SIDO yaibuka na viwanda kuyapa thamani mabunzi na vifuu

10Jun 2016
Restuta James
Dar es Salaam
Nipashe
SIDO yaibuka na viwanda kuyapa thamani mabunzi na vifuu

AMINI usiamini, huu ndio ukweli. Kwamba mhindi, mgomba, mhanzi, kifuu cha nazi na mazao mengineyo, ni kiwanda kinachojitegemea kabisa.

Naamini dhana ya kifuu cha nazi siyo ngeni. Wapo watu wametumia dawa ya mbu iliyotengenezwa kwa kifuu.

Mathalani katika mhindi utapata unga, majani ya ng’ombe na kikapu cha kuendea sokoni; japo nitaje faida zake kwa uchache.

Kwenye nazi utapata kiungo cha mboga (tui). Utaweza kutengeneza mafuta ya kupakaa, kuni (kifuu chenyewe) na mapambo ya aina mbalimbali, kutegemeana na macho yako yanaona fursa gani kwenye zao husika.

Unajiuliza inawezekanaje? Wengi wetu tunafahamu kuwa ukilima mahindi kwa sehemu kubwa unategemea kupata chakula cha familia, kuuza kwenye viwanda vinavyosaga na kufungasha unga na pengine kwa ajili ya majani ya mifugo.

Ukweli ni kwamba, fursa iliyopo kwenye zao kama mahindi ni zaidi ya hapo. Unaweza kutengeneza kikapu au chombo kizuri sana na cha kudumu kwa ajili ya kuhifadhia vitu nyumbani.

Meneja wa Shirika la Viwanda Vidogo (Sido), mkoa wa Dar es Salaam, Francisca Simon, anasema katika shirika hilo, kuna mafunzo ya kijasiriamali yanayotolewa kila mara ili kuwajengea uwezo wajasiriamali.

Mafunzo hayo anasema yanatolewa pamoja na mbinu mbalimbali za kibiashara kuanzia utengenezaji wa sabuni, uokaji wa mikate, namna ya kufungasha bidhaa na kutafuta masoko.

“Tunao wataalamu wa kuwajengea wananchi uwezo pia tunafanyakazi kwa karibu sana na taasisi nyingine za serikali kama TBS (Shirika la Viwango Tanzania), ili kuthibitishiwa ubora,” anasema.

Sido pia inashirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara (Brela) na kuwaelimisha wajasiriamali namna ya kusajili biashara na faida zake.

Aidha, miongoni mwa mafunzo ya SIDO ni pamoja na kuwatembelea wajasiriamali kwenye maeneo yao ya biashara ili kuwapa ushauri panapokuwa na mapungufu au kuwapendekeza kwa TBS kwa ajili ya kupewa kibali cha kupewa alama ya ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Katika mpango huo, maofisa wa Sido wamekuwa wakiwatembelea wajasiriamali mara mbili kwa wiki.

Meneja wa mradi wa Vinywelea Asilia (natural fibers centre), katika Shirika hilo, January Melkiado, anasema fursa za kuanzisha viwanda vidogo ziko kila mahali nchini, isipokuwa ni watu kuziona na kuzifanyia kazi.

Katika mradi huo ulioanzishwa mwaka 2004, meneja huyo anasema ulikuwa ukiitwa Bamboo fiber centre, lakini kutokana na kupanua wigo wa malighafi zilizopo kila mahali nchini, walilazimika kuufanya wa kitaifa.

Nje ya ofisi za mradi huo utakuta mazao kama migomba, katani, mianzi, mahindi na mengineyo, kama ishara kwamba mbali ya fursa za wazi kama chakula kwenye baadhi ya mazao, kuna ujasiriamali ndani yake.

Melkiado anasema, kinachofanyika kwenye mradi huo ni kuwafundisha wajasiriamali mbalimbali namna wanavyoweza kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao kuzalisha bidhaa zinazohitajika.

“Malighafi kubwa tunayotumia ni mianzi, hanzirani, katani, majani ya migomba, ngozi, mabaki ya nazi, majani ya mahindi na nyinginezo zinazofanana na hizo,” anasema Melkiado.

Anafafanua kuwa: “Malighafi hizi zinapatikana popote nchini kuanzia Dar es Salaam hadi Mbeya, Dodoma hadi Kigoma, Bagamoyo hadi Kilimanjaro. Inategemea tu kwenye mkoa husika kuna mazao gani.”

Mtaalamu huyo anasema kwa kutumia mianzi mjasiriamali anaweza kutengeneza samani za ndani kama meza (ya chai, kujipambia-dressing table), viti, stuli na makochi.

Mjasiriamali anaweza pia kutengeneza mapambo ya ndani na nje, masinia hasa ya kutoa huduma kwenye migahawa, viti vya baa, masanduku ya zawadi (gift boxes), mazulia, stendi za televisheni au radio na ‘ndoo’ za kuwekea takataka (dustbin), pamoja na nyinginezo kulingana na mahitaji ya mteja.

Anasema kituo hicho kinatoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa hizo, wakiwalenga zaidi vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Melkiado anasema wadau wao katika kutekeleza mradi huo ni wakulima na vyama vinavyowasaidia wakulima, wajasiriamali wadogo na wa kati walio katika eneo lenye rasilimali, waendelezaji wa biashara, watafiti na taasisi za kitafiti, wizara na halmashauri mbalimbali pamoja na wafadhili na wadau wa maendeleo.

MALENGO MAHUSUSI
Anasema nia ya kuanzishwa kwa mradi huo ni kutoa elimu na ujuzi wa matumizi ya malighafi asilia ili kutengeneza fursa za kibiashara na kuzalisha ajira zitakazopunguza umaskini katika jamii husika.

“Lengo lingine ni kutengeneza fursa za kiuchumi kwa kutumia malighafi zisizohitaji gharama au teknolojia kubwa, kutafuta masoko ya ndani na nje ya bidhaa za asilia na kujenga mtazamo wa kijasiriamali kwa wananchi,” anasema.

Aidha, katika kuanzisha mradi huo, SIDO imelenga kutengeneza kipato kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na kazi za mikono na kuchochea ubunifu na mbinu za kibiashara.

Mbali ya Dar es Salaam, mradi wa Vinywelea Asilia unatekelezwa pia Njombe ambako kuna ofisi, lakini pia mafunzo kama hayo yanatolewa katika ofisi za Sido katika mikoa mbalimbali.

Mkakati wa Sido kwa mujibu wa meneja mradi huo, ni kusambaza elimu ya matumizi ya vinywelea asilia nchi nzima ili wananchi wajikwamue kiuchumi na kupiga vita umasikini.

“Napenda tu kusisitiza kuwa malighafi zipo za kutosha na ni rahisi kutengeneza bidhaa kadha wa kadha kwa hiyo wajasiriamali waone hizi fursa,” anasema.