinywaji vikali.
Mtazamo huo wa serikali unatarajiwa kuhalalishwa, baada ya kikao cha bunge kuu Septemba mwaka huu na marekebisho Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
Mifuko ya plastiki inaelezwa kuchafua zaidi mazingira hasa katika vyanzo vya maji, fukwe za bahari na maeneo ya wazi hususan mjini kwani mifuko hiyo haiozi.
Ingawa watengenezaji wa mifuko hiyo nchini wataruhusiwa kuuza bidhaa yao nje ya nchi, bado kuna tahadhari inatolewa kwamba, wazalishaji wajiandae kukabiliana na mbadiliko ya kiuchumi.










