Tume ya Dawa za Kulevya katika mtihani wa ‘jipu lisilotumbuka’

09Jun 2016
Efracia Massawe
Dar es Salaam
Nipashe
Tume ya Dawa za Kulevya katika mtihani wa ‘jipu lisilotumbuka’

Tathimini katika mikoa mbalimbali nchini zinaonyesha watumiaji wakubwa wa dawa hizo, ni vijana wenye kati umri wa miaka 20 na 38.

Wengi wanadaiwa kutumia bangi, dawa inayozalishwa kwa siri katika mikoa mingi nchini na kuna nyingine zinazoigizwa kutoka nje ya nchi.

Pia kuna dawa zinazoingizwa kutumiwa na kundi hilo ni heroin, mirungi na cocaine, ambazo mbali na kuharibu kundi kubwa la vijana tegemezi, imesababishia kundi hilo kujikuta tegemezi na wengine kuingia katika matukio ya kikatili.

Kuongezeka usafirishaji wa heroin kupitia nchi za Afrika Mashariki, kumechangia matumizi ya dawa hiyo nchini kutokana na kundi la wafanyabiashara kuendelea kuziingiza.

Dawa hizo zinaelezwa kuwa hatari kwa afya za binadamu na watumiaji katika nchi za Amerika Kaskazini, ndio wanaongoza kufa kutokana na dawa za kulevya, hasa kwa kuzidisha kiwango cha kemikali hizo.

Nchini Colombia, kunaelezwa kwamba kilimo cha cocaine kimeongezeka kwa asilimia 44 mwaka juzi, tofauti na mataifa yalioyobobea kwa matatizo hayo, kama vile Bolivia na Peru, ambako janga hilio sasa linapungua.

Inaelezwa kimataifa kwamba, katika eneo la Asia Kusini, kuna ongezeko la utengenezaji, usafirishaji na matumizi makubwa ya dawa za kulevya, jambo ambalo ni hatari kwa vijana wa nchi hiyo.

TANZANIA
Ikiangaliwa nchini Tanzania, matokeo ya utafiti aina mbalimbali yanaashiria watumiaji wa heroin wanakadiriwa kuwa kati ya 200,000 na 425,000 na katika kundi hilo, 30,000 wanatumia dawa hiyo kwa njia ya kujidunga.

Ofisa Elimu wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Moza Makumbuli, anasema viashiria hivyo hutumika kuonyesha ukubwa wa tatizo dawa za kulevya nchini.

Anataja kiasi cha heroin kilichokamatwa nchini kuanzia mwaka jana hadi Aprili mwaka, huu ni kilo 53.49 na cocaine kilo 86.2.

Makumbuli anataja kiasi bangi iliyokamatwa nchini mwaka juzi ni tani 81.3 na mirungi tani 15.7.

Ofisa huyo anasema watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na usafirishaji wa dawa hizo wako 14,503.

“Takwimu hizi zinaonyesha sio tu ukubwa wa usafirishaji wa heroin na cocaine, bali matokeo ya jitihada zilizoelekezwa kukabiliana na biashara haramu katika kipindi husika,” anasema Makumbuli.

SHERIA MPYA
Anasema moja ya jitihada za serikali katika kukabiliana na tatizo hilo ni kutunga Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka jana, ambayo imeanza kutumika rasmi.

“Sheria hiyo inafuta Sheria Namba Tisa ya Mwaka 1995,. iliyokuwa na mapungufu na imeweka adhabu kali kwa makosa ya kujihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya,” anasisitiza Makumbuli..

Anafafanua kuwa, sheria hiyo mpya imeharamisha baadhi ya vitendo ambavyo havikuwepo kwenye sheria iliyofutwa na kuweka adhabu kali ya kifungo cha maisha au adhabu ya kifungo cha miaka 30 na faini ya Sh. mil. 200, kwa kumiliki mitambo ya kutengeneza dawa hizo.

Makumbuli anasema katika adhabu ya miaka 30, inamuanguki anayetiwa hatiani kuhusika na kosa la kushawishi watoto kuingia kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya, wakati sheria iliyofutwa ilikuwa kimya kuhusu suala kosa hilo.

Anafafanua kuwa, ni sheria inayofafanua kuwapo adhabu ya kifungo cha maisha faini ya Sh bilioni moja, watu wanaothibitika kufadhili biashara hiyo, ambao wana kipato cha ‘matajiri’. Hata hivyo hakufafanua ‘kipato cha matajiri.’.

Kutokana na kuwatia mbaroni na hatimaye hatiani mikononi mwa mamlaka za kisheria, kwa kukithiri wimbi la dawa hizo haramu duniani, serikali ya Marekani Machi mwaka huu ilitaifisha mali za mfanyabiashara wa dawa za kulevya kutoka Tanzania.

Pia ilipiga marufuku kampuni za nchi hiyo kujihusisha na biashara zake za aina yoyote.

Mfanyabishara huyo anamiliki mali nyingi, zikiwamo maduka ya kubadili fedha za kigeni (bureau de change), kampuni za ulinzi, nyumba na utitiri wa magari.

WAATHIRIKA WANAOTIBIWA
Hivi sasa, baadhi ya waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya, wanapatiwa katiba baadhi ya vituo na hospitali za kuwahudumia, ikiwamo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MH).

Miongoni mwa waathirika wanaohudumiwa, ni Horun Abubakar (32), mkazi wa Kinondoni kwa Manyanya, jijini Dar es Salaam, ambaye ana maini yake kadhaa.

Anasema, kitendo cha serikali kushindwa kutoa takwimu kwa ufasaha ni miongoni mwa sababu inayochangia kuongezeka matumizi ya dawa hizo.

Hata hivyo, takwimu za serilkali zinabainisha kuwa tangu Juni mwaka jana, hadi mwezi Aprili iliyopita, kulikuwapo watumiaji wa heroin kati ya 200,000 na 425,000 nchini nzima, kiwango kinachodaiwa hakionyeshi ama kupungua au kupungua.

Inaelezwa kuwa, jumla ya watumiaji wa heroin wanaopata matibabu kwa kutumia tiba ya dawa za methadone hadi kufikia mwezi Mei mwaka jana walikuwa 2,300 tu. Inadaiwa kuna kiasi kikubwa cha watumiaji ambao hawajajitokeza, hali inayochangiwa na wengi kutojitokeza kwa wingi.

Kupitia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na mamlaka zinginezo, serikali inazitaka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Pwani na Shinyanga, ambazo ni waathirika wakubwa wa dawa za kulevya, kuchukua hatua thabiti kukabiliana na tatizi hilo.

Kwa mujibu wa maagizo hayo, hatua zinazotakiwa ni kuanzisha na kuendeleza huduma za tiba, kama njia ya kukabiliana na wagonjwa.

Serikali katika nafasui yake, inawashauri viongozi wa mikoa na wilaya nchini kote, wafuatilie kwa makini mwenendo wa ongezeko la matumizi hayo, kama chachu katika utendaji wao wa kazi.

Infafanuliwa kwamba, hiyo itafanyika katika namna yakuwasilisha hoja hizo ndani ya Kamati za Ulinzi na Usalama za ama mikoa au wilaya, ambazo suala hilo ni miongoni mwa agenda ya kudumu katika vikao vyao.