Hayo ni maneno ya msichana Ngolo Katabi (16), mzaliwa wa kijiji cha Ugala wilayani Mpanda, ambaye anapatiwa matibabu baada ya kupata ugonjwa wa fistula katika hospitali ya CCRBT jijini, Dar es Salaam.
Anafafanua zaidi: “Nilikataa, akachukua miguu yangu kwa lazima na kuitumbukiza ndani ya kile chungu. Nilipata maumivu makali sana na kuungua miguu, lakini hakujali”.
Ngolo ambaye ni mtoto wa Mzee Katabi Lubinza, anasema hajawahi kupelekwa shule na hivyo hajui kusoma na kuandika hadi sasa.
Kwa nini yuko CCBRT kwa tiba ya fistula? Ngolo anaendekeza simulizsi kwa kusema: “Niliolewa mwaka juzi na Mzee… (jina tunalihifadhi) ambaye ni mganga wa kienyeji, kwa mahari ya ng’ombe watano. Sikupenda kuolewa naye, alinirubuni nikiwa machungani.
Alikuja na kuniambia kuwa ananipenda na atanipa pesa nyingi, lakini nisizitumie hadi akija kunioa niende nazo kwake, nami nilifanya hivyo.”
Msichana huyo anaendeleza simulizi kuwa anatokea katika jamii ya wafugaji na kiasi cha pesa alichorubuniwa na mganga huyoni Sh. 50,000 na baadaye alitoa mahari na kumuoa, lakini walipofika nyumbani kwake alimnyang’anya zile pesa.
Ngolo ambaye ana makovu miguuni, kutokana na kuunguzwa na maji ya moto, anasema kabla ya kuolewa na mganga huyo, alikuwa hajawahi kukutana kimwili na mwanaume.
Anasema siku ya kwanza alipokutana kimwili na mwanaume huyo akiwa kwenye ndoa, mkewe alikuwa anashuhudia na kufurahia tendo hilo.
Anasema baada ya mwezi mmoja, alipata ujauzito na katika kipindi chote cha ujauzito, alikuwa akipata mateso makali, kwani mke mwenziwe hakumtaka asilale wala kupumzika, badala yake afanye kazi.
Kwa mujibu wa Ngolo, mwanamke huyo alimtakia kwamba kuchapa kazi huko ni sehemu ya kurudisha mahari ya ng’ombe iliyotumika katika ndoa yake.
“Siku niliyopata uchungu wa kujifungua, niliwaambia lakini wakasema ninadeka na hivyo waliniacha niendelee kuumia, hadi siku ya tatu ndipo huyo babu ambaye ni mume wangu alichemsha maji, akaweka kwenye chungu akasema ameweka dawa.
“Halafu akasema nitumbukize miguu! Niliogopa kwani yale maji yalikuwa ya moto sana, lakini alinikandamiza kwa dakika kumi hivi, huku akisema nikiungua nitasukuma mtoto kwani, nashindwa kujifungua kwa sababu nina deka,” anasimulia Ngolo, akiwa wodini CCBRT.
Msichana huyo anasema baada ya hapo, alijifungua kwa shida mtoto aliyekufa, ambaye alizikwa na mume huyo mganga na mke mwenza na baada ya tukio hilo walimpigia simu baba yake amchukue, kwani alionekana ana hali mbaya.
“Baba aliuza ng’ombe akanipeleka Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, ambako nilitibiwa miguu na baadaye nilionekana nina ugonjwa wa kuvuja mkojo na haja kubwa, vyote kwa pamoja.
SAFARI YA CCBRT
“Kulikuwapo balozi wa CCBRT huko Mpanda, aliyeitwa Dk. Peter. Yeye alishauri nipelekwe CCBRT. kwani alidai ugonjwa huo unaitwa fistula na unatibiwa bure katika hopstali hiyo iliyoko Dar es Salaam.
Ngolo anasena ni mchakato ambao hakuwa na gharama yoyote. Kila kila kitu aligharamiwa na hospitali hiyo, ikiwamo nauli, chakula na hadi sasa anaendelea kuhudumiwa kwa mfumo huo akisubiri kufanyiwa upasuaji karibuni.
Muuguzi na Mwangalizi wa Kinamama Kisaikolojia Wanaogua Fistula katika hospitali hiyo, Teodora Milinga, anasema huwa anawapokea wanawake wa namna hiyo walioathirika kisaikolojia na kuwasaidia warudie saikolojia yao ya kawaida.
“Ngolo alikuja hapa mwezi mmoja uliopita na baada ya vipimo amegundulika ana fistula zote mbili na hivyo hapa anasubiri kufanyiwa upasuaji,
“Tunamuandaa kisaikolijia. Kwanza, ili arejee katika utu wake na kujiona naye ana thamani katika jamii, kwani wengi wanapokuja hapa wanakuwa wameathirika kisaikolojia kutokana na kutengwa na jamii na kutalikiwa, baada ya kuamini ugonjwa huo ni laana na hauna tiba,” anasema Mama Milinga.
Mwanasaikolojia huyo, alitoa maelezo hayo alipokutwa kazini katika kipindi na kinamama wanaougua fistula, hospitalini CCBRT.
MAISHA YA HOSPITALI
Mama Milinga anataja program zake ni za kukaa na magonjwa na kuwabadili, ili kuwaleta karibu ili kuwaoa matumaini ya kuishi vizuri.
Anasema baada ya kukosa matumaini ya kuishi katika jamii tena, amekuwa akifanya nao vipindi mbalimbali na ataja mfano wa ratina zake, kuwa siku ya Jumanne huwa anawafundisha lishe bora.
Mwanamke huyo anasema kuwa siku ya Jumatano anajifunza kusoma na kuandika, kwani baadhi ya waathirika hawajawahi kwenda shule.
Pia siku hiyo wagonjwa hao kila mmoja huopewa fursa ya kueleza historia binafsi na namna alivyopata fistula na wanaburudika na muziki.
Mama Milinga anasema siku ya Alhamisi, ni mahsusi kwa hujifunza kufuma na Ijumaa anafundishwa kuwa Balozi wa Fistula, pindi atakapopona na kurudi nyumbani.
FISTULA NI NINI?
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na upasuaji wa ugonjwa wa fistula hospitalini CCBRT, Dk. James Chapa, ana ufafanuzi kuhusu ugonjwa huo.
“Fistula ni tundu lisilo la kawaida, kati ya njia ya uzazi na kibofu cha mkojo au njia ya haja kubwa. Tundu hili, husababishwa na uchungu wa muda mrefu na uzazi pingamizi wakati wa kujifungua bila ya msaada wa haraka,” anasema Dk. Chapa.
Anasema mama mwenye fistula hutokwa na haja ndogo au kubwa na wakati mwingine vyote kwa pamoja, bila ya kuwa na uwezo wa kujizuia, hali inayomdhalilisha na kumfanya ashindwe kushiriki vyema katika shughuli za kijamii, huku akutengwa na jamii yake.
Mganga huyo anasema kuwa nchini Tanzania, inakadiriwa kuna zaidi ya wanawake 3,000 wanaopata fistula kila mwaka na kati yao.
Anasema katika idadi hiyo, kuna wastani wa wanawake 1000 kila mwaka wanaopatiwa matibabu na kuwaacha takriban wengine 2500 wanaiohangaika ila ya kupata msaada.










